Rais Samia akabidhiwa mapendekezo 284 ya kodi, TRA kubadilishwa jina

Dar es Salaam. Tume ya Rais ya Kutathmini Maboresho ya Mfumo wa Kodi nchini imewasilisha mapendekezo 284 yanayolenga kufanya mageuzi makubwa ya mfumo wa kodi, ikiwa ni hatua muhimu ya kujenga mfumo ulio wazi, thabiti na unaochochea ukuaji wa uchumi.

Tume hiyo yenye wajumbe wanane inayoongozwa na mwenyekiti wake, Katibu Mkuu Kiongozi mstaafu, Balozi Ombeni Sefue iliundwa na Rais Samia Suluhu Hassan Julai 31, 2024 akiipa jukumu la kwenda kutathmini na kushauri kuhusu masuala ya kodi.

Oktoba 4, 2024, Rais Samia aliizindua na kuitaka kwenda kufanya kazi na leo Jumatano, Machi 18, 2026 Balozi Sefue na wajumbe wake wamekabidhi ripoti Ikulu jijini Dar es Salaam kwa Rais Samia ikiwa na mapendekezo 284 yaliyogawanyika kwenye maeneo mbalimbali ya utekelezaji.

Mwenyekiti wa Tume ya Rais ya Kutathmini Maboresho ya Mfumo wa Kodi nchini Katibu Mkuu Kiongozi Mstaafu, Balozi Ombeni Sefue akizungumza kabla ya kukabidhi Ripoti ya Tume hiyo kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,  Samia Suluhu Hassan, Ikulu Jijini Dar es Salaam Machi 18, 2026.

Balozi Sefue amesema mapendekezo hayo yamegawanywa katika makundi saba muhimu yanayogusa maeneo yote ya msingi ya usimamizi wa kodi nchini.

Amesema kati ya mapendekezo hayo, 146 yanahusu sera na sheria, 41 mifumo ya teknolojia ya habari na mawasiliano (tehama), 30 masuala ya kiutawala, 25 urasimishaji na upanuzi wa wigo wa kodi, 15 mazingira ya uwekezaji na biashara, 14 utatuzi wa migogoro ya kodi na 13 muundo na mfumo wa usimamizi wa kodi.

Kwenye mageuzi ya sera na sheria yapewa kipaumbele, Balozi Sefue amesema tume imependekeza kuimarishwa kwa mfumo wa kisera na kisheria ili kuweka mwongozo wa kitaifa unaoeleweka na misingi madhubuti ya uandaaji na maboresho ya kodi.

Amesema mapendekezo hayo yanakusudia kuongeza uwazi, kuondoa mabadiliko ya mara kwa mara ya kodi na kuhakikisha hakuna kodi au tozo mpya zitakazoanzishwa bila kuzingatia athari zake kwa malengo mapana ya Taifa, ikiwemo Dira ya Maendeleo 2050.

Tume pia imependekeza kutungwa kwa sera mahsusi ya Taifa ya kodi sambamba na sheria maalumu ya kodi itakayoweka misingi ya jumla ya mfumo wa kodi nchini.

Hatua hiyo inalenga kuyapa matamko ya kisera nguvu ya kisheria na kuondoa mkanganyiko uliopo sasa.

Aidha, Balozi Sefue amesema sheria hiyo inapendekezwa kujumuisha pia mamlaka za serikali za mitaa ili kuweka utaratibu bora wa mgawanyo wa vyanzo vya mapato kati ya Serikali Kuu na serikali za mitaa.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,  Samia Suluhu Hassan akipokea Ripoti ya Tume ya Rais ya Kutathmini Maboresho ya Mfumo wa Kodi nchini kutoka kwa Mwenyekiti wa Tume hiyo, Katibu Mkuu Kiongozi Mstaafu Balozi Ombeni Sefue, Ikulu Jijini Dar es Salaam Machi 18, 2026.

Tume pia imependekeza kufutwa kwa baadhi ya sheria zilizopitwa na wakati, ikiwemo sheria ya ushuru wa bidhaa iliyopo sasa na badala yake kutungwa sheria mpya ya ushuru wa bidhaa na huduma, itakayoendana na mazingira ya sasa ya uchumi.

Vilevile, imependekezwa kutungwa upya sheria ya ushuru wa stempu ili iendane na mabadiliko ya kiuchumi na kiteknolojia yanayoendelea nchini na duniani.

Mbali na hayo, tume iliyofanya kazi mikoa ya Tanzania Bara na Zanzibar imependekeza kufanyika kwa marekebisho ya sheria mbalimbali za kodi ili kuwezesha utekelezaji wa mapendekezo yote yanayohitaji maboresho ya kisheria.

Katika kuhakikisha mfumo wa kodi unakuwa jumuishi na unaokubalika, tume imesisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikishwaji wa wadau katika mchakato wa maboresho ya sheria za kodi. Hatua hivyo inalenga kuongeza uelewa, uwazi na uaminifu wa walipa kodi kwa mfumo huo.

Kwenye eneo la mifumo ya Tehama tume inapendekeza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) itengeneze programu tumizi rahisi (app) itakayotumika kama lango la mlipa kodi.

