MATOKEO ya mechi ya leo Alhamisi yataamua mshale wa Simba katika msimamo wa Ligi Kuu Bara upande hatua mbili juu au ubaki hapohapo huku kikosi hicho cha Steve Barker kikiwa na mtihani mbele ya Pamba Jiji.
Ni mechi itakayochezwa saa 10:00 jioni kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza, dimba ambalo wenyeji Pamba Jiji msimu huu hawajapoteza wakiwa hapo, huku pia Simba nayo msimu huu haijapoteza ugenini, hivyo kuna kazi kubwa itaonekana ndani ya dakika tisini.
Mbali na hilo, kwa sasa Simba ina pointi 27 ikishika nafasi ya nne, imeiacha Pamba Jiji hatua tatu pekee ikiwa na pointi 24. Kabla ya jana Singida Black Stars kucheza dhidi ya Tanzania Prisons, Pamba Jiji ilikuwa nafasi ya tano.
Ushindi wa Pamba Jiji leo utakuwa na maana mbili kwa vijana hao wa Francis Baraza ambapo itaweka rekodi ya kuifunga Simba mara ya kwanza kutokana na msimu uliopita kupoteza mechi zote mbili za ligi dhidi ya Simba ikianza kufungwa 5-1 ugenini, kisha ikachapwa 1-0 nyumbani pale CCM Kirumba.
Jambo lingine, ushindi wa Pamba Jiji, itaifanya timu hiyo kuendelea kulinda heshima yao ya nyumbani kwani hivi sasa imecheza mechi nane ikiwa hapo, imeshinda tano na sare tatu, haijapoteza huku ikifunga mabao 13 na kuruhusu manne.
Simba mechi sita za ugenini za ugenini katika ligi ilizocheza msimu huu, imeshinda nne na sare mbili dhidi ya Yanga na Dodoma Jiji, leo ni mtihani mwingine unaomkabili Barker ambaye anataka ushindi ili kuzidi kuifukuzia Yanga kule juu.
Yanga iliyocheza jana na TRA United, kabla ya mechi hiyo ilikuwa na pointi 36 ikiwa kileleni, ikiiacha Simba pointi tisa, huku Wekundu hao wakiwa na viporo viwili ambavyo ikishinda, gepu la pointi na Yanga litakuwa tatu ambalo kama mbio zitaenda hivyohivyo, pengine Dabi ya Kariakoo ijayo inaweza kuamua jambo.
“Tunajua mchezo utakuwa mgumu, nimewaambia wachezaji wangu mechi kubwa chezeni kama wakubwa,” alisema Baraza.
kwa upande wa Barker, alisema: “Tunafahamu si mechi rahisi kulingana na ratiba yetu ilivyo, tumecheza mechi mfululizo ugenini ila hata ukiangalia mpinzani alivyo, ugumu utaongezeka, nimewaanda wachezaji wangu vya kutosha kuhakikisha tunatimiza malengo ya kupata pointi tatu.”
Mechi nyingine leo saa 10:00 jioni itachezwa pale Lake Tanganyika mkoani Kigoma ambapo Mashujaa inayofundishwa na Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ itaikaribisha Azam chini ya Florent Ibenge.
Mashujaa imekuwa na wakati mzuri inapocheza nyumbani, lakini mbele ya Azam, ina mitihani miwili, kushinda lakini pia kufunga bao la kwanza dhidi ya matajiri hao wa Dar es Salaam.
Rekodi zinaonyesha huu ukiwa ni msimu wa tatu Mashujaa inashiriki Ligi Kuu Bara, tayari imekutana na Azam mara nne, haijawahi kushinda wala kufunga bao zaidi ya kupoteza mechi mbili na sare mbili, ikiruhusu mabao matano ilipofungwa 3-0 (Novemba 1, 2023 pale Kigoma) na 2-0 (Februari 15, 2025 pale Chamazi). Zingine matokeo yalikuwa 0-0.
Mashujaa iliyopo nafasi ya 11 na pointi 18 ikicheza mechi 16, Julio kwake hii itakuwa mechi ya tatu tangu akabidhiwe kikosi hicho akianza na ushindi wa 3-1 dhidi ya Mtibwa Sugar, kisha sare ya 1-1 mbele ya Fountain Gate.
Katika msimamo wa ligi, Azam yenye pointi 28 ikiwa nafasi ya pili, inasaka ushindi mbele ya Mashujaa ili kuendelea kushikilia nafasi hiyo.
“Baada ya mechi dhidi ya Yanga tulisafiri na kurudisha vema miili sawa, hivyo kesho (leo) tutaingia uwanjani tukiwa fiti kucheza mchezo huu,” alisema Ibenge.
