Wanafunzi wajikusanyia mamilioni ya ubunifu, ujasiriamali

Dar es Salaam. Katika juhudi za kuchochea ubunifu, utafiti na uthubutu miongoni mwa vijana, sambamba na kuimarisha elimu ya fedha na ujasiriamali wa vitendo katika shule za sekondari, wanafunzi kutoka shule mbalimbali nchini wamezawadiwa fedha taslimu baada ya kuibuka washindi wa mashindano ya kitaifa.

Washindi hao wamepatikana kupitia mashindano ya uandishi wa insha na ubunifu wa mawazo ya biashara“NBC Essay Challenge” na “NBC Business Idea Competition” yaliyoandaliwa na Benki ya NBC kwa kushirikiana na Serikali pamoja na wadau wa maendeleo.

Hafla ya utoaji tuzo imefanyika leo Alhamis, Machi19, 2026 jijini Dar es Salaam huku mgeni rasmi akiwa, Naibu Waziri wa Kazi, Ajira na Mahusiano Kazini, Rahma Kisuo. Ikihudhuriwa na viongozi wa elimu, walimu, wazazi na maofisa wa benki hiyo wakiongozwa na Mkurugenzi wa Uendeshaji (COO), Alelio Lowassa.

Katika kipengele cha Wazo Bora la Biashara, Alyah Ali, mwanafunzi wa kidato cha tano wa Shule ya Sekondari ya Shaaban Robert, ameibuka mshindi wa jumla na kujinyakulia Sh10 milioni pamoja na vitabu vya masomo.

Nafasi ya pili imechukuliwa na Moses Tieng’o wa Sekondari ya Ilboru (Sh3 milioni), huku nafasi ya tatu ikienda kwa Wilfred Sengata wa Sekondari ya Kibaha (Sh2 milioni).

Washindi wengine ni Maryam Khatibu Tahiru (JKU Zanzibar) aliyeshika nafasi ya nne na kujipatia Shmilioni moja, pamoja na Mariam Jackson Athumani wa Sekondari ya Tambaza aliyeshika nafasi ya tano.

Kwa upande wa uandishi wa insha, Medard Elikana wa Sekondari ya Tabora alitangazwa mshindi wa jumla, huku Yasmin Hussein akiongoza upande wa Zanzibar. Washindi wengine waliojipatia fedha na vitabu ni pamoja na Shrifra Mwinuka (Busekelo), Anne Samwel Jacob (St Ann’s Seminary), Herman Asumwisye (Azania), Glorora Mallya (St Ann’s Seminary), Alice Kheri Mwaluko (St Ann’s Seminary) na Jonathael Sarwat (Mzumbe).

Mashindano hayo yalizinduliwa Mei mwaka jana na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, yakilenga kuwafikia zaidi ya wanafunzi milioni moja nchini. Mpango huo ulitekelezwa kwa ushirikiano na wadau mbalimbali, wakiwemo JICA na APE Network.

Akizungumza katika hafla hiyo, Kisuo amesema Serikali itaendelea kuunga mkono jitihada zinazolenga kujenga kizazi chenye uelewa mpana wa masuala ya uchumi.

“Mipango kama hii inachangia kwa kiasi kikubwa kuwaandaa vijana wetu kuwa wabunifu, wenye nidhamu ya fedha na uwezo wa kutumia taasisi za kifedha kwa maendeleo yao binafsi na taifa kwa ujumla,” amesema Kisuo.

Kwa upande wake, Lowassa amesema mashindano hayo yanalenga kuwajengea wanafunzi msingi imara wa ujasiriamali na kuwapa uwezo wa kubuni mawazo yatakayoshindana katika soko la kisasa.

“Tunaahidi kuendelea kuboresha mashindano haya ili kuwafikia wanafunzi wengi zaidi na kuwajengea uwezo utakaowawezesha kushindana katika soko la ajira na biashara,” amesema Lowassa.

Katika hatua nyingine, NBC imewashukuru washirika wake kwa kufanikisha utoaji wa zaidi ya vitabu 2,000 pamoja na zawadi za fedha taslimu kwa washindi.

Mashindano hayo pia yalishuhudia shule mbalimbali zikiingiza wanafunzi katika orodha ya 15 bora, zikiwemo Shaaban Robert, Tambaza, Ilboru, Minaki, Arusha, Umbwe, Benjamini Mkapa, Jangwani, Azania, JKU (Zanzibar) na Kibaha Sekondari.