Maridhiano yatajwa kichaka kukwamisha Katiba Mpya

Dar es Salaam. Wadau hao wamesisitiza kuwa mchakato wa Katiba Mpya ni wa kisheria unaohitaji kuanza kwa kuwasilisha muswada wa sharia bungeni, hivyo haupaswi kuhusishwa moja kwa moja na matukio ya hivi karibuni, ikiwemo uchunguzi wa vurugu hizo.

Hata hivyo, wengine wameeleza kuwa hatua zinazopendekezwa zinafanana na kuchomeka mambo ambayo hayahitajiki, hivyo kuweo uwezekano wa kuzuka lawama baadaye, hasa iwapo baadhi ya wadau hawatashiriki katika maridhiano na kuonekana kuwa chanzo cha kukwamisha mchakato huo.

Akizungumza jana Machi 17, jijini Dodoma wakati wa uzinduzi wa programu ya ‘Sema na Waziri’, Dk Homera alisema Katiba Mpya ni kipaumbele cha taifa, lakini utekelezaji wake unahitaji utulivu, umakini na mpangilio wa hatua za kimkakati.

Amesema baada ya kupokelewa kwa ripoti ya Tume, hatua inayofuata ni maridhiano ya kitaifa kabla ya kuanza rasmi kwa mchakato wa Katiba Mpya.

Amesema hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa ilani ya CCM na hivyo akawataka wananchi kuwa na subira.

Akizungumza na Mwananchi leo, Machi 18, 2026, kuhusu kauli hiyo, Mwanasheria na mkurugeniz katika Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Fulgence Massawe amesema mchakato wa Katiba Mpya ni wa kisheria, lakini kwa bahati mbaya umekuwa ukitekelezwa zaidi kwa mtazamo wa kisiasa.

“Mchakato wa kuanzisha Katiba Mpya ulianzishwa kwa mujibu wa sheria, na sheria hiyo ilifikia ukomo wake ilipoingia katika Bunge la Katiba. Mtu yeyote anayezungumzia Katiba Mpya lazima aeleze ni kipengele gani cha sheria kimebadilishwa,” amesema.

Kwa mujibu wa Massawe, hoja ya Waziri Homera kuhusu maridhiano ni jambo lililoibuka hivi karibuni na halikuwepo awali, ilhali kiu na mahitaji ya Katiba Mpya yamekuwepo kwa muda mrefu na ahadi zimekuwa zikijirudia bila utekelezaji.

“Mikutano ya kampeni na ilani za vyama vyote vinataka Katiba Mpya. Huenda matukio ya Oktoba 29, 2025 yalibadili mwelekeo wa utekelezaji wake, lakini bado hilo haliondoi uwepo wa siasa katika kushughulikia na kujibu kilio hicho cha Watanzania,” amesema.

Amesema kwa kuwa Waziri ameshazungumza, ni vyema apewe muda, lakini pia ni muhimu kuweka wazi kama sheria ya kuendeleza mchakato huo tayari imepelekwa bungeni na tume ya maridhiano imeundwa.

“Kusema kuwa Serikali imebakiza hatua moja si sahihi; bado kuna mchakato mrefu. Ni muhimu kuepuka kuwachanganya wananchi na kulifanya suala hili kuwa la kisiasa badala ya kulizingatia kisheria,” amesema.

Amesema suala hilo linatumika kisiasa licha ya kuathiri wananchi na kwamba haoni dhamira ya dhati kwa viongozi waliopo madarakani kuendesha mchakato wa upatikanaji wa Katiba Mpya.

“Maridhiano hayawezi kukamilika ndani ya mwezi mmoja au hata miaka miwili, kwani baada ya hapo tutakuwa tunaelekea katika maandalizi ya uchaguzi mwingine wa 2030. Hili limekuwa suala la kisiasa zaidi kuliko uhalisia,” amesema.

Kauli kama hiyo imetolewa na Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Boniface Mwabukusi, kuwa suala linaloendelea kuhusu tume ya uchunguzi halina uhusiano wowote na upatikanaji wa Katiba Mpya.

“Kusema hivyo ni sawa na kuchukua vipuri vya treni na kuvifunga kwenye gari. Katiba ni mchakato na wananchi wanahitaji ukweli na uwajibikaji, mambo ambayo hayahusiani na hoja hiyo (ya maridhiano),” amesema.

Mwabukusi amesema suala la Katiba tayari lilishajadiliwa na wananchi walishatoa maoni yao kupitia Tume ya Jaji Joseph Warioba, hivyo msingi wa kuanzia bado upo.

“Sehemu ya kuanzia ipo, lakini si kama anavyosema. Binafsi nafikiri hayo ni maoni yake na yanapaswa kuheshimiwa, lakini si hitaji halisi la Watanzania. Watanzania wanahitaji uwajibikaji, hasa katika masuala ya utekaji, upotevu na mauaji,” amesema.

Wakati wasomi hao wa sheria wakieleza  hayo, Profesa wa Elimu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, George Kahangwa, amesema kulingana na mifumo ya nchi, kinachokwamisha na kukushindwa kuanza mchakato wa Katiba Mpya ni nia kutoka kwa Rais na Serikali yake.

 “Hata kama wanalizungumzia, ukweli uliopo ni kwamba hakuna nia na utashi. Rais aliyeko madarakani akisema anahitaji Katiba sasa, mchakato utaanza mara moja; ni bora aseme sasa akiwa bado ana muda,” amesema.

Amesema kama Rais atasema mwishoni mwa kipindi chake, haitakuwa na tija, akitolea mfano kipindi cha Jakaya Kikwete ambapo mchakato uliishia njiani na Katiba haikupatikana. Baadaye alipoingia hayati John Magufuli, suala hilo halikuwa kwenye mipango yake wala halikuwa linazungumzwa.

“Kama ni suala la hatua, si la waziri kusema tu na kuwafanya wananchi waonekane hawaelewi. Tume ya Jaji Warioba ilibainisha hatua za kufuata, ikiwemo kura ya maoni,” amesema.

Profesa Kahangwa amesema hatua anayozungumzia Waziri Homera ni ‘hatua za kuchopeka’, kana kwamba wanaushutumu upande mwingine kwa kukwamisha mchakato wa Katiba iwapo hautaridhia maridhiano.

“Sababu wanazotoa ni njia ya kukimbia mchakato wa Katiba. Kumbuka kulikuwa na kikosi kazi kilichoongozwa na Profesa Rwekaza Mukandala kumshauri Rais kuhusu mageuzi ya kisiasa; katika mambo hayo walishauri pia ni lini Katiba Mpya ipatikane,” amesema.

Amesema kuna mambo mengi yaliyotajwa kwenye ripoti ya Profesa Mukandala na viongozi wanapaswa kutambua kuwa wananchi hawajasahau, kwa kuwa tayari walishamaliza upande wao kwa kueleza wanahitaji Katiba Mpya.

“Utashi wa kumalizia hatua za upatikanaji wa Katiba upo mikononi mwa Rais. Mambo mengine yanayosemwa ni ubabaishaji, ni muhimu kuwahurumia Watanzania kwani wamechoka kuambiwa kana kwamba hawajielewi,” amesema.