Deni la taifa la nchi la Marekani limefikia kiwango cha kihistoria cha dola trilioni 39 sawa na zaidi ya TSH trilioni 100,000, hatua inayokuja wiki chache tu tangu kuanza kwa vita kati ya Marekani, Israel na Iran.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka Associated Press, ongezeko hilo linaakisi shinikizo kubwa la matumizi ya serikali, likijumuisha gharama za vita, sera za kodi pamoja na matumizi ya ulinzi na usalama wa mipaka.
Rais wa Marekani, Donald Trump, ambaye aliwahi kuahidi kupunguza deni hilo wakati wa kampeni zake, sasa anakabiliwa na changamoto ya kusawazisha matumizi makubwa ya serikali na juhudi za kulidhibiti deni hilo linaloongezeka kwa kasi.
Ripoti ya Government Accountability Office inaeleza kuwa ongezeko la deni lina athari kwa wananchi wa kawaida, ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa riba za mikopo ya nyumba na magari, kupungua kwa uwekezaji wa biashara na hatimaye kushuka kwa mishahara.
Mwenyekiti na Mkurugenzi Mtendaji wa Peter G. Peterson Foundation, Michael Peterson, alionya kuwa kasi ya ongezeko la deni ni hatari kwa mustakabali wa kiuchumi wa taifa hilo.
“Tunapaswa kutambua kasi hii ya ongezeko la deni na mzigo mkubwa wa kifedha tunaowaachia kizazi kijacho,” alisema Peterson.
Takwimu zinaonesha kuwa deni hilo limekuwa likiongezeka kwa kasi kubwa, ambapo lilifikia dola trilioni 38 miezi mitano iliyopita, na trilioni 37 miezi miwili kabla ya hapo ikiashiria mwelekeo wa kuendelea kupaa.
Kwa mujibu wa mshauri wa uchumi wa Ikulu, Kevin Hassett, vita dhidi ya Iran tayari vimeigharimu Marekani zaidi ya dola bilioni 12, huku kukiwa bado hakuna uhakika wa lini vita hivyo vitaisha.
Hata hivyo, msemaji wa Ikulu Kush Desai alieleza kuwa pamoja na deni kuongezeka, nakisi ya bajeti imepungua kidogo katika mwaka wa fedha 2025.
Kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Fedha ya Marekani, matumizi ya serikali yalifikia dola trilioni 7.01 huku mapato yakiwa trilioni 5.23, na kusababisha nakisi ya dola trilioni 1.78—ikiwa ni punguzo la dola bilioni 41 ukilinganisha na mwaka uliopita.
Desai alieleza kuwa kupungua kwa nakisi kunatokana na kuongezeka kwa mapato ya kodi, kupunguza ajira serikalini na hatua kali dhidi ya udanganyifu wa misaada ya kijamii.
Hata hivyo, wachambuzi wa uchumi wanaonya kuwa endapo kasi ya ukopaji itaendelea, deni la taifa la Marekani linaweza kufikia dola trilioni 40 kabla ya uchaguzi ujao, hali ambayo inaweza kuleta changamoto kubwa za kiuchumi na kisera kwa taifa hilo.