Dar es Salaam. Iliyokuwa hadithi ya mapenzi yenye matumaini na ndoto za pamoja, imegeuka simulizi ya kushtua ya mauaji, kufuatia kifo cha msimamizi wa sauti za filamu, Athuman Nyanza anayedaiwa kuuawa na mpenzi wake na mwili wake kufukiwa shimoni.
Tukio hilo limetokea katika Mtaa wa Kimya Kimya, Kata ya Zingiziwa, Chanika jijini Dar es Salaam, ambako mwili wa marehemu uligundulika kwenye shimo lililochimbwa mbele ya nyumba yake, kabla ya mpenzi wake kutoweka.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamanda Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro Jumatano, Machi 18, 2026, uchunguzi wa tukio hilo unaendelea ili kubaini mazingira na chanzo cha mauaji hayo.
Jeshi la Polisi limesema tukio hilo limeibua maswali mengi, na limeahidi kutoa taarifa zaidi kadiri uchunguzi unavyoendelea.
Akizungumza na Mwananchi leo Alhamisi, Machi 19, 2026, rafiki wa karibu wa marehemu, Madebe Lidai amesema kwa sasa familia inasubiri majibu ya vipimo vya vinasaba (DNA) vilivyochukuliwa jana, ili kuthibitisha utambulisho wa mwili huo.
Ndugu, jamaa na marafiki wa marehemu Athuman Nyanza wakiwa kwenye kikao cha mazishi kilichofanyika nyumbani kwa wazazi wake, Chanika, jijini Dar es Salaam.
“Kwa sasa tunasubiri majibu. Tukishayapata ndipo tutakabidhiwa mwili. Jana hatukukabidhiwa mwili, tuliambiwa uchunguzi wa vinasaba ni muhimu kwa ajili ya upelelezi,” amesema Lidai.
Ameongeza kuwa familia inaendelea na vikao vya maandalizi ya mazishi, huku tarehe ya maziko ikitegemea kukamilika kwa taratibu za uchunguzi na kukabidhiwa kwa mwili.
Tukio hilo limeacha simanzi na mshangao kwa ndugu, jamaa na wakazi wa eneo hilo, wengi wakieleza kushindwa kuelewa namna uhusiano uliodhaniwa kuwa wa nguvu unavyoweza kugeuka na kuishia katika tukio la kikatili.
Akisimulia tukio hilo, rafiki wa karibu wa marehemu, Lidai amesema mara ya mwisho kukutana na Nyanza ilikuwa Februari 11, mwaka huu, walipokuwa wakijadiliana kuhusu uhamisho wa mwanawe shule.
“Baada ya kumaliza mazungumzo, aliniambia siku inayofuata angekwenda kwa mpenzi wake Kigamboni na tuwasiliana akirudi. Pia alinisisitizia kuhusu suala la uhamisho wa mtoto wake,” amesema Lidai.
Amesema siku iliyofuata alipokea simu kutoka kwa mwalimu akihitaji namba za usajili wa mtoto, lakini jitihada za kumpata Nyanza zilishindikana baada ya simu yake kutopatikana hewani kwa muda mrefu, hali ambayo haikuwa ya kawaida kwake.
Kutokana na hali hiyo, Machi 13, 2026, Lidai aliamua kwenda nyumbani kwa marehemu Chanika, lakini hakumkuta. Alirejea tena jioni na kukuta taa za nyumba hiyo zikiwa zimewashwa.
“Nilipopiga honi alitoka mpenzi wake akadai yupo hapo kwa ajili ya kufanya usafi na kwamba hata yeye hajaonana na Nyanza kwa muda,” amesema.
Hata hivyo, kilichozidi kuongeza shaka ni kuona shughuli zisizo za kawaida zikiendelea nyumbani hapo.
“Niliona watu wakichimba shimo usiku. Nikamuuliza (mpenzi wake) kama ni kawaida, maana kwa mila zetu si jambo la kawaida. Lakini aliniambia ni kwa ajili ya kutupa taka,” amesema Lidai.
Amesema aliondoka akiwa na mashaka, huku akiendelea kuwasiliana na ndugu wengine kutaka kujua kama kuna yeyote aliyekuwa na mawasiliano na marehemu, lakini hakuna aliyekuwa na taarifa zake.
Mashaka yalizidi kuongezeka siku iliyofuata baada ya kumfuata mpenzi wa marehemu katika duka lao la dawa walilokuwa wamefungua Chanika, lakini majibu aliyopatiwa hayakuwa ya kueleweka.
