Kelele za malori mazito yaliyokuwa yakibeba makaa ya mawe na mizigo mingine mikubwa zimekuwa sehemu ya maisha ya kila siku kwa wakazi wa Mtwara kwa miaka kadhaa sasa.
Lakini hali hiyo inatarajiwa kubadilika kadri ujenzi wa bandari mpya maalumu ya mizigo mikubwa katika Kisiwa cha Mgao unavyoendelea kushika kasi.
Mradi huo unaotekelezwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kwa gharama ya Sh434.5 bilioni umefikia asilimia 38.5 ya utekelezaji na unatarajiwa kukamilika Julai mwaka ujao.
Bandari hiyo mpya inalenga kushughulikia mizigo mikubwa na yenye hatari kama makaa ya mawe, saruji, mbolea ambayo kwa sasa imekuwa ikipitia Bandari ya Mtwara na wakati mwingine kusababisha changamoto za kimazingira na msongamano wa shughuli za usafirishaji ndani ya mji.
Akizungumza maendeleo ya bandari hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Plasduce Mbossa, anasema ujenzi wa bandari hiyo ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuboresha miundombinu ya bandari na kuifanya Mtwara kuwa kitovu muhimu cha biashara na usafirishaji katika ukanda wa kusini.
Anasema kukamilika kwa bandari hiyo kutasaidia kupunguza msongamano katika Bandari ya Mtwara na kurahisisha ushughulikiaji wa mizigo mbalimbali kwa ufanisi zaidi.
“Bandari ya Kisiwa Mgao itachukua mizigo mikubwa kama makaa ya mawe na mbolea, hivyo kuruhusu bandari ya sasa ya Mtwara kushughulikia zaidi mizigo ya kawaida kama korosho na makontena,” anasema Mbossa.
Kwa mujibu wa Mbossa, mgawanyo huo wa shughuli utaongeza ufanisi katika bandari zote mbili na kupunguza muda wa meli kusubiri kuhudumiwa.
Bandari ya Kisiwa Mgao itakuwa na teknolojia za kisasa ikiwemo mifumo ya mikanda ya kusafirisha mizigo (conveyor belts), mitambo maalumu ya kupakia mizigo kwenye meli na teknolojia za kudhibiti vumbi, hasa kwa mizigo kama makaa ya mawe ambayo imekuwa ikizua hofu ya uchafuzi wa mazingira.
Mhandisi msimamizi wa mradi huo, Hamis Nyembo yeye anasema eneo la bandari hiyo lina mkondo wa asili wa maji unaofaa kwa shughuli za bandari, hivyo kazi ya uchimbaji itakuwa ndogo ili kuongeza kina cha maji kutoka mita tisa hadi kati ya mita 14 na 16.5.
Anasema hatua hiyo itawezesha bandari hiyo kupokea meli kubwa zaidi bila changamoto za kiusalama.
“Faida ya eneo hili ni kwamba lina mkondo wa asili wa maji unaofaa kwa shughuli za bandari, hivyo uchimbaji unaohitajika ni mdogo lakini utaruhusu meli kubwa kuingia na kutoka kwa urahisi,” anasema Nyembo.
Kwa mujibu wa takwimu za TPA, Bandari ya Mtwara kwa sasa hushughulikia zaidi ya tani milioni moja za mizigo kwa mwaka, zikiwemo korosho, makaa ya mawe, mbolea na bidhaa mbalimbali za viwandani.
Hata hivyo, baada ya kukamilika kwa bandari ya Mgao, uwezo wa pamoja wa kushughulikia mizigo kati ya bandari hizo mbili unatarajiwa kuongezeka na kufikia kati ya tani milioni 2.5 hadi milioni 3 kwa mwaka.
Meneja wa Bandari ya Mtwara, Ferdinand Nyathi, alisema bandari mpya haitashindana na ile ya sasa bali itasaidiana katika kuongeza ufanisi wa huduma za usafirishaji.
Alieleza kuwa kwa muda mrefu mizigo kama makaa ya mawe imekuwa ikisafirishwa kwa malori kutoka migodi ya Ngaka mkoani Ruvuma kuelekea Mtwara kwa ajili ya kusafirishwa nje ya nchi, hali iliyosababisha msongamano wa magari na kuongezeka kwa gharama za matengenezo ya barabara.
Kwa kujengwa kwa bandari ya Mgao, shughuli hizo zinatarajiwa kuhamishiwa nje ya mji wa Mtwara na hivyo kupunguza msongamano wa magari mazito na athari za kimazingira kwa wakazi.
“Mgao itachukua mizigo mikubwa kama makaa ya mawe na mbolea, hivyo kuipunguzia mzigo bandari ya sasa ili iweze kushughulikia kwa ufanisi zaidi bidhaa za kawaida,” alisema Nyathi.
Bandari hiyo pia inapangwa kuunganishwa na reli ya kisasa ya Standard Gauge Railway (SGR) inayotarajiwa kuanzia Mtwara hadi Bandari ya Mbamba Bay katika mwambao wa Ziwa Nyasa mkoani Ruvuma.
