Dar es Salaam. Siku moja baada ya Tume ya Rais ya Kutathmini Maboresho ya Mfumo wa Kodi kuwasilisha mapendekezo 284 mbele ya Rais Samia Suluhu Hassan, wadau wamesema kuwa, ikiwa kilichosemwa kitatekelezwa kikamilifu, mageuzi makubwa yatashuhudiwa.
Miongoni mwa mapendekezo yaliyotolewa ni mabadiliko katika sekta ya kodi, ikiwamo kubadili jina la Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na kuitwa Huduma za Mapato Tanzania (TRS).
Tume hiyo, iliyoongozwa na mwenyekiti wake, Balozi Ombeni Sefue, ilianzishwa Julai 31, 2024 na kuanza kazi Oktoba 4, 2024, imekuja na mapendekezo hayo baada ya tathmini kuonesha mfumo wa kodi kuwa na dosari kadhaa zinazoathiri walipa kodi na mazingira ya uwekezaji.
Akiwasilisha mapendekezo hayo jana, Jumatano, Machi 18, 2026, wakati wa kukabidhi ripoti hiyo kwa Rais Samia Suluhu Hassan, Balozi Ombeni Sefue amesema katika mageuzi ya sera na sheria, tume imependekeza kuimarishwa kwa mfumo wa kisera na kisheria, ili kuweka mwongozo wa kitaifa unaoeleweka na misingi madhubuti ya uandaaji na maboresho ya kodi.
Miongoni mwa mapendekezo hayo ni kufutwa kwa baadhi ya sheria zilizopitwa na wakati, ikiwamo sheria ya ushuru wa bidhaa ya sasa, badala yake kutungwa sheria mpya ya ushuru wa bidhaa na huduma itakayozingatia mazingira ya uchumi wa kisasa.
Vilevile, tume imependekeza kutungwa upya kwa sheria ya ushuru wa stempu, ili iendane na mahitaji ya sasa ya kiuchumi na maendeleo ya teknolojia.
Katika hatua ya kupunguza mianya ya rushwa na kuongeza uwazi, tume imependekeza kuondoa utaratibu wa maofisa wa kodi kuonana uso kwa uso na walipa kodi, pamoja na kupunguza matumizi ya fedha taslimu na nyaraka za karatasi.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Deogratius Massawe, amesema iwapo mapendekezo hayo yatatekelezwa kikamilifu, mageuzi yanatarajiwa kuongeza uwiano wa kodi kwa Pato la Taifa hadi asilimia 22 ifikapo mwaka 2050.
Hata hivyo, TPSF imesema makadirio hayo yanahitaji kutambuliwa na kuchunguzwa kwa makini.
“Kwa mujibu wa tume, utekelezaji kamili wa mapendekezo unaweza kuongeza mapato ya Serikali kwa Sh11.02 trilioni ndani ya miaka mitatu, sawa na uwiano wa kodi kwa Pato la Taifa wa asilimia 18.
“Hili linawezekana tu ikiwa mageuzi yatapangwa kwa uangalifu, yatapatiwa rasilimali za kutosha, yataungwa mkono na dhamira endelevu ya kisiasa katika tawala mbalimbali, pamoja na ushiriki hai wa sekta binafsi katika mchakato wa kutunga sera, ikizingatiwa mchango wake wa asilimia 70 kama ilivyoainishwa katika Dira 2050,” amesema Massawe.
Massawe amesema katika maboresho yanayotarajiwa kwenye mtiririko wa fedha na usimamizi wa kifedha wa biashara, ikiwemo marejesho ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwa wakati, na kuwepo kwa taratibu zilizo thabiti, zitasaidia kutatua changamoto za muda mrefu za ukwasi, hasa kwa wauzaji nje na wakandarasi.
“Hii itafanya maboresho katika mifumo ya utatuzi wa migogoro ya kodi kuongeza uhakika na imani, hasa kwa uwekezaji mkubwa na wa muda mrefu,” amesema.
CTI: Imekuja wakati sahihi
Makamu Mwenyekiti wa Shirikisho la Viwanda Tanzania (CTI), Benedict Lema, amesema mapendekezo hayo yatakwenda kuweka mazingira mazuri ya biashara na kuvutia uwekezaji.
Amesema mapitio hayo yamefanyika kwa wakati sahihi, kwani mara ya mwisho ilikuwa miaka 35 iliyopita, wakati kuna mabadiliko mengi yametokea.
“Mfumo wa kodi unatakiwa ubadilike uendane na hali ya sasa. Imekuja wakati sahihi, mapendekezo yake ni mazuri na yanachochea mazingira ya biashara na uwekezaji,” amesema.
