Muelekeo mpya ukusanyaji wa mapato

Dar es Salaam. Tume ya Rais ya Kutathmini Maboresho ya Mfumo wa Kodi imependekeza mabadiliko katika sekta ya kodi, ikiwamo kubadili jina la Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na kuitwa Huduma za Mapato Tanzania (TRS).

Tume hiyo iliyoongozwa na mwenyekiti wake, Balozi Ombeni Sefue, ilianzishwa Julai 31, 2024 na kuanza kazi Oktoba 4, 2024 imekuja na mapendekezo hayo baada ya tathmini kuonesha mfumo wa kodi kuwa na dosari  kadha wa kadha zinazoathiri walipa kodi na mazingira ya uwekezaji.

Akiwasilisha mapendekezo 284 leo Jumatano Machi 18, 2026 wakati wa kukabidhi ripoti hiyo kwa Rais Samia Suluhu Hassan, Balozi Sefue amesema kwenye mageuzi ya sera na sheria, tume imependekeza kuimarishwa kwa mfumo wa kisera na kisheria ili kuweka mwongozo wa kitaifa unaoeleweka na misingi madhubuti ya uandaaji na maboresho ya kodi.

Mwenyekiti wa Tume ya Rais ya Kutathmini Maboresho ya Mfumo wa Kodi nchini Katibu Mkuu Kiongozi Mstaafu, Balozi Ombeni Sefue akizungumza kabla ya kukabidhi Ripoti ya Tume hiyo kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,  Samia Suluhu Hassan, Ikulu Jijini Dar es Salaam Machi 18, 2026.

Miongoni mwa mapendekezo hayo ni kufutwa kwa baadhi ya sheria zilizopitwa na wakati, ikiwamo Sheria ya Ushuru wa Bidhaa ya sasa, badala yake kutungwa sheria mpya ya ushuru wa bidhaa na huduma itakayozingatia mazingira ya uchumi wa kisasa.

Vilevile, tume imependekeza kutungwa upya kwa Sheria ya Ushuru wa Stempu ili iendane na mahitaji ya sasa ya kiuchumi na maendeleo ya teknolojia.

Katika hatua ya kupunguza mianya ya rushwa na kuongeza uwazi, tume imependekeza kuondoa utaratibu wa maofisa wa kodi kuonana uso kwa uso na walipa kodi, pamoja na kupunguza matumizi ya fedha taslimu na nyaraka za karatasi.

Pia, kwa mujibu wa tume, utekelezaji wa mapendekezo hayo unaweza kuongeza mapato ya Serikali kwa takriban Sh11.05 trilioni ndani ya miaka mitatu ya mwanzo.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,  Samia Suluhu Hassan akipokea Ripoti ya Tume ya Rais ya Kutathmini Maboresho ya Mfumo wa Kodi nchini kutoka kwa Mwenyekiti wa Tume hiyo, Katibu Mkuu Kiongozi Mstaafu Balozi Ombeni Sefue, Ikulu Jijini Dar es Salaam Machi 18, 2026.

“Ongezeko hili ni sawa na asilimia tano ya uwiano wa mapato ya kodi kwa pato la Taifa na litafikisha uwiano huo hadi asilimia 18,” amesema Sefue.

Amesema utekelezaji kamili wa mapendekezo hayo ni hatua muhimu katika kufanikisha Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2050.

Sefue amesema mageuzi hayo hayalengi tu kuongeza mapato, bali pia kuboresha mfumo mzima wa kodi kwa kukuza uwekezaji, kurasimisha shughuli za kiuchumi, kupanua wigo wa kodi na kuongeza ari ya ulipaji wa hiari.

Mapendekezo hayo 284 yanatolewa takribani miaka 35 tangu kufanyika kwa mapitio makubwa ya mfumo wa kodi nchini.

Kati ya mapendekezo hayo, 146 yanahusu sera na sheria, 41 mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), 30 masuala ya kiutawala, 25 urasimishaji na upanuzi wa wigo wa kodi, 15 mazingira ya uwekezaji na biashara, 14 utatuzi wa migogoro ya kodi na 13 muundo na mfumo wa usimamizi wa kodi.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akizungumza na viongozi mbalimbali mara baada ya kupokea Ripoti ya Tume ya Rais ya Kutathmini Maboresho ya Mfumo wa Kodi nchini, Ikulu Jijini Dar es Salaam Machi 18, 2026.

Amesema mapendekezo hayo yanakusudia kuongeza uwazi, kuondoa mabadiliko ya mara kwa mara ya kodi na kuhakikisha hakuna kodi au tozo mpya zitakazoanzishwa bila kuzingatia athari zake kwa malengo mapana ya Taifa, ikiwamo Dira ya Maendeleo 2050.

Katika mifumo ya Tehama, tume inapendekeza TRA itengeneze programu tumizi rahisi (app) itakayotumika kama lango la mlipa kodi.

