LORI LATEKETEA KWA MOTO MOROGORO, MTU MMOJA ASADIKIKA KUFARIKI

Farida Mangube Morogoro

Lori la mizigo lenye namba za usajili T729 BBT pamoja na tela namba T677 BTY limeteketea kwa moto katika eneo la Lugono, karibu na Nyama Choma  Barabara Kuu ya Iringa–Morogoro.
Tukio hilo la Lori kuwaka moto limetokea usiku wa kuamkia March 19  katika mazingira ambayo bado hayajafahamika wazi ambapo limeathiri vibaya sehemu ya mbele ya gari hiyo.
Jeshi la Zimamoto na Uokoaji lilifika  katika eneo la tukio na kufanikiwa kuudhibiti moto huo kabla haujasambaa zaidi, licha ya uharibifu mkubwa uliokwisha kutokea 
Mashuhuda waliokuwepo eneo la tukio, akiwemo mwandishi wa Michuzi Blog, walishuhudia lori hilo likiwa limeteketea huku juhudi za uokoaji zikiendelea.
Kwa mujibu wa taarifa za awali, mtu mmoja anasadikika kupoteza maisha kufuatia tukio hilo. Inadaiwa kuwa mwili wa mtu huyo uliungua vibaya kiasi cha kufanya utambuzi kuwa mgumu, huku mabaki yanayoaminika kuwa ya binadamu yakionekana katika eneo la tukio, ingawa utambuzi rasmi bado unasubiri uthibitisho wa mamlaka husika.
Wakati huo huo, jitihada za kumpata Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro zinaendelea ili kutoa taarifa rasmi kuhusu chanzo cha ajali hiyo, kuthibitisha idadi ya waathirika pamoja na kueleza hatua zinazochukuliwa.
Aendelea kutufuatilia Michuzi Blog na Michuzi Tv ili kupata taarifa zaidi