Dodoma. Utoro kazini na ubadhirifu wa mali za umma bado vinatajwa kuwa sababu kuu zinazopelekea migogoro na hatimaye watumishi wa umma kufukuzwa kazi.
Kauli hiyo imetolewa leo Jumatano, Machi 18, 2026 na Kaimu Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma, John Mbisso wakati akitangaza mkutano wa tatu wa Tume hiyo unaotarajiwa kufanyika jijini Dodoma kuanzia Machi 23 hadi Aprili 15, 2026.
Mbisso amesema katika mkutano wa pili wa Tume uliofanyika mwanzoni mwa mwaka huu mjini Morogoro, rufaa 15 kati ya 88 zilikubaliwa, huku utoro ukiwa miongoni mwa masuala yaliyojitokeza kwa kiasi kikubwa katika malalamiko ya warufani na warufaniwa.
“Masuala ya utoro na ubadhirifu wa mali za umma bado ni changamoto kubwa, ingawa yapo pia matatizo mengine,” amesema Mbisso.
Amewataka watumishi wote walioitwa au walioomba kufika mbele ya Tume kujiandaa kikamilifu, akisisitiza kuwa wanaweza kufika na wanasheria wao au wawakilishi wa vyama vya wafanyakazi ili kuhakikisha haki na uwazi vinazingatiwa.
Amesema uwepo wa wanasheria au viongozi wa vyama vya wafanyakazi utasaidia kupunguza hofu kwa watumishi wakati wa usikilizwaji wa rufaa, hasa wanapokutana uso kwa uso na waajiri wao.
“Tume itatoa nafasi kwa warufani na warufaniwa walioomba kufika mbele yake kutoa ufafanuzi wa ziada kuhusu hoja zao, kwa mujibu wa Kanuni ya 62(1) ya Kanuni za Utumishi wa Umma za mwaka 2022,” ameongeza.
Katika hatua nyingine, Tume imeonya mamlaka zinazoshindwa kutekeleza maamuzi yake, hususan kwa kutowarejesha kazini watumishi walioshinda rufaa, kuwa zitachukuliwa hatua za kinidhamu.
Kwa mujibu wa Mbisso, kabla ya kuanza vikao, Tume hufanya tathmini na katika mkutano uliopita iliziita mamlaka tano kutoa maelezo kwa nini hazikuwarejesha kazini watumishi waliopaswa kurejeshwa.
Amesisitiza kuwa kwa mujibu wa sheria, mtumishi anayeshinda rufaa anatakiwa kurejeshwa kazini mara moja.
Iwapo mamlaka husika haitaridhika na uamuzi wa Tume, inapaswa kukata rufaa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
