Arusha. Askofu wa Dayosisi ya Kaskazini ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk Frederick Shoo amependekeza neno “haki” liingizwe katika wimbo wa Taifa ili kusisitiza umuhimu wa kutekeleza haki, amani na maendeleo endelevu nchini.
Akizungumza katika jukwaa la wazi lililowakutanisha viongozi wa dini kutoka madhehebu mbalimbali na vijana, lililofanyika jijini Arusha, Dk Shoo amesema kuwa matukio makubwa yaliyotokea katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 bado yameacha maswali yasiyo na majibu katika mioyo ya vijana huku wakitamani kuona haki inatendeka.
“Isifike wakati tusione sauti za haki zinasumbua masikio yetu na dhamiri zetu zisizungumzwe, mimi natamani uwepo wa neno ‘haki’ kwenye wimbo wetu wa Taifa ili tuone umuhimu wa kutendeana haki bila ubaguzi wa dini au vyama na kuhakikisha Tanzania inaendelea kuwa taifa lenye umoja, upendo, utulivu, na maendeleo kwa wote,” amesema Dk Shoo.
Askofu huyo ameongeza kuwa yaliyotokea katika uchaguzi mkuu yameacha machungu na majeraha kwa baadhi ya watu na familia, ambayo hadi sasa bado hayajapatiwa majibu.
“Haya yaliyotokea yanafikirisha na tunajiuliza kwanini Tanzania tumefikia hapa, tunamuomba Mungu yasije kutokea tena hapa nchini,” amesema.
Dk Shoo amebainisha kuwa licha ya utulivu kuanza kurejea, mioyo ya wengi bado ina maswali mazito.
“Ni haki ya vijana kuwa na maswali na haki ya kuongea ni muhimu ili kuendeleza tunu ya amani katika taifa hivyo wapewe jukwaa au meza ya majadiliano wayaseme bila kuwachoka.”
Amesema changamoto zinazowakabili vijana, ikiwemo uhaba wa ajira, fursa finyu za kiuchumi, hisia za kutoshirikishwa katika uamuzi, na kupungua kwa imani katika mifumo ya kidemokrasia, ni miongoni mwa kiu yao na ndio chanzo cha kupaza sauti zao.
“Hali hii isipopatiwa majibu sahihi kwa wakati inaweza kuathiri mshikamano wa kijamii na amani yetu ya muda mrefu, na kupelekea wengi kupoteza matumaini,” amesema na kuongeza: “Hakuna mtu hatari kama kupoteza matumaini ndio maana nataka tuone umuhimu wa majadiliano.”
Amesema: “Wahenga wamesema hakuna cha kushindikana watu wanapokaa na kuzungumza walimaaniaha Meza ya majadiliano itatupa fursa ya kusikilizana kwa uaminifu na kujenga madaraja ya uelewano, kuibua suluhu zinazojenga, si kubomoa.”
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), Sheikh Khamis Mohamed Mataka amesema taifa lenye haki linaweza kudumisha amani na usalama huku akisisitiza kuwa haki inatakiwa kuendana na wajibu.
“Vijana, mnapodai haki, angalieni wajibu wenu katika taifa hili. Pia, mzingatie namna bora ya kuwasilisha maombi yenu ili kuepuka migongano ya kimaslahi na sintofahamu,” alieleza.
Sheikh Mataka alitumia jukwaa hilo kuitisha meza ya majadiliano kati ya wizara na vijana wa makundi mbalimbali nchini, ili kujua madai yao na kujadiliana namna bora ya kutengeneza mustakabali mwema wa taifa katika kizazi kijacho.
Mratibu wa jukwaa hilo, Israel Ilunde, Mkurugenzi Mtendaji wa The Youth Partnership Countrywide (YPC), amesema kuwa lengo ni kujadili yaliyotokea katika uchaguzi wa mwaka 2025 na jinsi ya kusonga mbele kama taifa.
“Mengi yaliyotokea yanapaswa kujadiliwa kwa mapana na marefu ili kutatua matatizo na kuhakikisha hayajatokei tena,” amesema.
Mmoja wa vijana, Iddi Mohamed amesema upo umuhimu wa kujieleza na haki ya kutoa maoni nchini.
“Isifike mahali ambapo kutoa maoni au kuhoji jambo liwe jambo la kihalifu. Tukifikia huko, naamini tutajenga taifa moja, kuliko sasa hivi ukitoa maoni tofauti uko hatarini kushtakiwa,” amesema.
