Rais Trump alivyoanza vita na Iran bila kuagana na Hormuz

Baburnama ni kitabu cha maisha ya mwasisi wa dola ya Mughal, ahir-ud-Din Muhammad Babur, ambacho rasimu yake ilikamilika ndani ya muongo wa tatu wa Karne ya 16. Kijiografia Mughal ndiyo nchi ya Uzbekistan kwa sasa, ambayo inapatikana katikati ya Bara la Asia.

Babur ni kitukuu wa Timur, bingwa wa vita, ambaye alianzisha dola ya Timurid, na kuasisi utawala wa Koo ya Timurid. Kijiografia, dola ya Timurid ilihusisha nchi za Afghanistan, Iran, Iraq, Asia ya Kati na Kusini ya Ulaya, zilipo nchi za Armenia, Georgia, na Azerbaijan.

Katika kitabu cha Baburnama, Babur alisimulia kuwa mlango bahari wa Hormuz, ilikuwa njia muhimu ya biashara ya almond. Bonde la Ferghana (Mashariki ya Uzbekistan, Kusini ya Kyrgyzstan na Kaskazini ya Tajikistan), Asia ya Kati, ndipo zilipolimwa almond, kisha zilisafirishwa kupitia mlango bahari wa Hormuz, hadi kufika sokoni.

Karne tano baadaye, Hormuz imeendelea kuwa mlango wa kibiashara, wenye kutegemewa na sehemu kubwa ulimwenguni. Mafuta, ambayo yameendelea kuwa nishati kiranja ulimwenguni, ili kuifikia dunia kutokea Mashariki ya Kati, inategemea zaidi mlango bahari wa Hormuz.

Katika jiografia ya dunia, Hormuz ni mlango bahari unaounganisha maji baina ya Ghuba ya Uajemi (Ghuba ya Arabuni) na Ghuba ya Oman (Bahari ya Makran). Mlango bahari huo unahusisha pia mkondo muhimu unaounganisha maji ya Bahari ya Arabuni na Bahari ya Hindi, vilevile huzitenganisha nchi za Iran (upande wa Kaskazini), halafu Kusini zipo Oman na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE).

Ukiifuata ramani ya Hormuz kutokea Ghuba ya Oman, nchi ya Pakistan inaingia upande wa Kaskazini. Iran ndiyo ambayo imechukua eneo kubwa la mlango bahari wa Hormuz. Zama za Iran ya kale, Hormuz ilikuwa bandari ya kimkakati ya nchi hiyo ya Kiajemi. Hormuz ni jiji kwenye kaunti ya Bandar Abbas, Iran.

Kutokana na sababu za kihistoria, bila shaka, Iran walitambua mapema nyenzo ya kuitikisa dunia, kama sehemu ya kimkakati ya kujilinda. Hormuz, haitegemewi kwa usafirishaji wa almond, kama ilivyokuwa kipindi cha Babur, bali ni eneo ambalo linashikilia fedha dola bilioni 1.2 (Sh3.12 trilioni), kila siku.

Asilimia 25 ya mafuta ghafi kwenda soko la dunia, hupitia Homurz. Ni wastani wa mapipa milioni 20 mpaka 25 kwa siku. Meli kubwa za kusafirisha mafuta, zisizopungua 14, hupita Hormuz zikiwa na shehena za mafuta na gesi asilia (LNG), kuelekea soko la dunia.

Pamoja na uwepo wa mabomba ya kusafirisha mafuta, lakini ujazo mkubwa zaidi hutegemea safari za meli. Nchi wazalishaji wakubwa wa mafuta duniani, Saudi Arabia, Qatar, Iraq, Iran, Kuwait, UAE, hutegemea mlango wa bahari wa Hormuz katika biashara yao ya mafuta. Nchi ambazo ni vituo vikuu vya upokeaji mafuta yanayopitia Hormuz ni China, India, Japan, Korea Kusini, na Singapore.

Upana wa njia ya meli kwenye mlango wa bahari wa Hormuz ni maili mbili tu, kwa hiyo inakuwa rahisi kwa dola yoyote ya ufukweni, kama Iran, kufuatilia, kudhibiti, kuvuruga au kuzuia safari yoyote ya meli. Ni sababu hizi za kijiografia, kisayansi na kihistoria, zimefanya Hormuz kuwa jina linalosikika zaidi ulimwenguni kwa sasa.

