Simiyu. Viongozi wa dini wameonywa kutojikita katika kutafuta utukufu wa wanadamu bali kumtukuza Mungu, wakihimizwa kusimama katika ukweli wa Injili bila kuficha maovu.
Aidha, wamekumbushwa kuwa kupindisha mafundisho kwa lengo la kuwafurahisha watu kunaweza kulidhoofisha Kanisa.
Wito huo umetolewa leo Alhamisi Machi 19, 2026, mkoani Simiyu katika Misa Takatifu ya kumsimika Askofu wa kwanza wa Jimbo jipya Katoliki la Bariadi, Prosper Lyimo.
Akitoa mahubiri kwenye misa hiyo, Askofu wa Jimbo Katoliki la Rulenge – Ngara, Severine Niwemugizi amesema viongozi wa dini wanapaswa kuhubiri Injili kwa uaminifu bila kupotoshwa na matakwa ya wanadamu.
“Ushauri wangu ni kumtumaini Mungu wala siyo binadamu. Hujaja kufanya kazi ya kufurahisha wanadamu, bali umepata kibali kwa Mungu kuwa mchungaji mkuu hapa Bariadi (Askofu Lyimo). Zingatia wosia wa Mtume Paulo kwa Wathesalonike kwamba maonyo yetu si ya ukosefu, wala ya uchafu au hila, bali tumekabidhiwa Injili tuitangaze kwa kumpendeza Mungu anayechunguza mioyo yetu,” amesema.
Ameongeza kuwa wachungaji hawapaswi kuficha maovu wala kutafuta sifa za wanadamu, bali wanapaswa kutafuta utukufu wa Mungu.
Amesema katika ulimwengu uliojaa mashaka, uwepo wa Askofu Lyimo utaleta faraja na matumaini kwa waamini, huku uongozi wake ukitarajiwa kuwahamasisha kufuata njia ya Kristo na kujenga jumuiya imara za Kikristo.
“Jina Prosper linabeba maana ya mafanikio; hivyo wana Bariadi wana bahati kwa kutumiwa kiongozi atakayechochea ustawi wa kiroho na kimwili,” amesema.
Baadhi ya viongozi wa serikali Mkoa wa Simiyu waliohudhuria sherehe ya kusimikwa kwa Askofu Prosper Lyimo kuwa askofu wa kwanza wa Jimbo jipya la Bariadi la kanisa Katoliki. Picha na Samwel Mwanga
Aidha, amesema licha ya upole wake, Askofu Lyimo anayo misimamo imara, akiwataka waamini kuwa tayari kupokea mafundisho ya haki hata pale yanapokuwa magumu.
Amesema kuanzishwa kwa Jimbo la Bariadi ni ishara ya ukuaji wa Kanisa Katoliki na ongezeko la waamini nchini, akibainisha kuwa mwaka 1997 kulikuwa na majimbo 25, huku sasa yakifikia 37.
Kwa upande wake, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) na Askofu wa Jimbo Katoliki la Lindi, Wolfgang Pisa amesema kuanzishwa kwa jimbo hilo ni hatua muhimu kihistoria, akibainisha kuwa Askofu Lyimo ana uzoefu wa kutosha katika utume.
Amesema ipo changamoto ya kishawishi cha Kanisa kuendana na dunia, akisisitiza kuwa ili kuhubiri Injili kwa ufanisi, ni lazima Kanisa liitambulishe dunia kwa Kristo badala ya kufuata mkondo wake.
“Kanisa likiandamana na dunia linaweza kupoteza mwelekeo na kushindwa kusimama imara,” amesema.
Naye Askofu wa Jimbo Kuu Katoliki la Mwanza, Renatus Nkwande amewataka waumini kushirikiana na Askofu wao mpya katika kuendeleza kazi ya Injili, huku akisisitiza umuhimu wa kusimamia ukweli bila woga.
Akitoa tafakari, amemrejelea Mtakatifu Yosefu kama mfano wa uadilifu na ujasiri, akisema alisimama katika ukweli hata katika mazingira magumu, akilinda kile alichokabidhiwa na Mungu.
Akizungumza katika Misa hiyo Takatifu, Balozi wa Baba Mtakatifu nchini, Askofu Mkuu, Angelo Accattino amemtaka Askofu Lyimo kuwa jasiri na mbunifu katika kulijenga jimbo hilo jipya.
“Kuweka msingi wa jimbo jipya si kazi rahisi; kunahitaji ubunifu, mipango thabiti na mikakati ya maendeleo endelevu,” amesema.
Katika hatua nyingine, Rais Samia Suluhu Hassan ametoa mchango wa Sh50 milioni kusaidia ujenzi wa Kanisa Katoliki katika Jimbo jipya la Bariadi.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anamringi Macha akizungumza wakati wa sherehe ya kumuingiza kazini Askofu, Prosper Lyimo wa Jimbo jipya la kanisa Katoliki Bariadi. Picha na Samwel Mwanga
Akizungumza kwa niaba yake, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anamringi Macha amesema mchango huo unalenga kuunga mkono juhudi za taasisi za dini katika kuchochea maendeleo ya nchi na wananchi.
“Taasisi za dini zimekuwa na mchango mkubwa katika kudumisha amani, mshikamano na maadili katika jamii,” amesema.
Kwa upande wake, Askofu Prosper Lyimo amemshukuru Mungu kwa uteuzi huo, akisema ni neema na dhamana kubwa kwake.
Ameahidi kushirikiana na waamini wote kuimarisha huduma za kiroho na kujenga umoja na mshikamano huku akitoa shukrani kwa Baba Mtakatifu Francis kwa kumteua, pamoja na Rais Samia kwa mchango wake.