Balozi Sefue amesema app hiyo inapaswa kuwa rahisi kutumiwa na kumuwezesha mlipa kodi mwenye kiwango chochote cha elimu na uelewa wa masuala ya kodi kufanya shughuli mbalimbali bila kufika ofisi za TRA.

“App hii pia imuwezeshe mlipa kodi kufanya usajili, kuangalia malimbikizo ya kodi na madeni, kulipa kodi moja kwa moja kwa njia za kidijiti, huduma  zinazohusisha mitandao ya simu na benki kupata stakabadhi na taarifa za miamala ya kikodi,” amesema Balozi Sefue.

Kwenye eneo la Tehama tume hiyo imependekeza pia TRA iboreshe lango la mlipa kodi ili kuruhusu tathmini kufanyika kwa njia za kielektroniki kuanzia kuwasilisha ritani, nyaraka za ziada, maelezo ya ziada na majadiliano ya marekebisho ya tathmini.

Pia, TRA imetakiwa kuanzisha mfumo wa kielektroniki wa kusimamia ukaguzi wa kodi utakaoruhusu maofisa wa ukaguzi kupakia na kuchakata taarifa zote za ukaguzi ndani ya mfumo na msimamizi kufuatilia mwenendo wa ukaguzi kwa wakati.

Pendekezo lingine lililotolewa na tume hiyo ni kuunganishwa kwa kadi zote za malipo ikiwemo N-Card na kadi za mwendokasi na kuwa kadi moja itakayoweza kulipia huduma zote za msingi kwa gharama ndogo au bila malipo kabisa.

Viongozi mbalimbali na Mabalozi waliohudhuria hafla ya kupokea Ripoti ya Tume ya Rais ya Kutathmini Maboresho ya Mfumo wa Kodi nchini, Ikulu Jijini Dar es Salaam Machi 18, 2026.

“Kadi hii iwe na toleo la kidijiti inayopatikana ndani ya programu tumizi yani e-wallet yenye taarifa zote za muhimu za mlipa kodi kwa malipo na huduma mbalimbali,” amesema Balozi Sefue.

Sambamba na hilo tume hiyo imependekeza kuboreshwa kwa mfumo wa TAUS na kuwezesha ukusanyaji wa mapato yote ya mamlaka za Serikali za Mitaa kwa njia za kidijiti na kuweka sharti la kisheria kwa taasisi zote za Serikali ikiwemo Tamisemi kufanya na kupokea malipo kwa njia za kidijiti.

Miongoni mwa mapendekezo ya tume hiyo ni kubadilisha jina la Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na kuwa Huduma za Mapato Tanzania (TRS), kama sehemu ya mageuzi makubwa yanayolenga kuimarisha ukusanyaji wa mapato na kuboresha huduma kwa walipa kodi.

Balozi Sefue amesema mabadiliko haya ni muhimu ili kuanzisha utamaduni mpya wa utendaji kazi kwa wote wenye mamlaka ya kukadiria na kukusanya mapato.

“Tumeona nchi nyingi ambazo wanaitwa hivyo, wala haitawapunguzia hadhi yao,” amesema Balozi Sefue.

Tume pia imeeleza kuwa ongezeko kubwa la mifumo ya Tehama linapaswa kwenda sambamba na hatua za kuboresha utawala, kuanzisha utamaduni mpya wa huduma kwa walipa kodi na kushughulikia malalamiko kwa uwazi na uwajibikaji.

Katika hilo, tume imependekeza TRA ibadilike kimtazamo huku haki na wajibu wa mlipa kodi zikiheshimika na utoaji wa elimu kuhusu haki na wajibu ukiongezeka.

Aidha, Balozi Sefue amesema utendaji wa TRA haupaswi kupimwa kwa kiwango cha makusanyo tu, bali pia kwa usahihi wa mbinu za ukusanyaji na uimarishaji wa mahusiano bora na walipa kodi.

Mbali na hayo, tume imependekeza kuondoa utaratibu wa maofisa wa kodi kuonana uso kwa uso na walipa kodi na kupunguza matumizi ya fedha taslimu na karatasi.

“Iwapo upo umuhimu wa kuonana ana kwa ana, yafanyike katika maeneo mahsusi yenye uwazi na kamera za CCTV ili kuweka rekodi na kuondoa usiri,” amesema Balozi Sefue.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akizungumza na viongozi mbalimbali mara baada ya kupokea Ripoti ya Tume ya Rais ya Kutathmini Maboresho ya Mfumo wa Kodi nchini, Ikulu Jijini Dar es Salaam Machi 18, 2026.

Pamoja na malengo ya kukusanya kodi, tume inapendekeza TRA iweke malengo ya kusajili walipa kodi wapya ili kupanua wigo wa kodi na mapato kwa kuzingatia misingi ya kitaifa ya usimamizi wa mapato.

Katika hotuba yake baada ya kukabidhiwa, Rais Samia amesema ameyapokea mapendekezo yote 284 na wanakwenda kuyafanyia kazi kwa yale ya muda mfupi yasiyohitaji mabadiliko ya sheria.