Usafiri kikwazo ufuatiliaji elimu, mwarobaini watolewa

Unguja. Licha ya maendeleo ya elimu kuanza kuimarika Zanzibar, imebainika kuwa ukosefu wa usafiri kwa maofisa elimu wa mikoa na wilaya unashusha ufanisi, kutokana na kushindwa kufuatilia utendaji wa shule, hasa zile zilizopo maeneo ya vijijini.

Kutokana na hali hiyo, Serikali imenunua pikipiki 15 kwa ajili ya maofisa wa wilaya na mikoa yote ya Zanzibar, ili kuimarisha ufuatiliaji wa shughuli za kila siku katika shule zilizopo ndani ya mikoa na wilaya zote za Unguja na Pemba. Zanzibar ina wilaya 11 na mikoa mitano.

Hatua hii inatarajiwa kuongeza uwajibikaji, kuboresha utoaji wa huduma za elimu na, hatimaye, kuinua kiwango cha ufaulu wa wanafunzi.

Akizungumza wakati wa kukabidhi pikipiki hizo katika viwanja vya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Unguja, Machi 19, 2026, Katibu wa Wizara, Khamis Abdulla Said, amesema kuwa katika mpango wa Serikali wa mageuzi makubwa ya elimu, lengo ni kushuka hadi ngazi ya wilaya, kwani ndicho kitakuwa chombo muhimu zaidi cha kuimarisha ubora wa elimu.

“Siyo rahisi katibu mkuu au watendaji wengine wizarani kutembelea shule zote, lakini maofisa elimu wa wilaya wao wanazijua shule na kuzitembelea, lakini hawana vifaa. Wakati mwingine tulikuwa tunawalaumu hatuoni kinachofanyika, lakini pengine ni kwa sababu ya kukosa vifaa, kwa hiyo Serikali imeliona hilo na kulifanyia kazi,” amesema.

Pamoja na pikipiki hizo, wizara pia imenunua magari mawili yatayosaidia kusafirisha vifaa shuleni, na kwa sasa ilikuwa na gari moja, hivyo kusababisha changamoto ya usafirishaji wa vifaa vinapohitajika.

Khamis amesema Serikali ilianza kujenga ofisi za watendaji hao na sasa imewezesha vitendea kazi, kwa maana ya usafiri, ili kuhakikisha wanatembelea kila shule na kuimarisha ubora wa elimu Zanzibar.

“Hii ni kwa ajili ya kufanya ufuatiliaji katika maeneo yenu, kwa kuwapa nguvu walimu wakuu wachukue hatua inapotokea mambo ya nidhamu. Wilaya mnatakiwa kuwasimamia, maana hata wizara imeshatoa maelekezo kwa sasa walimu wakuu hawafundishi, badala yake kazi yao ni kusimamia uendeshaji wa shule,” amesema.

Naye Meneja Mradi wa Kuboresha Elimu ya Lazima Zanzibar (ZIQUE), unaofadhiliwa na Benki ya Dunia, Juma Haruna Mwenga, amesema pikipiki hizo zina thamani ya Sh75.9 milioni, ambapo bei ya kila moja ni Sh5.060 milioni.

“Ununuzi wa vitendea kazi hivi ni sehemu ya juhudi za kuongeza ufanisi katika usimamizi na ubora wa elimu.”

Mwenga amesema kukabidhiwa kwa pikipiki hizi kutawawezesha maofisa elimu kufika kwa urahisi katika shule zilizopo maeneo mbalimbali ndani ya mikoa yao na wilaya zao.

“Kupitia uwezeshaji huu, maofisa elimu watafanya ukaguzi wa mara kwa mara, kufuatilia mahudhurio ya walimu na wanafunzi, kusimamia utekelezaji wa mitaala, pamoja na kutatua changamoto zinazojitokeza kwa wakati muafaka,” amesema.

“Maofisa elimu wanahimizwa kutumia vyombo hivi kwa uangalifu na kwa malengo yaliyokusudiwa, ili kuhakikisha vinadumu na kuleta matokeo chanya yaliyotarajiwa.”

Akizungumza kwa niaba ya maofisa wengine, Ofisa Elimu Mkoa wa Mjini Magharibi, Mohamed Abdalla Moh’d, amesema pikipiki hizo zitawasaidia kuyafikia maeneo mengi ambayo walishindwa kuyafikia.

“Tunashukuru wizara kutuwezesha usafiri. Kwa kweli, ilikuwa changamoto kubwa kwetu, lakini hapa tunaamini tutafika shule zote na kusimamia ubora wa elimu kwa kufika hata shule zilizopo pembezoni,” amesema.