Utoaji wa tuzo hizo umefanyika Machi 19, 2026 katika maeneo mbalimbali ya mji wa Songea, ambapo mamlaka imewafuata katika maeneo yao ya kazi na makazi kwa lengo la kuthamini mchango wao katika matumizi ya huduma ya maji na uwajibikaji wa malipo.
Akizungumza katika zoezi hilo, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa SOUWASA, Baby Biko, amesema hatua hiyo inalenga kuwatambua wateja wanaolipa ankara za maji kwa wakati na kuhamasisha wengine kuiga mfano huo. Amesema mamlaka imeweka vigezo vinavyozingatia matumizi ya maji yanayoendana na ulipaji sahihi wa bili katika makundi yote ya wateja.
Ameongeza kuwa utoaji wa tuzo hizo pia umehusisha wadau wanaoshirikiana na mamlaka katika kulinda miundombinu ya maji kwa kutoa taarifa za uharibifu, wizi wa mita pamoja na uvujaji wa mabomba, hali inayochangia kuboresha huduma kwa wananchi.
Katika kundi la biashara, Nipo Guest House imetunukiwa tuzo kutokana na rekodi nzuri ya ulipaji wa bili kwa wakati, huku Chuo cha Ualimu Songea kikipewa tuzo ya Taasisi kubwa kwa ulipaji wa ankara za maji kwa wakati.
Akizungumza baada ya kupokea tuzo hiyo, Mkuu wa Chuo cha Ualimu Songea, Catherine Thomas Kimboka, ameipongeza SOUWASA kwa huduma wanazozitoa, akieleza kuwa taasisi hiyo imekuwa ikinufaika na upatikanaji wa maji ya uhakika. Amesema hali hiyo imewezesha chuo chenye zaidi ya wanafunzi 400 kudumisha usafi wa mazingira na mazingira bora ya kujifunzia.
Kwa upande wake, Ibrahim Hakimu Faraji, aliyepokea tuzo ya mdau bora anaeshirikiana na Mamlaka kwa utoaji taarifa juu ya changamoto zinazohusu maji, amesema ushirikiano kati ya wananchi na mamlaka ni muhimu katika kulinda miundombinu ya maji. Amesisitiza umuhimu wa kutoa taarifa mapema pindi changamoto zinapojitokeza ili hatua zichukuliwe kwa haraka.
Amesisitiza kuwa mamlaka haiwezi kumzidishia bili mteja, kwani kila mteja hulipa kulingana na kiwango cha maji anachotumia, huku akiwataka wananchi kuendelea kulipa bili kwa wakati na kushirikiana na mamlaka katika kulinda miundombinu ya maji kwa manufaa ya wote.
Katika kuadhimisha Wiki ya Maji Duniani inayoendelea kuanzia Machi 16 hadi 22 chini ya kauli mbiu isemayo “Maji na Jinsia”, SOUWASA imeendelea na shughuli mbalimbali ikiwemo utoaji wa elimu kwa wananchi kupitia vyombo vya habari pamoja na zoezi la upandaji miti katika bonde la Mto Luhira, ikiwa ni sehemu ya kulinda vyanzo vya maji na kuhakikisha huduma inaendelea kuwa endelevu..jpeg)
.jpeg)
.jpeg)