“Aliniambia hajamuona Nyanza na kwamba mpenzi wake huyo amefanya tukio baya la kuuza nyumba na kumjeruhi mtu, kisha akakimbia. Hapo ndipo mashaka yalipozidi,” amesema.
Kwa mujibu wa Lidai, taarifa hizo zilisambazwa pia kwa ndugu wa marehemu huku mtuhumiwa akiahidi kutoa maelezo zaidi baadaye, jambo lililowasukuma ndugu nao kuanza jitihada za kumtafuta bila mafanikio.
Kadri siku zilivyopita, hali ilizidi kuwa ya kutatanisha baada ya ujumbe wa simu kuanza kusambazwa kwa ndugu na marafiki, ukidaiwa kutumwa na Nyanza.
“Ujumbe ulikuwa unasema tufuatilie mambo ya mtoto kupitia kwa mpenzi wake na kwamba yeye amefanya tukio baya lakini atarudi kuomba msamaha. Lakini tulitambua siyo yeye, hata namna ya uandishi ilikuwa tofauti,” amesema.
Kutokana na hali hiyo, ndugu waliamua kwenda kutoa taarifa Polisi Chanika, hatua iliyosaidia kuanzishwa kwa uchunguzi na kukamatwa kwa mtuhumiwa mkuu ambaye ni mpenzi wa marehemu.
Taarifa zinasema mtuhumiwa huyo alikamatwa na kuhojiwa na Polisi, akasema anajua mahali alipo Nyanza ila aliamua kuzima simu yake.
“Kwa maelezo hayo Polisi walisema kama mtu aliamua kuzima simu, jambo lake linadhaminika hivyo walimtoa kwa dhamana ambayo aliwekewa na dada yake,” alisema Lidai.
Amesema baada ya dhamana hiyo mwanamke huyo hakumpeleka Nyanza bali alianza kuishi kama digidigi na nyumbani kwake Kigamboni alianza kuuza vitu na akabadilisha mwonekano wa mavazi, jambo lililowatia mashaka wapangaji wenzake.
Lidai amesema mashaka yao yalitokana na matukio kadhaa yasiyo ya kawaida, ikiwemo kuchimba shimo usiku na juhudi za kulifukia kwa haraka na jinsi mtuhumiwa alivyobadilika.
“Ndipo tulipowaeleza askari kuwa tuna mashaka na lile shimo lililochimbwa nyumbani kwake na kuomba uchunguzi uanzie hapo,” amesema.
Baada ya kulifukua, ukweli ulifichuka kuwa Nyanza hakuwa ametoweka kama ilivyodaiwa, bali tayari alikuwa ameuawa na mwili wake kufukiwa kwenye shimo hilo ambalo lilifunikwa kwa kifusi cha mawe kuficha ushahidi.
Ameongeza kuwa uchunguzi pia ulibaini kuwa taarifa za kuuza nyumba kwa Sh30 milioni na madai ya kumjeruhi mtu zilikuwa sehemu ya mkakati wa kupotosha ukweli.
“(Mpenzi) alitengeneza hata nyaraka feki za mauziano na kuwahusisha watu wengine ili ionekane kweli. Pia aliwaambia wapangaji wenzake kuwa Nyanza ni kaka yake, si mpenzi wake,” amesema Lidai.
Shimo alilokuwa amefukiwa marehemu Athumani Nyanza nje ya nyumba yake iliyopo mtaa wa Kimya Kimya, Kata ya Zingiziwa, Chanika, jijini Dar es Salaam
Mwananchi imezungumza pia na majirani ambao wametoa ushuhuda kuwa waliwaona watu wakichimba shimo kuanzia jioni hadi usiku, lakini hawakutilia shaka wakidhani ni shughuli za kawaida za nyumbani.
“Hatukujua kama kuna jambo zito linaendelea. Nyumba ya mtu huwezi kuhoji kwa nini anachimba shimo,” amesema jirani mmoja ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini.
Jirani mwingine amesema kuna uwezekano Nyanza aliuawa eneo jingine na mwili wake kuletwa na kufukiwa Chanika usiku, akieleza hawakumuona kwa siku kadhaa kabla ya tukio hilo kugundulika.
Wakati uchunguzi wa tukio hilo ukiendelea, taarifa zilizochapishwa mitandao ambazo hazijathitishwa zimedai mtuhumiwa huyo amekamatwa mkoani Morogoro.
Si Kamanda Muliro wala Kamanda wa Polisi Mkoani Morogoro aliyepatikana kuthibitisha taarifa za kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo.