Dhahiri, Iran waliposema walijiandaa miaka 30 iliyopita kwa vita ya sasa ya Marekani na Israel dhidi yao, maana yake walijiandaa kijeshi, nyenzo na mazingira. Walitambua mapema kuwa nguvu ya Marekani ingewasumbua, kwa hiyo walijiandaa kuhakikisha wanaifanya dunia ipige magoti. Hiyo ndiyo hali ya sasa.

Februari 28, 2026, Marekani na Israel walipoanza mashambulizi ya kushitukiza dhidi ya Iran, na kumuua aliyekuwa Kiongozi Mkuu (Rahbar), Ayatollah Ali Khamenei, hawakuwa wamejiandaa na mbinu ya Iran katika mlango bahari wa Hormuz.

Inakumbusha onyo la Karne ya 20, la aliyekuwa kamanda Nyota-5 wa Jeshi la Marekani, Omar Nelson Bradley, kuhusu aina aina ya mapambano, adui, muda na mahali vita inapiganwa. Bradley alisema kuwa Marekani kujiingiza kwenye vita ya China na Korea ilikuwa “wrong war, at the wrong place, at the wrong time, and with the wrong enemy.” – “Vita batili, katika eneo batili, muda batili, na dhidi ya adui batili.”

Rais wa Marekani, Donald Trump, amekuwa akitapatapa. Kwanza alisema meli za kusafirisha mafuta kupitia Hormuz, zingepita salama chini ya ulinzi wao. Imeshindikana. Iran wamekuwa na matokeo bora katika misheni yao ya kuhakikisha haipiti meli ya mafuta kwenye mlango bahari huo.

Tambo na vitisho vya kila aina kutoka kwa Trump, havijasaidia kitu. Awali, aliwahi kuizodoa UK kuwa Marekani haikuihitaji ili kudhinda vita dhidi ya Iran. Hata hivyo, kwa sasa Trump anaomba msaada wa nchi za Magharibi, zenye kuunda Jeshi la Nato, ikiwemo UK, zisaidie kuikabili Iran ili kuwezesha meli za mafuta kupita Hormuz.

Waziri Mkuu wa UK, Sir Keir Starmer, amekataa wazo hilo la kwenda kuikabili Iran. Ujerumani imempinga Trump kupitia kwa Waziri wa Mambo ya Nje, Johann Wadephul, Waziri wa Ulinzi, Boris Pistorius, wakati Stefan Kornelius, ambaye ni msemaji wa Kansela wa Ujerumani, Friedrich Merz, alisema: “Nato haihusiki na mgogoro wa Marekani, Israel, dhidi ya Iran.”

Waziri Mkuu wa Uholanzi, Rob Jetten, naye amepinga wazo la kuingia kwenye mgogoro huo wa Mashariki ya Kati. Waziri Mkuu wa Estonia, Margus Tsahkna, alisema washirika wa Marekani Ulaya hawajui chochote kuhusu dhamira ya vita ya Marekani, mipango, na mikakati yao. Wakati msemaji wa serekali ya Ugiriki, Pavlos ⁠Marinakis, alisema nchi yao haitahusika na makabiliano ya kijeshi Hormuz.

Sauti za kumpinga Trump na wazo la nchi za Nato kuikabili Iran Hormuz, zinasikika Italia kupitia Waziri wa Mambo ya Nje, Antonio ⁠Tajani, vilevile Denmark kwa matamshi ya Waziri wa Mambo ya Nje, Lars Lokke Rasmussen, wakatu Waziri wa Mambo ya Nje wa Poland, Radek Sikorski, amemtaka Trump kufuata utaratibu.

Dhahiri Marekani iliingia vitani na Iran bila kushauriana na kukubaliana na washirika wake. Haikumsoma Iran sawia kubaini nguvu zake, na maeneo inayojivunia. Matokeo yake, dunia ipo kwenye hatari ya kupaa gharama za maisha kwa sababu mafuta hayapiti Hormuz. Waswahili walisema, “ukitaka kuruka agana na nyonga.” Trump hakuagana na Hormuz.

Leo imetimia siku ya 20 tangu vita ianze. Hasara ya Sh3.12 trioni kwa siku, maana yake ni Sh64.2 trilioni kwa siku 20. Halafu dalili ya vita kufika mwisho haionekani.