Dar es Salaam. Je, wewe ni Mtanzania? Unafurahia maisha? Jibu la swali hilo unalijua mwenyewe, lakini Tanzania inashika nafasi za chini katika viwango vya nchi zenye furaha duniani, kwa mujibu wa Ripoti ya Kimataifa ya Furaha ya mwaka 2025.
Kesho, Machi 20, 2026, ni Siku ya Kimataifa ya Furaha (IDH) ambayo huadhimishwa kila mwaka na kutoa tathmini ya kina kuhusu hali ya maisha ya watu katika mataifa yao na mambo yanayochochea au kuzuia furaha yao.
Vigezo vinavyotumika kupanga viwango vya furaha duniani ni pamoja na pato la taifa kwa kila mtu (GDP per capita), kiwango cha msaada wa kijamii, matarajio ya kuishi maisha yenye afya, uhuru wa mtu kufanya uamuzi kuhusu maisha yake, ukarimu wa wananchi kwa ujumla, pamoja na mitazamo ya viwango vya rushwa vya ndani na nje.
Nchi zinazoongoza kwa kuwa na furaha duniani na alama zilizopata kati ya 10, ni Finland (7.74), Denmark (7.52), Iceland (7.52), Sweden (7.35) na Uholanzi (7.31), Costa Rica (7.27), Norway (7.26), Israel (7.23), Luxenmbourg (7.12) na Mexico (6.98).
Kwa upande wa Afrika, nchi zilizo na kiwango cha juu cha furaha ni Tunisia (5.91) ikishika nafasi ya 70 duniani, Mauritius (5.83), Libya (5.81), Algeria (5.57), Afrika Kusini (5.21), Msumbiji (5.19), Gabon (5.12), Ivory Coast (5.10), Jamhuri ya Congo (5.03) na Guinea (4.93).
Tanzania, nchi yenye watu zaidi ya milioni 61, inashika nafasi ya 136 kati ya 147 duniani, nafasi ya 32 kati ya 40 za Afrika, ikiwa na kiwango cha 3.8. Katika Afrika Mashariki, Tanzania iko nyuma ya Kenya na Uganda ambazo zimeshika nafasi ya 115 na 116 mtawalia.
Wataalamu wanaeleza kwamba kutimizwa kwa mahitaji ya msingi kunaweza kuchangia furaha. Hata hivyo, kuwa na fedha nyingi zaidi si lazima kumfanye mtu kuwa na furaha zaidi, anaweza kukosa furaha pia.
Mwanasaikolojia, Charles Kalungu ameeleza kwamba furaha ni hali ya kuridhika na jambo au ni hisia ya kujisikia vizuri. Amesema kuna aina mbili za furaha, ya muda mfupi (hedonic) ambayo huletwa na matukio na ile ya muda mrefu.
Amesema kuna sababu nyingi zinazoweza kuathiri furaha ya mtu; kwanza, ni mtazamo binafsi wa mtu, mazingira aliyopo, watu wanaomzunguka au hali ya maisha kiuchumi, japo hilo haliwezi kuwa sababu ya moja kwa moja.
“Maeneo ya vijijini, watu wengi wana furaha lakini hawana fedha za kutosha. Kwa hiyo, suala la furaha ni mtambuka kidogo.”
Kuhusu nafasi ya Tanzania katika viwango vya furaha, amesema tafiti zimefanyika na zimetoa matokeo hayo, hivyo ni wakati wa kila mmoja kuangalia na kufanyia kazi kitu kinachoondoa furaha yake huku Serikali nayo ikitimiza wajibu wake.
Wakizungumzia kiwango cha chini cha furaha kwa Watanzania, baadhi ya watu wameelezea masuala mtambuka ambayo yanagusa moja kwa moja maisha yao na kuyafanya yasiwe ya furaha kama ilivyo kwa mataifa mengine.
Mkazi wa Tabata, Dar es Salaam, Gabriel Komba amesema yapo mambo mengi yanasababisha watu kukosa furaha ikiwemo suala la kutafuta matibabu, upatikanaji wa huduma za maji, umeme pamoja na ukosefu wa ajira.
Kuhusu maji, amesema katika maeneo mengi nchini, upatikanaji wa maji ni wa kusuasua, jambo ambalo huongeza msongo wa mawazo, namna gani mtu anaweza kusaka huduma hiyo na kuipata kwa wakati.
“Huna maji na hapohapo umeme umekatika, unafanya kazi saluni ya kunyoa watu, hiyo furaha unaitolea wapi, mfano tu huo umeme unarudi unaunguza kila kitu ndani, utafurahi? Kwa hiyo tuna matatizo mengi ambayo yanatufanya tusiwe na furaha,” amesema.
Ameongeza kuwa hata ndugu wa marehemu hawana furaha hata wanapojaribu kusahau mpendwa wao baada ya maziko, wanaweza kukumbushwa machungu kwa Serikali au wawekezaji kutaka kuhamisha kaburi au makaburi kwa madai kwamba eneo linahitajika.
“Bongo hata ukifa hupumziki, utasiki makaburi yanahamishwa, wanafukua kutoa mifupa yako kupeleka sehemu nyingine, msiba unaanza upya kwa ndugu zako, hakuna furaha kabisa,” amesisitiza kijana huyo.
Mbali na hayo, amesema eneo la kazi za kuajiriwa ni changamoto zaidi inayotengeneza watu wavumilivu wa shida kwani kuanzia mkuu wa idara hadi msaidizi hulumbana na wafanyakazi wa chini hadi wafanyakazi huiona kazi kama jehanamu.
“Unaingia kazini asubuhi, bosi anakusema tu muda wote, anatafutia visingizio ili akusulubu. Ukirudi nyumbani nako unakutana na changamoto nyingine za mke, mwenyenyumba au majirani, stress tupu,” amesema.
Kwa upande wake, mkazi wa Mabibo, Said Mrisho amesema kukosekana kwa uhuru wa kutoa maoni na aina ya siasa za Tanzania ni moja ya mambo yanayoondoa furaha ya wananchi kwani wanaishi na madonge mioyoni mwao.
“Siasa zetu ndiyo zimetufikisha hapa, siku hizi ukitoa maoni yako tu unaishia pabaya, kwa hiyo watu tumechagua kuwa kimya. Huo ukimya sasa ndiyo unachochea hasira na kuondoa furaha kabisa,” amesema Mrisho.
Wakati akizindua Bunge la 13, Novemba 14, 2025, Rais Samia Suluhu Hassan aliahidi kuwaacha Watanzania na tabasamu kama jambo watakalolikumbuka katika utumishi wa Serikali yake ya awamu ya sita aliyoiongoza kuanzia Machi 2021 hadi 2030.
“Namuomba Mwenyezi Mungu kuwa mwisho wa utumishi wa Awamu ya Sita usipimwe tu kwa vitu vitakavyoachwa, bali pia kwa tabasamu la utu litakaloachwa kwenye nyuso za Watanzania,” alisema Rais Samia katika hotuba hiyo.