Umuhimu wa sikukuu kwa biashara ndogo

Ingawa wengi huona kipindi cha sikukuu kama muda wa mapumziko na ibada, nyuma ya pazia kuna gurudumu kubwa la kiuchumi linalozunguka kwa kasi ya ajabu.

Katika muktadha wa Tanzania, msimu huu si tu wakati wa kula pilau na kutembelea ndugu, bali ni “mzunguko wa dhahabu” kwa biashara ndogo na za kati (SMEs), hasa zile zilizoko maeneo ya vijijini ambazo ndizo kitovu cha uzalishaji wa chakula na malighafi.

Uchumi wa sikukuu nchini Tanzania unachochewa na utamaduni wa “kurudi nyumbani.” Maelfu ya watu husafiri kutoka mijini kama Dar es Salaam, Mwanza, na Arusha kuelekea vijijini mwa mikoa ya Kilimanjaro, Kagera, Mbeya, na kwingineko. Mtiririko huu wa watu unaambatana na mtiririko mkubwa wa fedha taslimu kwenda vijijini.

Hapa ndipo SMEs za vijijini kuanzia wasafirishaji, wasindikaji wa mpunga, wamiliki wa maduka ya rejareja, hadi wafugaji wadogo wanapopata fursa ya kipekee ya kuongeza kipato chao cha mwaka. Kwa mfanyabiashara mdogo wa kijijini, mauzo ya wiki mbili yanaweza kulingana na mauzo ya miezi mitatu ya kawaida.

Sekta ya kilimo, ambayo ndiyo uti wa mgongo wa vijijini, ndiyo mnufaika mkuu. Takwimu zisizo rasmi zinaonyesha kuwa mahitaji ya mchele, kuku, na nyama ya ng’ombe huongezeka zaidi wakati wa kipindi cha sikukuu.

Kwa wakulima wa mpunga, huu ndio msimu ambapo bei ya mazao yao hupaa kutokana na mahitaji makubwa ya walaji wanaotaka sherehe zenye hadhi.

Hata hivyo, ili mkulima au mfanyabiashara wa kijijini anufaike kikamilifu, matumizi ya teknolojia kama ‘Power Tillers’ na mashine za kusindika yamekuwa nguzo muhimu. Kupungua kwa muda wa kuandaa mashamba na kuongezeka kwa ubora wa bidhaa kumewafanya vijana wengi vijijini kuiona sekta hii kama fursa ya kibiashara na si utumwa wa suluba.

Aidha, msimu huu unadhihirisha nguvu ya biashara ndogo katika sekta ya usafirishaji na huduma. Pikipiki (boda boda) na magari madogo ya mizigo vijijini hufanya kazi usiku na mchana kusambaza bidhaa na abiria.

Hii inatengeneza mzunguko wa fedha ambao huishia mikononi mwa mama ntilie, mafundi gereji, na wauzaji wa mafuta ya petroli maeneo ya ndani kabisa. Ni mfumo wa kiuchumi ambao unajitegemea na unaonyesha kuwa, kukiwa na miundombinu bora, vijijini kunaweza kuwa kitovu cha ukuaji wa uchumi wa kitaifa kupitia biashara ndogo ndogo.

Lakini, pamoja na fursa hizi, bado kuna changamoto zinazozuia SMEs hizi kukua zaidi. Ukosefu wa mikopo yenye riba nafuu na changamoto za uhifadhi wa mazao husababisha baadhi ya wakulima kupoteza sehemu ya faida yao. Sera za serikali zinapaswa kuelekezwa katika kuimarisha uwezo wa SMEs za vijijini si tu wakati wa sikukuu, bali mwaka mzima.

Kuimarisha usajili wa biashara hizi na kuzipa mafunzo ya usimamizi wa fedha kutawezesha fedha zinazopatikana mwezi Desemba kuwa mtaji wa kudumu wa kuendeleza miradi mikubwa zaidi mwezi Januari.