Wakati ucheleweshaji wa miradi ya maendeleo inayosimamiwa na taasisi za umma ukiendelea kuwagharimu walipa kodi, wadau wa sekta ya ujenzi wameshauri mbinu mbalimbali za kuepukana na hasara hiyo.
Mara kwa mara taarifa za ukaguzi za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) zimekuwa zikieleza kuwa hasara hiyo inatokana na kutokuzingatia vifungu 14.7(c) na 14.8 vya Masharti ya Jumla ya Mikataba ya Kawaida, vinavyotaka mkandarasi alipwe ndani ya siku 56 tangu Mhandisi au Meneja wa Mradi apokee madai na nyaraka za uthibitisho.
Kwa mujibu wa vifungu hivyo, mkandarasi anastahili kulipwa riba kwa fedha ambazo hazijalipwa iwapo malipo hayatafanyika ndani ya muda uliopangwa, huku riba hiyo ikiongezwa kila mwezi hadi deni litakapolipwa.
Mathalan, katika ripoti yake ya mwaka unaoishia Machi 2023 iliyowasilishwa bungeni Aprili 16, 2025, CAG Charles Kichere, ameeleza kuwa ucheleweshaji huo umeisababishia Serikali kulipa ziada ya Sh90 bilioni.
Kiasi hicho cha fedha, kwa mujibu wa CAG, kinahusisha miradi ya ujenzi wa Bwawa la Kidunda, Daraja la Kigongo–Busisi, ujenzi wa minara ya mawasiliano, ukarabati na ujenzi wa masoko na vituo vya mabasi, pamoja na miradi ya maji vijijini inayosimamiwa na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (Ruwasa).
Wadau wa sekta ya ujenzi wanasema kuchelewa kwa malipo kumekuwa chanzo cha ongezeko la gharama za miradi, hali inayosababisha Serikali kulazimika kulipa fedha zaidi ya kiwango kilichokubaliwa awali kwenye mikataba.
Wataalamu wa masuala ya usimamizi wa miradi na wachumi wanaeleza kuwa ni muhimu Serikali kuhakikisha kabla ya kusaini mkataba wowote, fedha za kutekeleza mradi husika zimehakikishwa na ratiba ya malipo kuwekwa wazi.
Mtaalamu wa usafirishaji Prosper Nyaki anasema miradi mingi ya barabara na majengo ya umma imekuwa ikikumbwa na changamoto za kuchelewa kukamilika kutokana na malipo kutofanyika kwa wakati.
“Usimamizi wa karibu ni muhimu. Ni lazima kujua chanzo cha kila ucheleweshaji je, ni mkandarasi ameshindwa kutekeleza wajibu wake au ni Serikali haijatoa fedha kwa wakati? Uwajibikaji lazima uwepo,” alisisitiza mtaalamu huyo.
Aidha, imeelezwa kuwa katika miradi inayofadhiliwa kwa mikopo au misaada kutoka nje ya nchi, masharti ya mikataba huwa na vigezo maalum vinavyohitaji kufuatwa kwa umakini.
Anasema kushindwa kuzingatia masharti hayo kunaweza kusababisha adhabu za kifedha au kuongezeka kwa gharama za mradi.
Nyaki anasema ni muhimu Serikali kufanya tathmini ya kina kabla ya kuingia mikataba na wakandarsi wa nje ili kuelewa masharti yake, ikiwemo riba, ada za usimamizi na adhabu za kuchelewesha utekelezaji au malipo.
Katika baadhi ya miradi, changamoto zimekuwa zikihusisha masuala ya upatikanaji wa maeneo ya ujenzi.
Imeelezwa kuwa wakati mwingine eneo la mradi halijakamilika kisheria au fidia kwa wananchi haijalipwa, hali inayosababisha mkandarasi kushindwa kuanza kazi kwa wakati huku muda wa mkataba ukiendelea kuhesabiwa.
“Serikali inapaswa kuhakikisha masuala ya upatikanaji wa ardhi na fidia yanakamilika kabla ya mkandarasi kupewa notisi ya kuanza kazi. Vinginevyo, tutazidi kuona miradi ikiongezewa muda na gharama kupanda,” anasema mhandisi mmoja wa ujenzi ambaye hakutaka jina lake litajwe.
Pia anapendekezwa kuimarishwa kwa mifumo ya ufuatiliaji na tathmini ili kubaini mapema changamoto zinazoweza kujitokeza wakati wa utekelezaji wa mradi. Hatua hiyo itasaidia kuchukua hatua za haraka kabla gharama hazijaongezeka.
Kwa upande wa uwajibikaji, wadau anasema ni muhimu kuwepo kwa utaratibu wa wazi wa kubaini chanzo cha ucheleweshaji.
“Endapo itathibitika kuwa mkandarasi ameshindwa kutekeleza wajibu wake kwa mujibu wa mkataba, hatua zichukuliwe kwa mujibu wa sheria na makubaliano ya pande zote,” anasema.
