Ratiba ya Ligi Yavuruga Ushindani, Simba Yatajwa Kunufaika, Bodi ya Ligi Yatajwa

Ratiba ya Ligi Kuu Bara imezua mjadala mkali miongoni mwa mashabiki, huku wengi wakieleza kutoridhishwa na namna baadhi ya timu zinavyopangiwa michezo yao.

Licha ya msimamo tofauti wa mashabiki, hoja kubwa imekuwa ni tofauti ya idadi ya mechi zilizochezwa kati ya timu mbalimbali, hali inayodaiwa kuibua sintofahamu kuhusu usawa wa ushindani.

Kwa mujibu wa takwimu za sasa, baadhi ya timu tayari zimecheza hadi michezo 17 zikiwemo JKT Tanzania, Namungo FC, Dodoma Jiji FC na Tanzania Prisons.

Timu nyingine zimefikia michezo 16 kama Mtibwa Sugar, Mashujaa FC, Fountain Gate FC, Coastal Union, Mbeya City na KMC FC.

Wakati huo huo, zipo timu zenye michezo 15 kama Yanga, Singida Black Stars, Pamba Jiji FC na TRA United.

Hata hivyo, macho na lawama nyingi zimeelekezwa kwa Simba, ambayo hadi sasa imecheza michezo 12 pekee idadi ndogo ikilinganishwa na wapinzani wake wakubwa.

Mashabiki wengi wanaona hali hiyo kama upendeleo kutoka kwa bodi ya ligi na Tanzania, wakidai kuwa Simba inapewa muda mrefu wa kupumzika, jambo linaloweza kuathiri ushindani wa ligi.

Tangu ilipocheza dabi dhidi ya Yanga Machi 1, 2026 katika Uwanja wa Amaan Complex, ratiba ya Simba imeonekana kuwa na nafasi zaidi ya mapumziko kati ya mechi zake.

Kwa upande wa Simba SC, imekuwa na ratiba ifuatayo:

  • Machi 7: dhidi ya B19 Meja Gen. Isaamunyo

  • Machi 11: dhidi ya Singida Black Stars (Ugenini)

  • Machi 14: dhidi ya TRA United (haikuchezwa kutokana na hali ya hewa)

  • Machi 19: dhidi ya Pamba Jiji (Ugenini)

  • Machi 22: dhidi ya TRA United (Nyumbani)

Wakati huo huo, Yanga imekuwa na ratiba ngumu zaidi kwa kucheza mechi nyingi ndani ya muda mfupi:

  • Machi 5: dhidi ya Singida Black Stars

  • Machi 8: dhidi ya Polisi Tanzania

  • Machi 12: dhidi ya Tanzania Prisons

  • Machi 15: dhidi ya Azam FC

  • Machi 18: dhidi ya TRA United

Tofauti hii ya ratiba imeibua maswali mengi kwa wadau wa soka, huku wengine wakitaka ufafanuzi rasmi kutoka mamlaka husika kuhusu vigezo vinavyotumika kupanga ratiba ili kuhakikisha haki na usawa kwa timu zote.

Mjadala huu unaendelea kushika kasi, huku mashabiki wakisubiri majibu kutoka kwa viongozi wa soka nchini kuhusu tuhuma za upendeleo na usawa wa ushindani ndani ya ligi.