Akizungumzia maboresho ya teknolojia yaliyopendekezwa, Lema amesema itasaidia Watanzania wanaofanya biashara kuchangia kulipa kodi kwa wingi, tofauti na zamani walipokuwa wachache.
“Wachache ndiyo walikuwa wanalipa. Tumeupenda, ni mzuri, kwa sababu miaka 35 ni mingi kwa ulimwengu unaobadilika, ni lazima twende na mabadiliko hayo,” amesema.
Amesema walichopenda ni mfumo kuwa na uwezo wa kufanya kazi bila kukutana ana kwa ana na watu, jambo litakalopunguza mianya ya rushwa na kuifanya Tanzania kwenda sambamba na ulimwengu unavyokwenda.
“Ni vyema Rais Samia Suluhu Hassan atekeleze mambo haya akiwa bado katika nafasi hii, ili atakapoondoka aache kitu ambacho Watanzania watamkumbuka,” amesema Lema.
Akizungumzia mapendekezo hayo, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania (JWT), Hamis Livembe, amesema asilimia 90 ya yaliyosemwa na tume mbele ya Rais yalikuwa ni mapendekezo yaliyotolewa na wafanyabiashara na vyama mbalimbali kupitia mikutano waliyofanya na tume hiyo.
“Msingi wa mambo yote haya ni kuhakikisha kodi ziwe rafiki, zitakazoshawishi ulipaji kodi wa hiari na kupunguza upotevu wa mapato. Tunashukuru maoni mengi yaliyozungumzwa, zaidi ya asilimia 90 ni maneno ambayo tulisema sisi. Tunashukuru kwa usikivu wa tume kwa kuyachukua na kuyapeleka mbele ya Serikali ili yatekelezwe.
Ikiwa mambo yote yaliyosemwa yatatekelezwa kama ilivyoainishwa, itasaidia kuboresha biashara na kutanua wigo wa ulipaji kodi, badala ya kutumia wachache waliopo kupata kodi nyingi,” amesema.
Makamu Mwenyekiti wa Machinga Tanzania, Steven Lusinde, amesema kilichosemwa katika tume ni mapendekezo yao yanayolenga kuwafanya watambulike na wapate huduma kirahisi.
“Yatasaidia kuboresha utendaji wetu na itawafanya viongozi kuwa na takwimu sahihi. Tunatamani sana tuingie Tamisemi (Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa) watutambue, kwa sababu huku chini tulipo wanaotushughulikia ni wakuu wa mikoa na wakurugenzi,” amesema.
Amesema kitendo cha wao kuhamishiwa huko kitawasaidia kupata huduma kwa haraka, tofauti na sasa kuwa chini ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, kunawafanya kuzunguka wanapohitaji huduma.
“Wakuu wa mikoa na wakurugenzi ndiyo wenye maeneo tunayofanyia kazi, tukiwa chini yao itakuwa rahisi kwetu kupata huduma,” amesema.
Mtaalamu wa uchumi, Dk Lutengano Mwinuka, amesema kilichopendekezwa kikifanyiwa kazi kitasaidia kusogeza mbele na kutanua wigo wa mapato, ambao utaongeza makusanyo zaidi na kuiwezesha Serikali kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.
Akizungumzia wazo la kubadilisha jina la TRA, amesema limeangalia wajibu mkubwa na litaifanya ifanye kazi kama chombo cha huduma badala ya mamlaka, jambo litakalochochea ufanisi.
“Ni kweli mambo mengi yanabadilika watu, teknolojia, mifumo na mazingira, hivyo ni lazima kubadilika ili kutoa huduma kirahisi. Sasa, kumhudumia mtu si lazima kwenda ofisini, bali awe na uwezo wa kujihudumia popote alipo,” amesema.
Ili matokeo yapatikane, amesema ni lazima kwenda na uhalisia, huku akitazamia ukadiriaji wa kodi ambao bado unaonekana kama una uonevu kwa baadhi ya watu, jambo linaloleta manung’uniko.
“Unaweza kukuta mfanyabiashara mkubwa anakadiriwa kitu ambacho hakifanani na ukubwa wake, huku wale wadogo wakilipa kiwango kikubwa. Maana yake, kunakuwa hakuna usawa. Kama haupo, tuweke mifumo ya ulipaji kodi iendane na uhalisia.
“Pia, mabadiliko ya sheria yaliyopendekezwa, utendaji uakisi kile kilichopendekezwa, na yakianza kufanyiwa kazi yatekelezwe kwa ufanisi ili kusogea mbele, kwani yatakuwa na maana yakitekelezwa badala ya kubaki katika karatasi,” amesema.