Dar es Salaam. Wataalamu wa afya nchini wamesema saratani ya utumbo mpana, kitaalamu ikiitwa Colorectal Cancer, imeanza kuongezeka kwa kasi nchini, huku mabadiliko ya mtindo wa maisha yakitajwa kuwa sababu kubwa inayochangia ongezeko hilo.
Miji mikubwa imetajwa kuwa hatarini, huku wataalamu wakisema ongezeko hilo linachangiwa zaidi na mabadiliko ya mtindo wa maisha, ikiwamo ulaji wa vyakula vilivyosindikwa, pombe, tumbaku na ukosefu wa lishe yenye mboga na matunda.
Takwimu zinaonesha ugonjwa huo ambao miaka takribani 10 iliyopita ulikuwa ukishika nafasi ya 11 miongoni mwa saratani zinazoonekana kwa wanaume nchini, sasa umeingia katika saratani tano zinazoongoza na kushika nafasi ya tatu kwa wanaume.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Huduma za Kinga na Daktari Bingwa wa Saratani katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road, Crispin Kahesa, alipozungumza na Mwananchi Jumapili, Machi 15, 2026.
Kahesa amesema Tanzania inakadiriwa kuwa na wagonjwa wapya takribani 1,800 wa saratani ya utumbo mpana kila mwaka.
Amesema kati ya hao, wagonjwa wapya wapatao 220 hupokewa kila mwaka Ocean Road kwa ajili ya uchunguzi na matibabu.
“Kwa kipindi cha miaka 10 iliyopita tulikuwa tunaiona saratani hii katika nafasi ya 11, lakini sasa imeingia katika saratani tano zinazoongoza. Kwa wanaume sasa iko nafasi ya tatu,” amesema.
Dk Kahesa amesema takribani asilimia 95 ya wagonjwa wa saratani ya utumbo mpana wanahusishwa na tabia hatarishi za maisha.
Ametaja baadhi ya tabia hizo kuwa ni matumizi ya pombe, tumbaku na shisha pamoja na ulaji usiozingatia lishe bora hasa ulaji mdogo wa mbogamboga, matunda na vyakula vyenye nyuzinyuzi (fiber).
“Lishe isiyo na uwiano na ukosefu wa vyakula vya asili kama mboga za majani na matunda ni sababu kubwa. Pia, kuna maambukizi ya baadhi ya bakteria na vidonda vya tumbo vya muda mrefu ambavyo vinaweza kusababisha mabadiliko kwenye utumbo na hatimaye kuleta saratani,” amesema.
Amesema wanaume wanaonekana kuathirika zaidi na ugonjwa huo ikilinganishwa na wanawake, huku umri wa wastani wa wagonjwa nao ukionekana kushuka.
Dk Kahesa amesema awali wagonjwa wengi walikuwa na wastani wa miaka 50, lakini kwa sasa wastani umeshuka hadi miaka 45.
“Hii inaonesha kuna kundi kubwa la watu wenye umri mdogo wanaoanza kupata saratani hii, hata vijana wenye umri wa miaka 30 wanaonekana kuathirika,” amesema.
Kuhusu dalili, amesema katika hatua za mwanzo ugonjwa huo huwa hauna dalili za wazi, hali inayosababisha watu wengi kuchelewa kugundua tatizo hilo.
Ametaja baadhi ya dalili zinazoweza kuonekana kuwa ni maumivu ya tumbo, kujaa gesi mara kwa mara pamoja na mabadiliko ya tabia ya kupata choo.
Amesema katika hatua za juu zaidi, mgonjwa anaweza kupoteza hamu ya kula, kupungua uzito au kutoa choo chenye damu.
“Endapo saratani itasambaa kwenda kwenye viungo vingine kama ini, mgonjwa anaweza kuanza kupata dalili nyingine kulingana na kiungo kilichoathirika,” amesema.
Ameongeza kuwa wakati uvimbe unapokuwa mkubwa kwenye utumbo unaweza kusababisha chakula kushindwa kupita vizuri, hali inayomfanya mgonjwa ashindwe kula na kupoteza uzito kwa haraka.
Kuhusu matibabu, Dk Kahesa amesema hatua ya kwanza ni kufanya vipimo ili kuthibitisha kama mgonjwa ana saratani ya utumbo mpana.
Amesema vipimo hivyo ni pamoja na ultrasound, CT scan, MRI na PET-CT scan pamoja na kipimo cha kuchukua chembehai (biopsy) kwa ajili ya uchunguzi wa maabara.
“Baada ya hapo matibabu hutegemea hatua ya ugonjwa. Inaweza kuwa upasuaji wa kuondoa uvimbe au sehemu ya utumbo iliyoathirika, tiba ya kemikali (chemotherapy) au tiba ya mionzi,” amesema.
Amesisitiza kuwa pamoja na matibabu, kinga ndiyo silaha muhimu zaidi katika kupunguza ongezeko la ugonjwa huo.
Amesema taasisi hiyo imeanza kuimarisha programu za uchunguzi wa mapema ikiwemo kipimo cha kuchunguza damu ndogo kwenye kinyesi pamoja na uchunguzi kwa kutumia darubini maalumu ya utumbo.
“Tunataka watu wapate uchunguzi mapema kwa sababu saratani hii ikigundulika mapema ina uwezekano mkubwa wa kutibika,” amesema.
Kwa upande wake mtaalamu wa afya ya jamii, Ali Mzige, amesema ongezeko la saratani ya utumbo mpana linahusishwa kwa kiasi kikubwa na mabadiliko ya tabia za ulaji.
Amesema ulaji mdogo wa vyakula vyenye nyuzinyuzi kama mboga za majani, matunda, kunde na nafaka zisizokobolewa unachangia kuongezeka kwa tatizo hilo.
“Vyakula vyenye nyuzinyuzi vinasaidia kusafisha mfumo wa mmeng’enyo wa chakula na kurahisisha utoaji wa kinyesi. Bila hivyo taka hubaki kwenye utumbo kwa muda mrefu na kuongeza hatari ya magonjwa,” amesema.
Ameonya pia dhidi ya matumizi makubwa ya vyakula vilivyosindikwa kama soseji, pizza, burger na vyakula vingine vya haraka vinavyotengenezwa kwa kemikali ili kudumu kwa muda mrefu.
Amesema vyakula hivyo mara nyingi huwa na mafuta mengi, chumvi nyingi na hukosa virutubisho muhimu vinavyopatikana katika vyakula vya asili.
“Matunda na mboga za majani zina kemikali asilia zinazosaidia kuondoa sumu mwilini na kupunguza athari za chembe hatarishi zinazoitwa free radicals ambazo zinaweza kusababisha saratani,” amesema.
Dk Mzige amesema pamoja na lishe bora, watu wanapaswa kufanya mazoezi mara kwa mara, kunywa maji ya kutosha na kupunguza matumizi ya pombe na vyakula vyenye sukari nyingi.
Amesema bila kufanya mabadiliko hayo ya mtindo wa maisha, hatari ya saratani ya utumbo mpana itaendelea kuongezeka huku ikianza kuathiri watu katika umri mdogo zaidi.
