Bei ya gesi barani Ulaya imepanda kwa zaidi ya asilimia 30, baada ya Rais wa Marekani, Donald Trump kutishia kulipua kwa nguvu eneo kubwa la gesi Mashariki ya Kati, huku kukiwa na hofu ya bei ya mafuta ghafi kufikia Dola 200 za Marekani kwa pipa na madhara ya kiuchumi yanayoweza kudumu kwa miaka kadhaa.
Si Ulaya pekee itakayoathirika na athari hizo, bali dunia nzima kutokana na Mashariki ya Kati kuwa kitovu katika uzalishaji wa gesi na mafuta yanayotumika katika mataifa mbalimbali duniani ikiwamo barani Afrika.
Kwa mujibu wa Jarida la Daily Mail la Uingereza, hali hiyo imekuja baada ya Iran kutishia jana usiku kuvuruga kabisa soko la nishati duniani kupitia vita kamili ya kiuchumi, kwa kuongeza mashambulizi ya makombora dhidi ya mitambo ya mafuta na gesi.
Katika hatua mpya ya kuchochea mvutano wa mzozo wa Mashariki ya Kati, vituo vya nishati katika nchi jirani za Ghuba vililazimika kuhamisha wafanyakazi wake baada ya utawala huo kutishia kuvishambulia ndani ya saa chache zijazo.
Hatua hiyo imefuatia shambulizi la anga la Israel dhidi ya eneo kubwa zaidi la gesi asilia duniani, South Pars lililoko Iran, linalochangia takribani asilimia 70 ya uzalishaji wa gesi wa nchi hiyo.
Trump amesema hakujua chochote kuhusu shambulizi hilo, lakini akatishia kulipua kabisa kituo hicho kwa nguvu na uwezo ambao Iran haijawahi kuona iwapo Iran itaendelea kuishambulia Qatar.
Chanzo kimoja chenye ufahamu wa suala hilo kilisema mapema Jumatano kuwa Marekani ilikuwa imearifiwa kuhusu mipango ya Israel kulishambulia eneo hilo la gesi, lakini haikushiriki katika operesheni hiyo.
“Sitaki kuidhinisha kiwango hiki cha vurugu na uharibifu kutokana na athari zake za muda mrefu kwa mustakabali wa Iran,” Trump ameandika katika mtandao wa Truth Social, akiongeza kuwa “hatasita” kujibu mashambulizi.
Mashambulizi ya Iran dhidi ya Qatar yameendelea leo asubuhi, mitambo ya gesi kimiminika (LNG) katika eneo la viwanda la Ras Laffan imewaka moto.
Qatar imesema zimamoto wamefanikiwa kuzima moto katika kituo kikubwa cha LNG baada ya kulengwa na makombora ya Iran, jambo lililosababisha bei za gesi Ulaya kupanda kwa kasi.
Uzalishaji katika eneo hilo ulikuwa tayari umesitishwa kufuatia mashambulizi ya awali, lakini wimbi jipya la makombora limesababisha mioto mikubwa na uharibifu zaidi, kwa mujibu wa taarifa.
Bei za mafuta duniani zilipanda kwa asilimia tano jana, baada ya masoko kuitikia kauli ya kiongozi mpya wa Iran aliyesema vituo vya nishati vya Saudi Arabia, Falme za Kiarabu na Qatar sasa ni maeneo halali ya kushambuliwa.
Gavana wa Mkoa wa Iran, Eskandar Pasalar amesema: “Mwelekeo wa vita sasa umegeuka na kuwa vita kamili ya kiuchumi.”
Wakati huohuo, bei za mafuta kwa waendesha vyombo vya moto nchini Uingereza zimepanda hadi kiwango cha juu zaidi katika kipindi cha miezi 18.
Katika ishara nyingine ya athari za kiuchumi kuanza kuonekana, Trump ameidhinisha meli zenye bendera za nchi nyingine kusafirisha mafuta kuelekea Marekani.
Jana, Waziri Mkuu wa Uingereza, Keir Starmer ameonya kuwa kadri mgogoro huo unavyoendelea kwa muda mrefu, ndivyo utakavyokuwa na athari kubwa zaidi kwa gharama za maisha kwa wananchi.
Wakati huohuo, nchi za Ulaya zimeanza kuchukua hatua za haraka kupunguza athari za kupanda kwa bei ya mafuta kufuatia mashambulizi katika mitambo ya nishati ya Ghuba, ikiwamo kituo kikubwa zaidi cha gesi duniani kilichopo Qatar, hatua inayotajwa kuwa ongezeko kubwa zaidi la mzozo wa kiuchumi katika vita vya Marekani na Israel dhidi ya Iran.
Kwa mujibu wa Reuters, Kampuni ya Mafuta ya Taifa ya Qatar, Qatar Energy, imeripoti uharibifu mkubwa baada ya makombora ya Iran kulenga mji wa viwanda wa Ras Laffan, unaochakata takriban theluthi moja ya gesi kimiminika (LNG) duniani.
Mashambulizi hayo yalikuwa ni jibu kwa Israel baada ya kushambulia eneo kubwa la gesi la Iran.
Aidha, bandari ya akiba ya mafuta ya Saudi Arabia katika Bahari ya Shamu pia ilishambuliwa.
Mashambulizi hayo yaliyolengwa kwa umakini mkubwa yameonesha uwezo wa Iran kuendelea kulipiza kisasi kwa gharama kubwa dhidi ya kampeni ya Marekani na Israel, pamoja na kuonyesha mipaka ya mifumo ya ulinzi wa anga katika kulinda mali muhimu na za kimkakati katika eneo la Ghuba.
Pia, yameibua dalili za ukosefu wa uratibu wa mkakati na malengo ya vita kati ya wahusika wakuu wawili, karibu wiki tatu tangu vita hivyo kuanza.
