Thamani ya ngozi mbichi zilizouzwa sokoni imeongezeka kwa asilimia 35.3 na kufikia Sh3.823 bilioni katika robo mwaka ulioishia Septemba 2025, Ripoti ya uchumi wa kikanda ya Benki Kuu (BoT) inaeleza.
Ripoti hiyo inayoangazia ufanisi katika robo mwaka ulioishia Septemba 2025 inaeleza kuwa utendaji huo ulichangiwa kwa kiasi kikubwa na jitihada zinazoendelea za serikali kutoa mafunzo kuhusu mbinu za kisasa za ufugaji wa mifugo, pamoja na njia sahihi za uchunaji na uhifadhi wa ngozi.
Hali hiyo ilifanya sasa mauzo ya Ngozi kufikia kiwango kilichopo kutoka Sh2.826 bilioni zilizokuwapo mwaka ulioishia Septemba 24 huku ngozi ya ng’ombe ikiongoza kuwa na mauzo ya Sh3.477 bilioni.
Mauzo ya ngozi ya mbuzi yalikuwa kwa Sh287.8 milioni huku kondoo ikiwa kwa Sh58.3 milioni.
Kanda ya Ziwa ilichangia sehemu kubwa zaidi ya thamani ya jumla ya biashara hiyo kwa asilimia 30, ikifuatiwa na kanda ya Dar es Salaam na Kanda ya Kaskazini.
Akizungumzia suala hilo, Sabinus Msafiri ambaye ni mtengenezaji wa viatu vya Ngozi anayekiri kuwa siku za hivi karibuni kumekuwa na ongezeko la watu wanaopenda bidhaa zinazotengenezwa kwa Ngozi.
“Tofauti na zamani, hivi sasa watu wananunua sana viatu vya Ngozi, wanavaa na hata hawaogopi tena bei, tofauti na miaka michache nyuma, nadhani wametambua uimara uliopo ndani yake, hali hii imefanya hata kiwango cha mauzo kuongezeka,” amesema.
Kwa mujibu wake, alilazimika tena kuongeza bidhaa alizokuwa akitengeneza katikati ya mdororo wa kibiashara na alikuwa akiona kuwa biashara inakufa.
“Nilidhani nitakosa cha kufanya maana wateja walipungua sana lakini katikati hapa nilipata soko la kuuza bidhaa mkoani Dar es Salaam na mitandao imenisaidia sana kuvuta wateja kutoka maeneo mbalimbali,” amesema Msafiri.
Lakini ukuaji huu haujashuhudiwa tu kwa wanaotengeneza bidhaa bali umekuwa na faida hadi kwa wauzaji wa ng’ombe na ngozi zenyewe kutoka maeneo mbalimbali mikoani.
Wauzaji hao wamesema, kuchangamka kwa soko hilo kumechangiwa zaidi na kusisimka kwa soko la nyama kimataifa ambalo limeongeza upatikanaji wa ngozi kwa ajili ya utengenezaji wa bidhaa mbalimbali.
“Kiwango cha nyama kinavyokuwa kingi maana yake na Ngozi inayozalishwa baada ya kuchinja inakuwa nyingi, hii inafanya hata wanunuzi kutohangaika, ni fursa ya kuongeza kipato,” amesema.
Akizungumzia katika mtazamo wa kiuchumi, Mchambuzi wa Uchumi, Oscar Mkude amesema wafugaji wengi wa Tanzania bado wanafuga kienyeji huku wakiweka nguvu sana katika kulinda vitu vinavyoweza kuwalete fedha kwa haraka ikiwemo maziwa na nyama.
Hali hiyo imewafanya kutozingatia sana ubora wa ngozi ya mifuko hali inayofanya bidhaa hiyo kukosa soko kutokana na kushindwa kukidhi mahitaji ya soko.
Pia eneo la uchakataji wa Ngozi bado halina watu wengi wanaolifanyia kazi kutokana na watu wanaotoka nje ya nchi kutoa bei inayokaribiana na wale wa ndani.
“Njia pekee tunayoweza kuongeza hili ni kuhamasisha uchakataji Ngozi katika awamu ya kwanza ili kuiongezea thamani hii itasaidia kuongeza bei na fedha tunazopata tofauti na kuuza bidhaa ghafi ambazo hazitupi fedha za kutosha,” anasema.
Amesema mauzo haya pia huenda yamekua kutokana na watu kuhamasika katika utengenezaji wa bidhaa mbalimbali za Ngozi ikiwemo viatu, mikoba na mikanda.
Akieleza njia inayoweza kutumika kuongeza mauzo hayo amesema ni kuwajengea uwezo ili waweze kuwa na ufugaji unaolenga uuzaji wa bidhaa nje ya nchi kwa bidhaa zote ikiwemo nyama, maziwa na Ngozi.
“Tuwafundishe na kuwasaidia namna ya kulinda mifugo yao ili waachane na mihuri ya moto ambayo hupunguza thamani ya Ngozi za mifugo yao na kuwasaidia kubadili mifumo ya ufugaji inayopunguza thamani ya Ngozi,” anasema.
Aidha hotuba ya bajeti ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi ya mwaka 2025/2026 inataja kuimarika kwa soko la ngozi mwaka hadi mwaka huku sababu ikitajwa kuwa ni kukuwa kwa masoko ya bidhaa hizo katika nchi za Nigeria, Kenya, Djibout, Ethiopia, China na Pakistan.
Wizara ilieleza kuwa imewawezesha wamiliki wa machinjio za kisasa zilizo chini ya Ukanda maalumu wa viwanda (EPZA) kwa kuwaondolea kodi ya kusafirisha ngozi nje ya nchi.