Sefue amesema app hiyo inapaswa kuwa rahisi kutumiwa na kumwezesha mlipa kodi mwenye kiwango chochote cha elimu na uelewa wa masuala ya kodi kufanya shughuli mbalimbali bila kufika ofisi za TRA.

“App hii pia imuwezeshe mlipa kodi kufanya usajili, kuangalia malimbikizo ya kodi na madeni, kulipa kodi moja kwa moja kwa njia za kidijitali zinazohusisha mitandao ya simu na benki kupata stakabadhi na taarifa za miamala ya kikodi,” amesema Sefue.

Katika eneo la Tehama, tume hiyo imependekeza pia TRA iboreshe lango la mlipa kodi ili kuruhusu tathmini kufanyika kwa njia za kielektroniki kuanzia kuwasilisha ritani, nyaraka za ziada, maelezo ya ziada na majadiliano ya marekebisho ya tathmini.

Pia, TRA imetakiwa kuanzisha mfumo wa kielektroniki wa kusimamia ukaguzi wa kodi utakaoruhusu maofisa wa ukaguzi kupakia na kuchakata taarifa zote za ukaguzi ndani ya mfumo na msimamizi kufuatilia mwenendo wa ukaguzi kwa wakati.

Pendekezo lingine lililotolewa na tume hiyo ni kuunganishwa kwa kadi zote za malipo ikiwamo N-Card na kadi za mwendokasi na kuwa kadi moja itakayoweza kulipia huduma zote za msingi kwa gharama ndogo au bila malipo kabisa.

“Kadi hii iwe na toleo la kidijitali inayopatikana ndani ya programu tumizi yani e-wallet yenye taarifa zote za muhimu za mlipa kodi kwa malipo na huduma mbalimbali,”amesema Sefue.

Sambamba na hilo,tume hiyo imependekeza kuboreshwa kwa mfumo wa TAUS na kuwezesha ukusanyaji wa mapato yote ya mamlaka za Serikali za Mitaa kwa njia za kidijitali na kuweka sharti la kisheria kwa taasisi zote za Serikali ikiwamo Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kufanya na kupokea malipo kwa njia za kidigiti.

Tume hiyo pia imependekeza kubadilisha jina la TRA na kuwa Huduma za Mapato Tanzania (TRS), kama sehemu ya mageuzi yanayolenga kuimarisha ukusanyaji wa mapato na kuboresha huduma kwa walipa kodi.

“Tumeona nchi nyingi ambao wanaitwa hivyo, wala haitawapunguzia hadhi yao,” amesema Sefue.

Tume pia, imeeleza kuwa ongezeko kubwa la mifumo ya Tehama linapaswa kwenda sambamba na hatua za kuboresha utawala, kuanzisha utamaduni mpya wa huduma kwa walipa kodi na kushughulikia malalamiko kwa uwazi na uwajibikaji.

Viongozi mbalimbali na Mabalozi waliohudhuria hafla ya kupokea Ripoti ya Tume ya Rais ya Kutathmini Maboresho ya Mfumo wa Kodi nchini, Ikulu Jijini Dar es Salaam Machi 18, 2026.

Tume imependekeza TRA ibadilike kimtazamo, huku haki na wajibu wa mlipakodi zikiheshimika na utoaji wa elimu kuhusu haki na wajibu ukiongezeka.

Sefue amesema utendaji wa TRA haupaswi kupimwa kwa kiwango cha makusanyo tu, bali pia kwa usahihi wa mbinu za ukusanyaji na uimarishaji wa mahusiano bora na walipa kodi.

Mbali na hayo, tume imependekeza kuondoa utaratibu wa maofisa wa kodi kuonana uso kwa uso na walipakodi na kupunguza matumizi ya fedha taslimu na karatasi.

 “Iwapo upo umuhimu wa kuonana ana kwa ana, ufanyike katika maeneo mahsusi yenye uwazi na kamera za CCTV ili kuweka rekodi na kuondoa usiri,”amesema Sefue.

Pamoja na malengo ya kukusanya kodi, Tume inapendekeza TRA iweke malengo ya kusajili walipa kodi wapya ili kupanua wigo wa kodi na mapato kwa kuzingatia misingi ya kitaifa ya usimamizi wa mapato.

Tume pia imependekeza Serikali kuweka utaratibu mahususi kwa taasisi za udhibiti kufanya kaguzi za pamoja katika baadhi ya maeneo za biashara ambao hautasababisha usumbufu kwa wafanyabiashara lakini bila kuathiri majukumu yao ya msingi kwenye taasisi hizo.

Sambamba na hilo, imependekeza kufanyika mapitio ya ushuru, tozo na ada zinazotozwa na taasisi na mamlaka mbalimbali za Serikali ili kuondoa zile zinazofanana na kujirudia ambazo ni kero kwa wafanyabiashara na wananchi.

