Aliongeza kuwa nafasi ya Tanzania katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) inaipa nchi faida ya kipekee ya kuhudumia soko kubwa la kikanda, jambo linalovutia zaidi wawekezaji.
Katika hatua ya kuimarisha sekta hiyo, serikali inaendelea kuendeleza Eneo Maalum la Kiuchumi la Dawa la Mloganzila pamoja na vituo vya uzalishaji wa dawa katika maeneo ya Mloganzila na Kibaha. Pia imeanzisha Kikosi Kazi cha Kuharakisha Uwekezaji wa Dawa (PIAT) kwa lengo la kurahisisha taratibu na kuharakisha uwekezaji wa kimkakati.
Mchengerwa alisisitiza kuwa Tanzania haitaki kuwa soko la teknolojia zilizopitwa na wakati au bidhaa duni, bali inalenga uzalishaji wa dawa za kisasa zinazokidhi viwango vya kimataifa. “Dawa duni hugharimu maisha. Hatuwezi kuendelea kuwa soko la dawa za jana wakati dunia imeendelea,” alionya.
Alihimiza wawekezaji kuangalia fursa zilizopo katika uzalishaji wa dawa, vifaa tiba, uchunguzi wa magonjwa, mifumo ya usambazaji, pamoja na utafiti na maendeleo ya rasilimali watu.
Kwa upande wake, alisema Uingereza ina nafasi muhimu katika kushirikiana na Tanzania kutokana na uzoefu wake katika teknolojia ya afya, utafiti na uwekezaji, akikaribisha ubia wa kimkakati utakaosaidia kukuza sekta hiyo.
Akihitimisha, Waziri Mchengerwa alitoa wito kwa wawekezaji wa kimataifa kuchangamkia fursa zilizopo nchini Tanzania, akisisitiza kuwa serikali iko tayari kuwezesha mazingira bora ya uwekezaji.
“Fursa ipo, soko linakua, na dhamira ni thabiti. Tunakaribisha wawekezaji kushirikiana nasi kujenga mustakabali wa afya barani Afrika,” alisema.
Katika Jukwaa hilo pia Meneja wa Biashara na Maendeleo, Philip Conradi wa Kampuni kubwa Duniani ya uzalishaji wa Bidhaa za Afya- Sartorius alihudhuria.

