Uchaguzi Mkuu wa Congo Brazzaville unavyoibua mjadala wa demokrasia

 Dar es Salaam. Kura zinaendelea kuhesabiwa huko Congo Brazzaville kufuatia uchaguzi wa rais uliofanyika jana, huku ukishuhudia mwitikio mdogo wa wapiga kura.

Vituo vya kupigia kura vilifungwa saa kumi na mbili jioni, na mamlaka nchini humo zimetangaza kuwa matokeo ya awali yanatarajiwa kuanza kutolewa ndani ya saa 48 hadi 72 zijazo, huku matokeo rasmi yakitarajiwa kupatikana ndani ya kipindi cha wiki mbili.

Hata hivyo, pamoja na mchakato huo kuendelea, hali ya sintofahamu imeendelea kutawala miongoni mwa wananchi na wachambuzi wa siasa, wengi wakieleza kutokuwa na imani na uchaguzi huo kama utaleta mabadiliko ya kisiasa.

Wasiwasi huo unatokana na historia ya muda mrefu ya utawala wa Rais wa sasa, Denis Sassou Nguesso, ambaye ameiongoza nchi hiyo kwa zaidi ya miongo minne.

Ushiriki mdogo na mazingira tata

Uchaguzi huo umefanyika katika mazingira yaliyogubikwa na changamoto kadhaa, zikiwemo wito wa kususia uliotolewa na vyama vikubwa vya upinzani.

Gari la kampeni likiwa limebandiikwa picha ya Rais wa Congo Brazzaville, Denis Sassou Nguesso. Picha na Mtandao

Vyama viwili vikuu havikushiriki katika uchaguzi huo, huku vikihamasisha wananchi kutojitokeza kupiga kura, jambo lililochangia kupungua kwa mwitikio wa wapiga kura.

Licha ya kuwepo kwa wagombea sita kutoka vyama vidogo, wachambuzi wa siasa wanaeleza kuwa hakuna aliyekuwa na nguvu ya kumpa ushindani wa maana Rais wa sasa mwenye umri wa miaka 82.

Hali hiyo imeibua hoja kuhusu ubora wa ushindani wa kisiasa na uhalisia wa demokrasia nchini humo huku kwa upande mwingine, hali ya usalama na hatua zilizochukuliwa na mamlaka wakati wa uchaguzi zimezua mjadala. Mawasiliano ya mtandao yalizimwa katika maeneo mbalimbali ya nchi, huku usafiri wa magari ukidhibitiwa katika mji mkuu wa Brazzaville. Hatua hizo, kwa mujibu wa wachambuzi, zilichangia kuongeza hofu na kupunguza ushiriki wa wananchi katika zoezi la kupiga kura.

Wachambuzi wanaeleza kuwa mabadiliko hayo ya Katiba ni miongoni mwa mambo yanayochangia kupungua kwa imani ya wananchi katika mchakato wa kidemokrasia, kwani yanaonekana kupunguza ushindani wa kisiasa na kufifisha matumaini ya mabadiliko ya uongozi.

Changamoto za uchumi na maisha ya wananchi

Pamoja na mjadala wa kisiasa, hali ya uchumi wa Jamhuri ya Congo Brazzaville imeendelea kuwa kitovu cha wasiwasi kwa wananchi wengi.

Licha ya kuwa na utajiri mkubwa wa rasilimali za asili, hususan mafuta na madini, taifa hilo linakabiliwa na changamoto kubwa za kiuchumi.

Kwa mujibu wa Benki ya Dunia, deni la taifa hilo limefikia takribani asilimia 94 ya pato la taifa, hali inayozorotesha uwezo wa serikali kutoa huduma muhimu kwa wananchi.

Aidha, kiwango cha umasikini kinaendelea kuwa cha juu, huku vijana wengi wakikosa ajira na fursa za kujikwamua kiuchumi.

