Maximo aiombea KMC | Mwanaspoti

LICHA ya kuachana na kikosi cha KMC, kocha Marcio Maximo amesema bado anaiombea dua njema timu hiyo ibaki Ligi Kuu Bara.

Ni wazi kwamba KMC haina msimu mzuri kwani ndiyo inayoshika mkia ikiwa imecheza mechi 16, imeshinda mbili, sare mbili na kupoteza 12 ikikusanya pointi 18.

Maximo ambaye alianza na timu hiyo msimu huu kabla ya kuondoshwa kwa makubaliano ya pande mbili kisha nafasi yake ikachukuliwa na Mohamed Abdallah ‘Bares’, ameliambia Mwanaspoti kuwa, haoni kama alikuwa chanzo cha timu hiyo kutopata matokeo mazuri kwani makosa yalifanyika.

Alisema KMC inaweza kupambana na kusalia Ligi Kuu kama wachezaji wataendelea kuongezewa mbinu na kusaidiwa kisaikolojia.

“Sioni kama nilikuwa chanzo cha timu hiyo kutopata matokeo mazuri kwani makosa yalifanyika wakati unafanyika usajili msimu huu. KMC inaweza kupambana na kusalia Ligi Kuu kama wachezaji wataendelea kuongezewa mbinu uwanjani lakini pia kusaidiwa kisaikolojia,” alisema.

Maximo aliyedumu siku 131  ndani ya kikosi hicho, alikiongoza kwenye mechi tisa za Ligi Kuu Bara, akiambulia ushindi mara moja, vipigo saba na sare moja. Tangu kuondoka kwa kocha huyo, KMC imeshinda mechi moja na sare moja pia, huku ikipotezatano kati ya saba ikiwa chini ya Bares.