Dar es Salaam. Wakati baadhi ya maeneo ya jiji la Dar es Salaam yakishuhudia kukatikakatika kwa umeme nyakati tofauti Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) limesema hali hiyo inatokana na athari zitokanazo na mvua zinazoendelea kunyesha.
Katika siku za hivi karibuni wakazi wa maeneo mbalimbali ya Jiji hilo kama Ubungo, Kimara, Tabata, Goba na Chanika wameeleza kupitia changamoto hiyo ya umeme kukatika zaidi ya mara moja kwa siku.
Akizungumza na Mwananchi leo Jumatano, Machi 16, 2026, Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano na Huduma kwa Wateja wa Tanesco, Irene Gowelle amesema kimsingi hakuna tatizo kubwa linalosababisha umeme kukatwa.
“Bali athari za mvua kama upepo kuwa mkali unaoweza kuangusha nguzo, au matawi ya miti kudondokea kwenye miundombinu ya umeme ndizo zinawalazimu kusitisha huduma ili warekebishe changamoto kwa lengo la kurejesha huduma bila kuleta madhara kwa wananchi,” amesema.
Hata hivyo, amesisitiza mvua haina uhusiano wowote na umeme kukatwa bali athari zake ndizo zinaweza kusababisha huduma ya umeme kuweza kusitishwa.
Mkazi wa Tabata Kimanga, Anitha Julius anasema japo si sana lakini umeme umekuwa ukikatika na kurudi suala linalomletea kero na mshangao wa nini kunakuwa na hali hiyo na wahusika wapo.
“Huwa najiuliza kuna nini au ndio mvua hizi naomba kama kuna matengenezo yafanywe yaishe ili tuendelee kupata huduma hii kwa uhakika,” amesema.
Raphael Nathan kutoka Kimara anasema umeme kuna siku unakatika usiku mzima unarudi kesho yake mchana.
“Umeme hasa siku za Jumanne za majuma mawili yaliyopita umekuwa ukikatika siku nzima au ukakata na kurudi zaidi ya mara moja,” amesema.
Mkazi wa Tabata Magenge, Rashid Hassan, amesema umeme unakatika mara kwa mara hasa kuanzia saa tatu usiku unakaa saa mbili kisha unarudi.
“Imekuwa ikijirudia karibu kila siku wiki ya pili sasa kwa mchana sijajua kwa kuwa nashinda kazini,” amesema.
Wakazi wa Chanika wameonyesha kushangazwa na hali hiyo wakisema kama kuna matengenezo mbona hayaishi, “hii hali karibu kila siku sasa mnakata umeme usiku hasa maeneo ya Kidugalo yaani mnataka tuibiwe sasa na hizi sikukuu,” amesema Ramadhan Hamis.
Mariam Hamad kutoka Ubungo Kibangu amesema umeme umeanza kukatika usiku katika siku za hivi karibuni suala linalomshangaza tatizo nini haswa, kama anavyosema mkazi wa Goba Hassan Anwar kwamba usiku ndio umeme unakatika kwa saa mbili hadi mbili na nusu kisha unarudi jambo ambalo ni tofauti na zamani.
“Sijajua nini kinaendelea haswa kwa sababu tatizo hili halikuwepo zamani, nafikiri watatupatia taarifa zaidi,” amesema.
Gowelle amesema athari zinazotokana na ongezeko la mvua zinazonyesha zimekuwa zikisababisha usumbufu ambao muda mchache huduma ya umeme inakosekana baadhi ya maeneo.
“Wateja wakishazoea mfululizo wa upatikanaji wa huduma halafu ukaanza usumbufu lazima walalamike lakini kimsingi hakuna tatizo kubwa na maboresho yanaendelea kufanyika katika maeneo ambayo changamoto hiyo inatokea, kuhakikisha huduma inaendelea kupatikana bila usumbufu,” amesema.
Katika hatua nyingine, shirika hilo linatarajia kutumia teknolojia ya ‘drones’ kukagua na kufuatilia changamoto mbalimbali katika njia zake za kusafirisha na kusambaza umeme ili kuweza kugundua tatizo kabla na kulifanyia kazi kwa haraka.
Hayo yamesemwa jana Jumanne Machi 17, 2026 na Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo, Lazaro Twange, alipokuwa akizindua mfumo wa matumizi ya vifaa hivyo, ofisi za Tanesco Ubungo Jijini Dar es Salaam.
Twange amesema mpaka sasa wana njia za kusafirisha umeme zilizotembea kilomita 8,500 na njia za kusambaza umeme zilizotembea urefu wa takribani kilomita 280,000 ili kuweza kuwahudumia wateja wao vizuri.
Kati ya hizo zipo zilizopita kwenye mapori yenye wanyama wakali, pembezoni mwa barabara, pia zipo zinazopita kwenye mitaa na maeneo chepechepe kutokana na mabadiliko ya tabianchi.
Wakati hali ikiwa hivyo amesema kazi yao ya kuhudumia wateja moja ya kitu wanachopambana ni kuhakikisha wanapata huduma wakati wote, japo kuna wakati miundombinu yao hupata hitilafu na ndio maana huwa wakitoa matangazo ya mara kwa mara ikiwemo picha kuonyesha maeneo yaliyoathirika na juhudi wanazochukua kutatua tatizo.
