Dar es Salaam. Wadau wa elimu wamekutana jijini Dar es Salaam kujadili mbinu za kuboresha ufundishaji na ujifunzaji wa somo la hisabati, wakilenga kuwasaidia wanafunzi kulipenda na kufanya vizuri zaidi.
Mjadala huo uliandaliwa na Taasisi ya Maendeleo ya Elimu Afrika Mashariki ya Chuo Kikuu cha Aga Khan (AKU-IED, EA) jana Jumatatu, Machi 17, 2025 ukiadhimisha Hisabati Duniani (IDM), yenye kaulimbiu, “Hisabati na Matumaini.”
Wadau hao walisisitiza matumizi ya mbinu shirikishi, ubunifu darasani na kuunganisha somo hilo na maisha halisi ya wanafunzi.
Mwanafunzi akichangia hoja katika mjadala uliolenga kutafuta suluhisho za kuboresha ujifunzaji wa somo la hisabati. Picha na Mpigapicha Maalumu.
Katika maadhimisho hayo yaliyofanyika kwa ushirikiano na Young Engineers Tanzania, wanafunzi walishiriki katika shughuli za vitendo zikiwamo kubuni na kujenga madaraja kwa kutumia kanuni za hisabati kama vile uwiano na vipimo.
Lengo lilikuwa kuonyesha namna hisabati inavyoweza kuwa rahisi, ya kuvutia na yenye matumizi ya moja kwa moja.
Akizungumza katika tukio hilo, Mhadhiri wa AKU-IED, EA, Dk Howard Omukami alisema mbinu za kujifunza kwa kushirikiana, mrejesho chanya na ushiriki wa wanafunzi ni muhimu katika kubadili mtazamo hasi kuhusu hisabati.
“Tunajenga jamii ya walimu na wanafunzi wanaojifunza kwa pamoja, tukilenga kubadili mitazamo na kuongeza ufaulu hasa kwa watoto katika ngazi za awali,” alisema.
Naye Naibu Mkuu wa chuo hicho, Dk Nicholas Wachira alisema hisabati ni somo linalohitaji uvumilivu na majaribio ya mara kwa mara.
“Hisabati siyo kuogopa bali ni kujaribu tena na tena hadi ufanikiwe. Pia inaendana na teknolojia na ndiyo msingi wa ubunifu wa baadaye,” alisema.
Wanafunzi wa shule za msingi jijini Dar es Salaam wakifanya kwa vitendo utambuzi wa maumbo wakati wa maadhimisho ya Siku ya Hisabati Duniani (IDM). Semina hii iliandaliwa na Taasisi ya Maendeleo ya Elimu Afrika Mashariki ya Chuo Kikuu cha Aga Khan (AKU-IED, EA).
Mwanafunzi kutoka Shule ya Sekondari Zanaki, Agatha Loman, alisema shughuli za vitendo zimemsaidia kuelewa namna ya kuunganisha hisabati na sayansi katika ubunifu.
“Nimejifunza kubuni daraja nikitumia hisabati. Imenipa hamasa ya kuwa mbunifu,” alisema.
Kwa upande wake, Bernadette Kasuku aliyekuwa mwezeshaji alisema kuona wanafunzi wakishirikiana kulimfanya atambue kuwa kila mtu ana nafasi ya kuchangia kujenga matumaini katika hisabati.
Maadhimisho hayo yalihusisha washiriki zaidi ya 183 kutoka shule nane za msingi na sekondari jijini Dar es Salaam, huku yakihitimishwa kwa maonyesho ya ubunifu ikiwamo matumizi ya mashine ya uchapishaji wa 3D.
Kwa mujibu wa matokeo ya kumaliza elimu ya msingi yanayotolewa na Baraza la Mitihani la Taifa (Necta), zaidi ya asilimia 40 ya wanafunzi hufeli somo la hisabati.
Mwaka 2025 asilimia 43.3 ya wanafunzi walipata wastani wa alama D na F, ikilinganishwa na asilimia 44.9 mwaka 2024. Hata hivyo, kati ya mwaka 2020 na 2022 zaidi ya nusu ya wanafunzi walifaulu kwa kupata alama A, B na C.
