Tume yabaini changamoto lukuki mfumo wa kodi,  yasisitiza mageuzi

Dar es Salaam. Baada ya takribani miaka 30 tangu kufanyika kwa mapitio makubwa ya mfumo wa kodi nchini, Tume ya Rais ya Kutathmini Maboresho ya Mfumo wa Kodi imebaini changamoto lukuki zinazoathiri walipa kodi na mazingira ya uwekezaji, huku ikisisitiza umuhimu wa mageuzi ya haraka ili kufikia malengo ya maendeleo ya muda mrefu.

Julai 31, 2024, Rais Samia alitangaza kuunda tume hiyo na kumteua Katibu Mkuu Kiongozi mstaafu, Balozi Ombeni Sefue kuiongoza ikiwa na wajumbe wanane akiwemo aliyewahi kuwa Gavana wa Benki Kuu, (BoT), Profesa Florens Luoga.

Oktoba 4, 2024, Rais Samia aliizindua tume hiyo na kuanza kazi na leo Jumatano, Machi 18, 2026 Balozi Sefue amewaongoza wajumbe wenzake kukabidhi ripoti hiyo kwa Rais Samia, Ikulu jijini Dar es Salaam.

Rais Samia aliunda tume hiyo ikafanye kazi ya kutathmini na kushauri kuhusu masuala ya kodi.

Akiwasilisha tathmini ya tume hiyo, Balozi Sefue amesema mfumo wa sasa haujapitiwa kwa kina tangu enzi za tume iliyoongozwa na marehemu Edwin Mtei, wakati ambao mazingira ya kiuchumi yalikuwa tofauti kabisa na ya sasa.

Licha ya mafanikio ya ukuaji wa uchumi unaozidi asilimia sita na ongezeko la mapato ya Serikali, tume imeonya bado kuna upungufu unaoweza kudhoofisha kasi hiyo, hasa kama hayatashughulikiwa kwa wakati.

Moja ya mambo makubwa yaliyobainishwa ni uwepo wa viwango vikubwa vya baadhi ya kodi pamoja na kuanzishwa kwa tozo, ada na ushuru mpya bila kuzingatia kikamilifu malengo mapana ya kitaifa.

Balozi Sefue amesema hali hiyo husababisha kutotabirika hivyo kuathiri mazingira ya uwekezaji na biashara.

Aidha, mfumo wa utatuzi wa migogoro ya kikodi umeonekana kutoridhisha walipa kodi, huku wengi wakikosa imani kutokana na mtazamo kuwa vyombo vinavyosimamia migogoro hiyo havina uhuru wa kutosha.

Balozi Sefue amesema Tume pia imebaini kuwepo kwa mamlaka nyingi zinazokusanya mapato sambamba na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na serikali za mitaa bila uratibu wa pamoja.

“Hali hii husababisha walipa kodi kutozwa ada na ushuru mara kwa mara katika chanzo kimoja, jambo linaloongeza gharama na usumbufu na hata kuchochea vitendo vya rushwa,” amesema Balozi Sefue.

Katika tathmini hiyo pia imeelezwa hakuna mfumo jumuishi wa kuwatambua, kuwalea na kuwakuza wajasiriamali wadogo, jambo linaloendelea kuwa kilio kikubwa kwa wananchi, hasa vijana.

Tume hiyo imeonya bila mkakati madhubuti katika eneo hilo, ndoto ya uchumi shirikishi itabaki kuwa nadharia.

Dosari nyingine iliyoonekana na wigo mdogo wa walipa kodi ambapo licha ya takwimu kuonesha uwiano wa mapato ya kodi kwa pato la Taifa kumeongezeka hadi asilimia 13.5 mwaka 2025 kutoka asilimia 11.5 mwaka 2023, bado uko chini ya wastani wa asilimia 16 kwa nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na chini ya lengo la zaidi ya asilimia 20 linalohitajika kufikia dira ya maendeleo 2050.

Tume imeeleza wigo mdogo wa walipa kodi unasababisha mzigo mkubwa kubebwa na kundi dogo lililo kwenye mfumo rasmi, huku wengi walioko kwenye sekta isiyo rasmi wakibaki nje ya mfumo huo.

Changamoto nyingine iliyobainishwa ni mchakato mgumu na gharama kubwa za kurasimisha biashara, hali inayowakatisha tamaa wengi.

“Baadhi ya wananchi wamelalamika kudaiwa kodi hata kabla ya kuanza kupata mapato, jambo linalowafanya wengine kujuta kurasimisha biashara zao. Hakuna popote tulikopita ambapo wananchi hawataki kulipa kodi wala kurasimisha biashara za wanachotaka ni mfumo rahisi, wa haki na unaoeleweka,” amesema Balozi Sefue.

Ingawa kumekuwa na maboresho ya mifumo ya Tehama katika ukusanyaji wa kodi, tume imeeleza bado mifumo hiyo haisomani kikamilifu na si rafiki kwa watumiaji, hasa wafanyabiashara wadogo.

Pia, imebainika matumizi ya risiti za kielektroniki (EFD) bado ni madogo, huku elimu ya kodi na fedha kwa wananchi ikiwa chini, hali inayochangia kutokuelewa wajibu wao ipasavyo.

Hafla hiyo imehudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo, Makamu wa Rais, Dk Emmanuel Nchimbi, Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi, Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba, Jaji Mkuu wa Tanzania, George Masaju na Spika wa Bunge, Mussa Zungu.

Pia, wamehudhuria mawaziri, makatibu wakuu, mabalozi na wawakilishi wa mataifa mashirika mbalimbali ya kimataifa nchini.