MWENYEKITI wa timu ya Uhamiaji inayoshiriki Ligi Kuu Zanzibar (ZPL), Ali Juma Abdulkadir amesema kipindi cha mapumziko kwa ajili ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhan kimewafanya wachezaji kupumzisha miili yao.
Alisema hilo limekuwa ahueni kwao ikizingatiwa mechi 10 za mwisho zitachezwa mfululizo, hivyo limewajenga vizuri kimwili na kiakili.
Mwenyekiti huyo alisema Uhamiaji ya msimu wa 2025-2026 siyo iliyozoeleka miaka yote inapambana isishuke daraja, bali msimu huu ipo kwa ajili ya kutafuta ubingwa wa ligi hiyo.
“Malengo ya msimu huu ni kumaliza tukiwa na mataji mawili au moja ndiyo maana michezo yote iliyobaki tumesema ni kama fainali kwetu,” alisema.
Alisema timu hiyo itaanza mazoezi siku ya pili ya Eid ili kuona kwa namna gani kocha wa timu hiyo anakifua kikosi hicho kuelekea mechi za kumaliza msimu.
Aliongeza, uamuzi wa kuanza mazoezi kipindi hicho umetokana na ratiba ya ligi kuwa ndefu kwa upande wao, hivyo hawana ulazima wa kuanza ndani ya mwezi wa Ramadhan.
Alisisitiza, timu hiyo itakuwa bora zaidi ya iliyocheza michezo iliyopita kabla ya kusimama kwa ligi hiyo kupisha mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan.
Uhamiaji FC ipo nafasi ya nne katika msimamo wa Ligi Kuu Zanzibar ikiwa na pointi 36 ilizovuna katika mechi 20 ilizocheza na baada ya ligi kurejea, timu hiyo itacheza ugenini dhidi ya Junguni United kwenye Uwanja wa Gombani uliopo Pemba, Aprili 2,2026.