Tujifunze kwa Finland utoaji elimu ya fedha

Fikiria mtoto wa miaka 13 tayari anaelewa kuweka akiba, kupanga bajeti, au kujaribu biashara ndogondogo. Katika makuzi ni umri mzuri wa kujenga na kuzoesha kwa urahisi zaidi kuwa sehemu ya maisha ya mtu.

Nchi ya Finland utoaji wa elimu ya umezingatia msingi huo, programu maalum kujifunza masuala ya fedha binafsi na kipato kwa vitendo maarufu kwa kifini ‘Yrityskylä’ inatolewa kwa Watoto mashuleni na imeleta matokeo mazuri.

Katika programu hiyo wanafunzi wenye umri wa miaka 13 hadi 15 wanashiriki kwa pamoja kujifunza masuala ya kifedha. Inaanza kwa kujifunza dhana za kifedha darasani kulingana na ratiba iliyopangwa, na kisha kushiriki katika zoezi la mfano linalofanana na maisha halisi, ambalo ni kama igizo la maisha ya kila siku.

Mathalan katika taswira ya maisha ya mjini au kijini, wanafunzi wanaonesha ubunifu kwa wanachokipenda mfano kubuni biashara, kuandaa bajeti, kuuza bidhaa, kufanya manunuzi, kupatana bei, na kufanya maamuzi mengine ya kifedha.

Kila mtu anachagua nafasi yake kulingana na anachokipenda, wanacheza nafasi za wafanyakazi, wamiliki wa biashara, maafisa wa umma, wenye maduka, wakaazi wa mji, nk, wakifanya maamuzi ya kifedha katika mazingira yanayofanana na maisha halisi. Kuuza, kununua, kupanga bei, kuomba punguzo la bei, kuanzisha biashara, nk. Zoezi zima linasimamiwa na walimu wenye mafunzo maalum ya ufundishaji elimu ya fedha.

Vilevile, wanafunzi pia wanajifunza changamoto za kifedha zinazoweza kutokea ikiwa mtu hata kuwa na utaratibu mzuri wa kujiongoza, matumizi ya israfu, kutokuwa na bajeti inaweza kumweka mtu katika hali ngumu kifedha, na mengine.

Programu hiyo inatekelezwa kwa ushirikiano kati ya halmashauri za miji, sekta binafsi, na taasisi za elimu. Kwa mujibu wa tovuti ya programu hiyo, asilimia 75 ya watoto wa Kifini katika umri huu wanashiriki programu hiyo.

Tathmini ya ripoti ya ufuatiliaji kuhusu elimu ya fedha kwa nchi za OECD, PISA ripoti ya mwaka 2018, inataja kuwa vijana wa Kifini wa miaka 15 kuwa miongoni mwa walio na uelewa mkubwa zaidi wa masuala ya kifedha duniani.

Mfano huo wa Finland, utaona ni ubunifu wa kutoa mafunzo ambao unakuza uelewa mpana wa uwajibikaji wa kifedha na kiuchumi kwa Watoto wa umri mdogo ambao kiuhalisia wanajifunza na kuelewa kwa urahisi zaidi kwa vitendo kuliko warsha au kipindi cha kawaida darasani.

Kuna mambo kadhaa tunaweza kujifunza kutoka kwenye programu hiyo.

Kwanza, mbinu ya kujifunza kwa vitendo hufanya somo la fedha kuwa la kuvutia na rahisi, hasa kwa watoto. Elimu ya fedha inageuka kuwa zoezi la kusisimua ambapo watoto hujifunza kwa kushirikiana na kufanya majaribio, kama michezo yao ya kawaida. Inaongeza mwamko wa kujifunza kuliko mtindo wa kawaida wa Ubao na chaki.

Pili, mfumo huu unawajengea watoto kwamba fedha ni matokeo ya kitabia, kipato ni matokeo ya kazi. Mtu haonekani tu kwamba anapata ela, lakini kupitia vitendo (simulation) mtoto anajifunza kuwa anatakiwa abuni wazo, afungue biashara, asimamie na kuuza vizuri, mwishowe apate kipato. Mtiririko mzima unafundisha misingi ya uwajibikaji. Katika dunia ambayo vijana wanavutiwa zaidi na njia za mkato mafunzo haya ni muhimu kwa kizazi kinachokuwa.

Tanzania inaweza kujifunza kutoka kwa Finland kwa kusisitiza elimu ya fedha katika ngazi za elimu ya awali. Ufundishaji uwe na taswira na mifano inayohusiana na maisha halisi katika kuwaelezea watoto kuhusu kuweka akiba, matumizi sahihi ya fedha, nk. Vilevile, mbinu shirikishi kama michezo, maigizo, na majaribio zinaweza kutumika kuongeza hamasa ya kujifunza.

Walimu wanapaswa pia kujengewa uwezo kwa kupewa mafunzo maalum ya namna ya kufundisha elimu ya fedha kwa watoto, ili kuwapatia mbinu itakayowawezesha kufundisha elimu kwa rika hilo la Watoto kwa ufanisi.