Tabora/Dar. Sakata la zuio la mkutano wa Injili mkoani Tabora limechukua sura mpya baada ya Serikali kuruhusu ufanyike lakini kwa masharti, ikiwamo mmoja wa wainjilisti kutohudhuria.
Mkutano huo unaanza leo Alhamisi, Machi 19–22, 2026 huku muinjilisti Paulo Ndutu akipigwa marufuku kushiriki katika shughuli hiyo.
Katika kikao cha maridhiano kilichoongozwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Richard Abwao na viongozi wa kanisa la CPCT Yerusalem, kimeridhia mkutano wa Injili kufanyika, Abwao akisisitiza utakuwa wa kuhubiri Injili pekee na si vinginevyo.
“Hatutakiwi kuona utoaji wa zawadi au vitu vingine; ni Injili tu. Vilevile muinjilisti Paulo Ndutu hataruhusiwa kushiriki katika shughuli hiyo,” amesema.
Katika kikao cha maridhiano, viongozi wa CPCT waliomba radhi kwa taarifa zao za awali na kukubali kufuata maelekezo ya Serikali.
Awali, viongozi hao walipinga uamuzi wa Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Paul Chacha, kusitisha kufanyika kwa mkutano huo uliotangazwa kuongozwa na mchungaji Dana Morey kutoka Marekani.
Mkuu wa mkoa alidai kubaini kuwepo kwa viashiria vinavyodaiwa kuhusishwa na kampeni ya kuhamasisha mapenzi ya jinsia moja.
Alidai kuwepo kwa kampeni ya kuweka vipeperushi katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Tabora vyenye ujumbe “Maisha Yako Mapya,” pamoja na ugawaji wa mipira ya kuchezea katika shule 55.
Mkuu wa Mkoa wa Tabora Paul Chacha
“Baada ya uchunguzi, ilibainika baadhi ya mipira na vipeperushi hivyo vilikuwa na alama zinazoashiria ujumbe wa kuhamasisha mapenzi ya jinsia moja, jambo lililopelekea kuchukua hatua ya kusitisha mkutano huo,” alisema.
Katibu wa Umoja wa Makanisa ya Kipentekoste Mkoa wa Tabora, Mchungaji Lameck Hazina, alidai kushangazwa na zuio hilo na kwamba muhubiri aliyekuwa aongoze mkutano huo alikuwa na vibali halali.
“Tulifuata taratibu zote na hatuna uhusiano wowote na masuala ya ushoga. Lengo letu ni kuhubiri Injili na kuifikia jamii,” alisema juzi kabla ya jana kuomba msamaha na kueleza kufuata kile watakachoelekezwa na Serikali.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Haki, Amani na Maadili ya Madhehebu ya Dini, Askofu William Mwamalanga amesema kilichotokea Tabora hakipaswi kufumbiwa macho, akihoji uhusiano wa Injili na ugawaji wa mipira.
“Unakwenda kuhubiri neno la Mungu, uhusiano na ugawaji wa mipira wapi na wapi? Neno la Mungu linajitegemea, halisaidiwi na kitu kingine. Serikali ya mkoa ipo sahihi kutilia mashaka suala hilo,” amesema.
Miongoni mwa mabango ya muinjilist Dana Morey kutoka Marekani yaliyopaswa kuondolewa Tabora.
Amesema kama walihitaji kutoa msaada, shule zina uhitaji wa visima; wangehamasisha upandaji wa miti ya matunda au hata kilimo na si kuwapa mipira na vipeperushi.
“Kama viongozi wa dini, hili jambo limetusaidia kuelewa mambo mengi. Niwasihi viongozi wenzangu kuwa makini; unapohubiri Injili basi simama kwenye Injili,” amesema.
