Dar es Salaam. Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa Tanzania (TALGWU), kinatarajiwa kufanya uchaguzi wa kupata viongozi wapya kuanzia ngazi ya matawi hadi Taifa Aprili na kukamilika Septemba 2026.
Kwa mujibu wa tangazo lililotolewa leo Jumatano Machi 18,2026 na Kaimu Katibu Mkuu wa TALGWU, Wandiba Ngocho, katika uchaguzi huo kutakuwa na uchaguzi mkuu wa ngazi ya matawi, wilaya, mikoa na Taifa na viongozi watakaochaguliwa watakiongoza chama hicho kwa kipindi cha miaka mitano.
Ngocho amesema uchukuaji na urejeshaji wa fomu unaanza Machi 23 hadi Machi 27, 2026 katika ofisi za matawi na mikoa huku muda wa kuzichukua ukiwa ni kuanzia saa 2:00 asubuhi hadi saa 9:30 alasiri.
Amesema fomu hizo za kugombea zitatolewa bure ambapo kwa ngazi ya tawi kila mwanachama atapaswa kurejesha fomu hizo kwa katibu wa tawi lake analofanyia kazi.
Kwa mujibu wa tangazo hilo, ratiba ya uchaguzi huo kwa ngazi ya matawi unatarajiwa kufanyika kuanzia Aprili 22 hadi Juni 1, 2026 wakati ngazi ya wilaya uchaguzi huo utafanyika kuanzia Juni 22 hadi Julai 4, 2026 huku ngazi ya mkoa uchaguzi huo utafanyika kuanzia Julai 13 hadi Septemba 4, 2026.
Amesema uchaguzi mkuu unatarajia kufanyika Septemba 18, 2026 ukifuatiwa na uchaguzi wa baraza kuu utakaofanyika Septemba 19, 2026.
Nafasi zinazogombewa katika ngazi ya matawi kwa mujibu wa tangazo hilo ni pamoja na wajumbe akiwemo mwenyekiti na katibu ambapo idadi hiyo ya wajumbe itategemea na idadi ya wanachama waliopo.
Katika hili, kwa tawi lenye wanachama wasiozidi 10 au 50, wajumbe watakaotakiwa ni watano, huku lenye wanachama 50 lakini sio chini ya 100 wanatakiwa wajumbe kumi na wajumbe 15 kwa tawi linalozidi wanachama 100 lakini sio chini ya 500.
Aidha wajumbe 20 kwa tawi lenye wanachama wanaozidi 500 lakini sio chini ya 100.
Nafasi zingine ni Mwenyekiti na kamati ya ushauri ya wafanyakazi wanawake wa tawi, wajumbe wawili wa kamati ya ushauri wafanyakazi wanawake, mwakilishi wa wafanyakazi vijana wa tawi na mwakilishi wa wafanyakazi wenye ulemavu katika tawi.
Kwenye ngazi ya wilaya nafasi zinazogombewa ni mwenyekiti wa wilaya, mjumbe anayeingia kamati ya utendaji wilaya, mjumbe anayewakilisha wilaya kwenye kamati ya utendaji mkoa.
Pia, ipo nafasi ya mwenyekiti na katibu wa kamati ya ushauri ya wafanyakazi wanawake wilaya, wajumbe watatu wa kamati ya ushauri ya wafanyakazi wanawake ,mjumbe mmoja anayewakilisha wilaya kwenye kamati ya ushauri wafanyakazi wanawake mkoa.
Nafasi nyingine ni mwakilishi wa wafanyakazi vijana anayewakilisha vijana kwenye kamati ya utendaji wilaya, mwakilishi wafanyakazi walemavu, wawaikilishi watatu watakaoingia kamati ya utendaji wilaya na wajumbe watatu watakaoigia kwenye mkutano wa mkuu wa mkoa.
Kwenye ngazi ya mkoa nafasi zinazogombewa ni mwenyekiti wa mkoa, mjumbe mmoja wa baraza kuu la taifa atakayewakilisha mkoa, mjumbe mmoja wa kamati ya utendaji taifa atakayewakilisha mkoa.
Pia wapo wajumbe watatu watakaowakilisha mkoa katika mkutano mkuu wa taifa, mwenyekiti wa kamati ya ushauri ya wafanyakazi wanawake mkoa.
Wengine ni katibu wa kamati ya ushauri wafanyakazi wanawake mkoa, mwakilishi wa shirika la maendeleo la uchumi lililopo katika mkoa.
Pia mjumbe mmoja mwakilishi wa watu wenye ulemavu kuwa mjumbe wa kamati ya utendaji mkoa kutoka miongoni mwa wawakilishi wa wafanyakazi wenye ulemavu wa wilaya.
Mjumbe mmoja mwakilishi wa vijana kuwa mjumbe wa kamati ya utendaji mkoa kutoka miongoni mwa wawakilishi wa vijana wa wilaya.
Wajumbe watatu (3) wanaoingia kwenye kamati ya utendaji mkoa kutoka miongoni mwa wanachama wanaofanya kazi serikali kuu, wakala na taasisi za serikali.
Wajumbe watatu wa mkutano mkuu wa mkoa kutoka miongoni mwa wanachama wanaofanya kazi serikali kuu, wakala na taasisi za serikali.
Mjumbe mmoja anayewakilisha chama katika mkutano mkuu wa shirikisho la vyama vya wafanyakazi tanzania (tucta). Kwa upande wa ngazi ya taifa, nafasi zinazogombewa mwenyekiti wa chama wa taifa, makamu mwenyekiti wa chama, katibu mkuu, naibu katibu mkuu wa chama, mweka hazina wa chama, mwenyekiti na katibu wa kamati ya ushauri ya wafanyakazi wanawake taifa.
Nafasi zingine ni wajumbe kumi wa kamati ya ushauri wafanyakazi wanawake taifa.