Senegal Yatishia Kususia Mashindano ya CAF Kufuatia Uamuzi wa AFCON

Rais wa Senegal, Bassirou Diomaye Faye

Rais wa Senegal, Bassirou Diomaye Faye, ametoa tamko kali kwa Shirikisho la Soka la Afrika CAF kufuatia uamuzi ulioibua mshtuko mkubwa wa kuipokonya Senegal taji la AFCON 2025 na kulikabidhi kwa Morocco.

Katika kauli ambayo imesambaa kwa kasi katika mitandao ya kijamii na kuzua mjadala mpana miongoni mwa mashabiki wa soka, viongozi na wachambuzi wa masuala ya michezo barani Afrika, Rais Faye amenukuliwa akionesha kutoridhishwa kwa kiwango kikubwa na hatua hiyo ya CAF, akieleza kuwa uamuzi huo umeibua maswali mazito kuhusu uendeshaji wa soka la Afrika na uadilifu wa taasisi zinazolisimamia.

Kwa mujibu wa kauli hiyo, Rais wa Senegal amesema kuwa iwapo CAF haitabadilika na kuendelea kunyonya pamoja na kuingiza rushwa katika soka la Afrika, basi Senegal haitakuwa tayari kushiriki tena michuano yoyote inayoratibiwa na shirikisho hilo.

Amesisitiza kuwa taifa lake haliko tayari kuendelea kuvumilia kile alichokieleza kuwa ni mfumo usio wa haki kwa nchi zinazotafuta usawa na heshima katika mashindano ya bara hilo.

Ameongeza kwa msisitizo kuwa Senegal si taifa dhaifu wala la kuogopa tena, kauli ambayo imeonekana kubeba ujumbe mzito wa kisiasa na kimichezo kwa wakati mmoja. Matamshi hayo yamepokelewa kwa hisia kubwa na sehemu ya mashabiki wa Senegal, ambao wamekuwa wakionesha ghadhabu zao tangu kutangazwa kwa uamuzi huo wa kuinyang’anya nchi yao ubingwa wa AFCON 2025.

Tamko hilo linaonesha jinsi suala hilo lilivyovuka mipaka ya kawaida ya soka na kuingia katika mjadala mpana wa heshima ya taifa, uwajibikaji wa taasisi za michezo na mustakabali wa mashindano ya Afrika.

Kauli ya Rais Faye imeongeza uzito mkubwa katika sakata hilo, huku wengi wakisubiri kuona kama CAF itajibu tuhuma hizo nzito au kuchukua hatua yoyote ya kufafanua msimamo wake.

Kwa ujumla, kauli hiyo imezidi kuongeza presha kwa CAF katika kipindi hiki ambacho taasisi hiyo inakabiliwa na ukosoaji mkubwa kutoka kwa wadau mbalimbali wa soka. Wakati mjadala ukiendelea kushika kasi, macho ya wengi sasa yanaelekezwa kuona hatma ya mzozo huu mkubwa na athari zake kwa soka la Afrika katika siku zijazo.

Stori na Elvan Stambuli, Global Digital