Mchambuzi wa masuala ya kijamii na uchumi, Marie Therese Ndziessi, anasema zaidi ya nusu ya wananchi wanaishi katika mazingira magumu ya kiuchumi, hali inayoongeza shinikizo kwa serikali inayotarajiwa kuundwa baada ya uchaguzi. Anabainisha kuwa, ingawa uchaguzi unaweza kuendeleza utulivu wa kisiasa, matarajio ya wananchi yako zaidi katika mageuzi ya kiuchumi yatakayoboresha maisha yao ya kila siku, ikiwemo upatikanaji wa ajira, huduma za kijamii na usimamizi bora wa rasilimali za taifa.

Taswira ya demokrasia barani Afrika

Hata hivyo, hali ya kisiasa inayoonekana Congo Brazzaville imeibua mjadala mpana kuhusu mustakabali wa demokrasia barani Afrika. Wachambuzi wengi wanaona kuwa changamoto zinazojitokeza nchini humo zinafanana na zile zinazoshuhudiwa katika baadhi ya mataifa mengine ya Afrika.

Kwa mujibu wa Wakili, Onesmo Kyauke, hali ya Congo Brazzaville inaakisi changamoto ya viongozi kudumu madarakani kwa muda mrefu, jambo linaloonekana pia katika mataifa kama Uganda na Ivory Coast.

Anasema hali hiyo inadhoofisha misingi ya demokrasia kwa kupunguza ushindani wa kisiasa na kuzuia kuibuka kwa fikra mpya katika uongozi. Pia, inachangia kudhibiti uhuru wa wananchi na kusababisha rasilimali za umma kunufaisha kundi dogo la watu.

“Demokrasia yenye ushindani wa kweli ni muhimu kwa maendeleo, kwani hutoa nafasi ya mabadiliko ya uongozi na kuwawajibisha viongozi kwa wananchi,” anasisitiza.

Mjadala wa mifumo ya utawala

Kwa upande wake, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Paul Loisulie anaona kuwa hali hiyo inapaswa kuchambuliwa kwa kina zaidi katika muktadha wa mifumo ya utawala inayotumika barani Afrika.

Anabainisha kuwa mataifa mengi ya Afrika yaliingia katika mfumo wa demokrasia kwa shinikizo la nje, hasa kutoka kwa mataifa ya Magharibi na masharti ya misaada ya kifedha. Hali hiyo imefanya baadhi ya chaguzi kufanyika kama taratibu za kukidhi mahitaji ya nje badala ya kuakisi matakwa halisi ya wananchi.

Aidha, anasema kuendelea kwa mfumo wa chama dola katika baadhi ya nchi kunakinzana na misingi ya demokrasia, na kuchangia viongozi kubaki madarakani kwa muda mrefu bila ushindani wa kweli.

“Ili kupata suluhisho la kudumu, ni muhimu kwa mataifa ya Afrika kujitafakari na kuamua kwa hiari mfumo wa utawala unaofaa kwa mazingira yao ya kijamii, kisiasa na kiuchumi,” anasema.

Anasisitiza kuwa mjadala wa wadau mbalimbali unahitajika ili kubaini mwelekeo sahihi wa siasa za Afrika, hasa katika kipindi hiki ambacho matarajio ya wananchi kuhusu uwajibikaji na maendeleo yanaendelea kuongezeka.

Wakati matokeo ya uchaguzi huo yakisubiriwa, mjadala haujikita tu kwa nani ataibuka mshindi, bali pia katika mustakabali wa demokrasia na maendeleo ya taifa hilo.

Iwapo changamoto za kisiasa na kiuchumi hazitashughulikiwa kwa kina, wachambuzi wanaonya kuwa hata mabadiliko ya uongozi hayatakuwa na maana kubwa kwa wananchi wanaotarajia kuona maisha yao yakiboreka. Hivyo, macho na masikio ya wengi yameelekezwa si tu katika matokeo ya kura, bali pia katika hatua zitakazofuata baada ya uchaguzi huo.