Katika kuongeza wigo wa walipa kodi na biashara, tume imependekeza Tamisemi kutumia kikamilifu mfumo wa Serikali ambao unafika hadi ngazi za jamii kwa ajili ya kurahisisha na kuweka utaratibu mzuri wa utambuzi wa vitu kama nyumba, biashara na shughuli nyingine za kiuchumi ili iwe rahisi kwa kila mtu kulipa kodi kwa kadri ya kipato chake.

Pendekezo hilo limeenda sambamba na kuandaliwa mfumo wa kanzidata ya usajili wa shughuli zote hizo katika maeneo ya mamlaka za Serikali za Mitaa, tume inaamini kazi hii inaweza kufanyika ndani ya mwaka mmoja.

“Tunashauri Serikali itoe muda wa mpito wa mwaka mmoja wa kutolipa kodi ya mapato kwa biashara mpya zinazoanzishwa na wajasiriamali wadogo ikiwamo startups. Waziri wa Fedha atunge kanuni kuhusu utaratibu wa kutekeleza pendekezo hilo na kuhakikisha msamaha huo hautatumika vibaya,” alisema.

Vitambulisho vya wamachinga

Tume hiyo imependekeza utaratibu wa kuandaa na kutoa vitambulisho vya wamachinga utazamwe upya na kuboreshwa huku ikiielekeza Tamisemi kuwa, mamlaka itakayotoa vitambulisho hivyo.

“Tunapendekeza Tamisemi iwe ndiyo mamlaka pekee ya kutoa vitambulisho vya wafanyabiashara wadogo kwa kuzingatia sheria.

“Vitambulisho hivyo vijumuishe taarifa muhimu za mlipakodi na kufungamanisha na leseni ya biashara, kitambulisho cha Taifa na namba ya mlipa kodi TIN. Vitambulisho hivyo viwezeshwe kufanya malipo ya kidigiti kwa kuwekewa QR code” amesema Sefue.

Katika kuongeza wigo wa elimu ya kodi, tume hiyo imependekeza ngazi zote za mitalaa kuanzia elimu ya msingi, iboreshwe kwa kuongeza somo la kodi na uzalendo ili kuweka msingi imara wa uelewa wa kila mtu kuhusu wajibu wa raia na umuhimu wa kodi kwa maendeleo ya nchi sambamba na kujenga maadili na utamaduni wa uwajibikaji kwa kila mtu.

Akizungumza baada ya kupokea ripoti hiyo, Rais Samia amesema marekebisho ni nyenzo muhimu ya kuondoa malalamiko ya muda mrefu kuhusu kodi na kuimarisha uchumi wa Taifa.

Ripoti hiyo imekabidhiwa katika kipindi ambacho Tanzania imeanza utekelezaji wa Dira ya Maendeleo 2050, mwelekeo wake ukiwa ni ukuaji wa uchumi wa kibiashara na uwekezaji.

“Nilifanya uamuzi wa kuunda tume hii ili kufanya tathmini ya kina ya mfumo wetu wa kodi kufuatia malalamiko ya muda mrefu kutoka kwa wananchi, wafanyabiashara, wawekezaji pamoja na wadau wa maendeleo kuhusu changamoto za mfumo wa kodi nchini.

“Pamoja na hayo, mabadiliko ndiyo maendeleo, mnapokaa muda mrefu lazima mjitathmini na mbadilike. Tunataka kuvua gamba la malalamiko ya kodi ili tuanze upya,” amesema Rais Samia.

Amesema mfumo bora wa kodi ni sehemu ya mkakati wa kujenga uchumi imara, jumuishi na shindani.

Pia, amesema ni nyenzo muhimu inayoiwezesha Serikali kukusanya rasilimali zinazohitajika kwa ajili ya maendeleo ya nchi na ustawi wa wananchi wake.

“Serikali na wadau tuna wajibu wa kuhakikisha tunakuwa na mfumo bora wa kodi, ukirahisisha kufuatilia makusanyo na kudhibiti mianya ya ukwepaji,” amesema.

Rais Samia ametumia fursa hiyo wakumbusha watendaji wa Serikali, wafanyabiashara na wajasiriamali kuendelea kuwa na moyo wa kushirikiana katika mchakato wa mabadiliko haya, akibainisha kwamba mabadiliko yanauma lakini ni muhimu kwa maendeleo ya Taifa.

“Kwenye mabadiliko yoyote kuna maumivu, niwaombe twende kwa mtindo ule ule wa kuvumiliana, kustahamiliana ili tujenge upya nchi yetu, tukiyatekeleza vyema haya mapendekezo yatatuelekeza kwenye kuwa na mfumo wa haki na usawa kwa walipajikodi,” amesema Rais Samia.