MSAKO wa pointi tatu kwa Yanga unaendelea leo huku ikiwa na wimbi kubwa la mastaa majeruhi ambapo wameongezeka wengine wanne na kufikia sita, baada Clement Mzize na Dickon Job kuwa nje.
Yanga inayoongoza msimamo wa Ligi Kuu Bara ikiwa na pointi 36, leo ni mgeni wa TRA United, mechi ikichezwa Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha kuanzia saa 10:00 jioni.
Mbali na Mzize na Job, Yanga itawakosa Ibrahim Abdullah ‘Bacca’ mwenye jeraha la nyonga na atakuwa nje ya uwanja kwa wiki tatu, Laurindo Dilson ‘Depu’ anayesumbuliwa na nyama za paja akitarajiwa kukaa nje wiki mbili, huku Chadrack Boka ana jeraha la enka ya mguu wa kushoto na atakuwa nje kwa wiki mbili. Pia Edmund John ana jeraha la bega na atakuwa nje kwa wiki mbili.
Mechi hiyo ambayo inazikutanisha timu zinazomaliza mzunguko wa kwanza, inarudisha kumbukumbu ya msimu uliopita ambapo zilipokutana duru la kwanza Novemba 7, 2024, TRA United ilishinda 3-1 ugenini. Safari hii ipo nyumbani na Yanga ndiyo wageni. Kwa namna moja ama nyingine imekaa kimkakati zaidi kwani kila moja inahitaji kufunga hesabu vizuri.
Rekodi zinaonyesha TRA United tangu inaitwa Tabora United imekutana na Yanga mara tano, nne ikiwa Ligi Kuu Bara na moja Kombe la FA. Katika mechi nne za Ligi Kuu Bara, TRA United imeshinda moja, huku Yanga ikishinda tatu sambamba na ile ya Kombe la FA.
Zinapokutana TRA United na Yanga nyavu zinatikiswa kwani mechi zote tano zilizochezwa kuna angalau bao moja limefungwa huku jumla yakipatikana mabao 14, Yanga ikifunga 11, TRA United inayo matatu, yote ikiyafunga katika ushindi wa 3-1. Yanga pia ina rekodi ya kutoka uwanjani mechi nne bila ya kuruhusu bao dhidi ya TRA United.
Kocha wa TRA United, Ettiene Ndayiragije, amezungumzia mechi hiyo akisema: “Tunashukuru Mungu baada ya kutocheza mechi dhidi ya Simba tumerudi uwanja wa mazoezi kubadilisha mipango ambayo tutaitumia kucheza na Yanga, vijana wote wapo, hakuna shida, tuna imani kwa baraka za Mwenyezi Mungu tutapambana kupata pointi tatu.”
Kwa upande wa Kocha wa Yanga, Pedro Goncalves, alisema: “Kesho (leo) itakuwa mechi yetu ya mwisho katika mzunguko wa kwanza wa ligi dhidi ya timu nzuri, wamejijenga vizuri kwa ajili ya baadaye, natarajia mzunguko wa pili TRA itaonyesha nguvu kubwa. Nafahamu ina mipango ya kukua zaidi, ninaheshimu hilo. Kiukweli kesho (leo) tutakuwa na mechi ngumu sana.
“Tuna siku mbili kutoka mechi ya mwisho ambayo ilikuwa kali sana dhidi ya Azam na sasa ni dhidi ya TRA.
“Wapinzani wetu walikuwa na takribani wiki moja ya kujiandaa kwa ajili ya mechi hii. Ni mechi itakayotupa ushindani mkubwa kwa sababu tunakwenda kukutana na timu ambayo haijajiandaa kwa ajili ya kumiliki mchezo tu bali kushambulia.
“Hata hivyo, tunajiamini, bado tupo kileleni mwa msimamo wa ligi, tunacheza vizuri, kwa hiyo kesho (leo) tunakutana na changamoto kutoka kwa mpinzani wetu lakini pia changamoto za ndani ya timu kutokana na majeruhi tulionao.”
TRA United inasaka ushindi katika mechi hii ili kufikisha pointi 22 na kupanda hadi nafasi ya sita kutoka ya kumi ilipo sasa, huku Yanga inahitaji kumaliza duru la kwanza kukaa kileleni kwa pointi 39 baada ya sasa kuwa nazo 36.
Saa 2:00 usiku, itashuhudiwa mechi nyingine ya Ligi Kuu Bara ambapo Shadrack Nsajigwa atawaongoza vijana wake wa Tanzania Prisons kulinda heshima ya uwanja wa nyumbani itakapoikaribisha Singida Black Stars.
Ni mechi ambayo kwa Nsajigwa mtihani mwingine baada ya kutoka kupoteza mechi tatu mfululizo dhidi ya TMA Stars katika Kombe la Shirikisho la CRDB, pia dhidi ya Yanga katika Ligi Kuu Bara na zote ikipokea kichapo kinachofanana cha bao 1-0.
Hii itachezwa kwenye Uwanja wa Jamhuri pale Dodoma ambapo Tanzania Prisons inautumia kwa mechi za nyumbani baada ya ule wa Sokoine jijini Mbeya kufungwa kutokana na kutokidhi vigezo vya kikanuni.
Singida Black Stars inaingia uwanjani ikiwa imetoka kushusha mvua ya mabao kwa ndugu zao Tanzania Prisons, Mbeya City ilipoichapa 4-1 ugenini pia, mechi iliyochezwa Tanzanite Kwaraa, Manyara.
Msimu uliopita, Singida Black Stars ikiwa ugenini iliichapa Tanzania Prisons mabao 2-0, lakini iliporudi nyumbani matokeo yakawa 3-3.
Tangu inaitwa Ihefu kabla ya kubadilishwa na kuwa Singida Black Stars, timu hizi zimekutana mara nane kwenye ligi, Singida Black Stars ikishinda nne, Tanzania Prisons imeshinda moja, huku tatu zikiwa sare.
Tanzania Prisons, hii ni mechi ya nne mfululizo inakwenda kucheza dhidi ya timu zilizomaliza nafasi nne za juu katika Ligi Kuu Bara msimu uliopita baada ya Februari 22, 2026 kupigwa 2-0 na Simba, ikatoka 0-0 dhidi ya Azam (Machi 5, 2026), kisha ikapokea kichapo cha 1-0 dhidi ya Yanga (Machi 12, 2026).
Nsajigwa alisema: “Sisi kiujumla tumejiandaa vizuri na mchezo dhidi ya Singida, tunajua Singida wametoka kupata ushindi mnono dhidi ya Mbeya City. Sisi tunabaki kusema vilevile, tunaendelea kucheza dhidi ya timu zenye kariba zinazokaribiana.
Meneja Mkuu wa Singida Black Stars, Othmen Najjar, alisema: “Tumetoka kucheza mchezo mgumu dhidi ya Mbeya City na tumepata muda mchache wa kupumzika ila haiondoi utayari wetu kuelekea mchezo wa kesho (leo) dhidi ya Tanzania Prisons hapa Dodoma.”