UCHAMBUZI WA MAYALA: Mwaka mmoja wa Jab na hatua zake muhimu

Machi, 2026 unaashiria hatua muhimu katika historia ya sekta ya habari nchini baada ya Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (Jab) kutimiza mwaka mmoja tangu kuzinduliwa kwake rasmi tarehe 3 Machi 2025.

Kuanzishwa kwa bodi hiyo kulitekeleza matakwa ya Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016, ambayo inalenga kusimamia ithibati ya waandishi wa habari na kuhakikisha taaluma hiyo inaendeshwa kwa kuzingatia maadili na viwango vya kitaaluma.

Baada ya mwaka mmoja wa utendaji, tathmini ya haraka inaonyesha kuwa Jab imefanikiwa kufikia hatua kadhaa muhimu, hususan katika kuanzisha mfumo wa kisasa wa usajili wa waandishi wa habari na kuongeza idadi ya wanataaluma waliopata ithibati.

Hata hivyo, pamoja na mafanikio hayo, bado kuna masuala yanayohitaji kufanyiwa kazi ili kuimarisha zaidi ufanisi wa bodi hiyo.

Moja ya mafanikio makubwa yaliyopatikana katika kipindi hicho ni kuanzishwa kwa mfumo wa kidijitali wa usajili unaojulikana kama TAI Habari. Kabla ya mfumo huo, waandishi waliokuwa wanahitaji vitambulisho vya kazi walilazimika kufika katika ofisi za Idara ya Habari Maelezo kwa ajili ya kujaza fomu kwa njia ya kawaida. Utaratibu huo ulihusisha matumizi ya makaratasi, kupiga picha za pasipoti na kupitia hatua kadhaa za uhakiki zilizoweza kuchukua siku kadhaa kukamilika.

Kupitia mfumo mpya wa TAI Habari, mwandishi anaweza kujisajili akiwa mahali popote nchini bila kulazimika kusafiri kwenda ofisini. Ikiwa nyaraka zote muhimu zimewasilishwa kikamilifu, mchakato wa usajili unaweza kukamilika ndani ya muda mfupi sana, hali ambayo imeondoa kwa kiasi kikubwa urasimu uliokuwa ukilalamikiwa na wadau wa sekta ya habari. Matokeo ya maboresho hayo yanaonekana wazi katika takwimu za usajili. Tangu mfumo wa ithibati ulipoanza kufanya kazi Mei 21, 2025 hadi Machi 10, 2026, jumla ya maombi 4,110 ya usajili yalipokelewa na bodi hiyo. Kati ya maombi hayo, 3,337 sawa na asilimia 81.19 yaliidhinishwa na waombaji wake kupewa ithibati ya kufanya kazi za uandishi wa habari.

Kwa upande mwingine, maombi 240 sawa na asilimia 5.84 bado yanaendelea kufanyiwa kazi, huku maombi 136 sawa na asilimia 3.31 yakikataliwa. Aidha, maombi 397 sawa na asilimia 9.66 hayajakamilika kutokana na baadhi ya waombaji kutokamilisha taarifa au malipo ya ada zinazohitajika.

Ukilinganisha na utaratibu wa awali uliokuwa ukisimamiwa na Idara ya Habari Maelezo, takwimu hizi zinaonyesha ongezeko kubwa la waandishi wanaojitokeza kupata vitambulisho vya kazi. Hapo awali, idadi ya waandishi waliokuwa wakipata vitambulisho kwa mwaka mara nyingi haikuzidi 900.

Awali JAB ilikuwa imeweka lengo la kusajili waandishi kati ya 1,000 hadi 1,200 katika kipindi cha mwanzo cha utekelezaji wake. Hata hivyo, kutokana na urahisi wa mfumo wa kidijitali na kuongezeka kwa uhamasishaji, idadi ya waandishi waliojitokeza imezidi matarajio.

Baada ya kuvuka lengo hilo la awali, bodi iliweka lengo jipya la kusajili waandishi 3,000 ifikapo Desemba 31, 2025. Kufikia tarehe hiyo, jumla ya waandishi 3,839 walikuwa tayari wamesajiliwa, ikiwa ni waandishi 839 zaidi ya lengo lililowekwa, sawa na ongezeko la takribani asilimia 28.

Mafanikio haya yanaonyesha kuwepo kwa mfumo wa kidijitali kumesaidia kupunguza vikwazo vilivyokuwa vinawakwamisha baadhi ya waandishi kuomba vitambulisho vya kazi hapo awali. Waandishi wengi ambao hawakuwa wakijisumbua kuomba vitambulisho kutokana na urasimu uliokuwepo sasa wamejitokeza kwa wingi kupata ithibati.

Kwa mujibu wa takwimu za bodi, kati ya waandishi 3,337 waliopata ithibati, takribani 3,158 sawa na asilimia 94.63 tayari wamechukua vitambulisho vyao vya kazi.

Mbali na kuongeza idadi ya waandishi waliopata ithibati, bodi pia imefanya jitihada za kutoa elimu kwa wadau wa sekta ya habari kuhusu umuhimu wa kuzingatia maadili ya taaluma. Kampeni mbalimbali za uhamasishaji zimefanyika katika vyombo vya habari na taasisi zinazohusika na mawasiliano ili kueleza majukumu ya bodi na umuhimu wa ithibati kwa waandishi.

Miongoni mwa matokeo yanayotajwa kuanza kuonekana ni kupungua kwa baadhi ya malalamiko yanayohusu ukiukwaji wa maadili ya uandishi wa habari yaliyokuwa yakipelekwa kwa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania pamoja na JAB. Kupungua kwa malalamiko hayo kunahusishwa kwa kiasi kikubwa na kuongezeka kwa uelewa wa waandishi kuhusu wajibu wao wa kitaaluma, pamoja na uwepo wa mfumo rasmi wa ithibati unaoweka viwango vinavyopaswa kuzingatiwa katika utekelezaji wa majukumu yao. Hata hivyo, pamoja na mafanikio haya ya mwaka mmoja, wadau wa sekta ya habari wanaona bado kuna changamoto kadhaa zinazohitaji kushughulikiwa ili kuhakikisha mfumo wa ithibati unakuwa na ufanisi zaidi.

Changamoto hizo ni pamoja na uelewa mdogo wa mfumo wa kidijitali kwa baadhi ya waandishi wa zamani, pamoja na haja ya kuendelea kutoa elimu na mafunzo kuhusu maadili ya taaluma ya uandishi wa habari.

Kwa ujumla, mwaka mmoja wa utendaji wa JAB unaonyesha wenye matumaini katika juhudi za kuimarisha taaluma ya habari nchini.

Mafanikio hayo yatakuwa na maana zaidi iwapo changamoto zilizopo zitatambuliwa mapema na kutafutiwa ufumbuzi ili kuifanya bodi hiyo kuwa chombo madhubuti katika kusimamia taaluma hiyo muhimu kwa maendeleo ya jamii.