Anaongeza kuwa, iwapo ucheleweshaji unatokana na upande wa Serikali kwa mfano kuchelewa kutoa malipo au kushindwa kukamilisha taratibu za awali basi ni lazima kuwe na maboresho ya kiutendaji ili kuzuia hali hiyo kujirudia.
Mtaalamu huyo pia anashauri Serikali kuimarisha mipango ya bajeti kwa kutenga fedha za kutosha kwa ajili ya miradi inayoendelea badala ya kuanzisha miradi mipya bila kukamilisha iliyopo.
Wakala ya Barabara Tanzania (Tanroads) ni miongoni mwa taasisi za Serikali zinazotekeleza miradi mingi ambayo pia hupoteza pesa kupitia njia hiyo, Kaimu Mtendaji Mkuu wake, Ephatar Mlavi, amesema masharti ya mikataba kati ya wakala huo na wakandarasi hutofautiana kulingana na aina ya mradi na makubaliano yaliyofikiwa kati ya pande husika.
Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, Tanroads imetekeleza miradi ya barabara yenye urefu wa zaidi ya kilomita 5,700 katika hatua mbalimbali, ikiwemo barabara zilizokamilika kwa kiwango cha lami na zinazoendelea kujengwa pamoja na madaraja kadhaa makubwa ikiwemo (Kigongo–Busisi) na Daraja la Tanzanite.
Mlavi anasema kutokana na tofauti hizo za kimkataba, wakati mwingine endapo kutatokea ucheleweshaji wa malipo, Serikali hulazimika kulipa gharama za ziada kulingana na masharti yaliyobainishwa katika mkataba husika.
Hata hivyo, amesisitiza kuwa hali hiyo haijitokezi katika miradi yote, kwani baadhi ya mikataba haina kipengele kinachoruhusu malipo ya gharama za ziada pindi malipo yanapochelewa.
Kwa upande mwingine anasema Tanraods huingia mikataba na wakandarasi wenye uwezo wa kutekeleza miradi ya maendeleo kwa ufanisi, hali inayosaidia kuhakikisha kuwa hata pale kunapotokea ucheleweshaji wa malipo kutoka serikalini, kazi za ujenzi zinaendelea badala ya kusimama.
Mchambuzi wa uchumi kutoka Chuo cha Dar es Salaam (UDSM), Wailhelm Ngasamiaku, ameishauri serikali kuimarisha uchunguzi wa kina kwa wakandarasi kabla ya kuwapa zabuni za miradi ya maendeleo, ili kuhakikisha wanakuwa na uwezo wa kifedha na kiutendaji wa kukamilisha kazi kwa wakati hata pale malipo yanapochelewa.
Amesema hatua hiyo itasaidia kupunguza ucheleweshaji wa miradi pamoja na gharama zisizo za lazima zinazoweza kujitokeza wakati wa utekelezaji.
“Ni muhimu kwa serikali kuchunguza kwa makini uwezo wa makampuni ya ujenzi kabla ya kusaini mikataba ya utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo,” anasema.
Kwa mujibu wa Ngasiaku, kuchelewa kukamilika kwa miradi mara nyingi husababisha ongezeko la gharama za utekelezaji, hasa kutokana na mabadiliko ya mara kwa mara ya bei za vifaa vya ujenzi.
Anasema tofauti ya bei za vifaa vya ujenzi kati ya mwaka mmoja na mwingine ni kubwa, hali inayochangiwa na sababu mbalimbali ikiwemo kupanda kwa gharama za malighafi pamoja na mabadiliko ya thamani ya fedha za kigeni.
“Vifaa vya ujenzi ulivyonunua mwaka jana haviwezi kuwa na bei ileile leo. Mabadiliko ya bei pamoja na mwenendo wa thamani ya fedha za kigeni huathiri moja kwa moja gharama za ujenzi,” anasema.
Hata hivyo, amesema kwa kawaida serikali hulipa madeni yake kwa wakandarasi, ingawa wakati mwingine malipo yanaweza kuchelewa kutokana na taratibu za kiutendaji. Kutokana na hali hiyo, amesisitiza umuhimu wa wakandarasi kuwa na uwezo wa kifedha unaowawezesha kuendelea na kazi bila kusimamisha miradi.
“Serikali inapotoa zabuni ya mradi, kwa mfano wa Sh5 bilioni, ni muhimu ihakikishe mkandarasi anayechaguliwa ana uwezo wa kifedha unaolingana na ukubwa wa kazi hiyo. Vinginevyo unaweza kukuta mkandarasi hana mtaji wa kuendesha mradi na hivyo kazi kusimama katikati,” anasema.
Anaeleza kuwa kuchelewesha kwa malipo kwa wakandarasi kunawaathiri wananchi moja kwa moja kwa kuwanyima huduma zinazotarajiwa kutokana na miradi hiyo. Kutokana na hali hiyo, anasisitiza umuhimu wa serikali kuimarisha zaidi mchakato wa kuchagua wakandarasi ili kuhakikisha miradi ya maendeleo inatekelezwa kwa ufanisi na kwa wakati uliopangwa.
