KAMA unahisi Yanga imeridhika na kikosi chake cha sasa, basi umekosea kwani mabingwa hao wa kihistoria wa Ligi Kuu Bara wameshaanza kupiga hesabu za kumchukua winga mmoja wa DR Congo, huku wakichuana na Waarabu kutoka Algeria kuwania saini ya staa huyo.
Iko hivi; Yanga imejikuta ikipishana mlangoni na MC Alger ya Algeria katika kuulizia saini ya winga huyo anayefahamika kwa jina la Obed Mbala anayecheza AS Maniema Union.
Winga huyo anawachanganya mabosi wa klabu hizo, ukiachilia mbali umri wake mdogo wa miaka 21, lakini uwezo wa kucheza kama mshambuliaji ndiyo unaozivutia klabu mbalimbali, jambo ambalo Yanga na MC Alger zimeona ziwahi sokoni mapema.
Taarifa za ndani zililiambia Mwanaspoti kuwa, Yanga inazungumza na MC Alger kumwania winga Obed Mbala wa Union Maniema. “Yanga ina mahusiano mazuri na AS Maniema, kwa hiyo lolote linaweza kutoka kwani haitakuwa biashara ya kwanza kwa timu hizo kufanya,” kimesema chanzo hicho.
Mwanaspoti lilimtafuta mtu wa karibu na winga huyo ambapo alisema, mchezaji mwenyewe anatamani kuichezea Yanga kwa sababu ni timu ambayo anaifahamu vizuri.
“Mbala anataka kuja Yanga ingawa Alger ndio wameweka ofa kubwa zaidi, ila mabosi zake ndio wataamua wampeleke wapi kati ya timu hizo,” alisema mtu huyo.
Ikumbukwe kuwa, winga huyo jina lake lilijadiliwa sana ndani ya Yanga kipindi cha usajili wa dirisha dogo msimu huu kabla ya hesabu kubadilishwa na kwenda kusajiliwa Buba Jammeh.
Mbala bado ana mkataba wa mwaka mmoja na nusu wa kuitumikia AS Maniema Union, huku akiwa na rekodi ya kuhusika na mabao manne katika Kombe la Shirikisho Afrika msimu huu akifunga moja na asisti tatu.
Hii haitakuwa mara ya kwanza kwa Maniema kuuza mchezaji kwenda Yanga, kwani mara ya mwisho ilimuuza Maxi Nzengeli. Mbali na Maxi, Maniema pia imewauzia Azam nyota wawili, Jephte Kitambala aliyeingia dirisha kubwa na Jean-Jacques Ngita akitua dirisha dogo.
Katika kikosi cha Yanga, tayari kuna idadi ya wachezaji 12 wa kimataifa wanaotakiwa kikanuni, hivyo kuna uwezekano wa kupunguzwa mtu ili aingie nyota huyo kutokana na wapo wanaomaliza mikataba akiwamo Frank Assinki anayecheza hapo kwa mkopo hadi mwisho wa msimu huu. Kwa nafasi anayocheza Mbala, pale Yanga kuna nyota kadhaa wa kimataifa ambao ni Maxi, Buba, Allan Okello.
Wakati ikipiga hesabu za kuimarisha kikosi chake, Yanga imevutwa shati na TRA United katika mechi ya Ligi Kuu Bara iliyochezwa jana Jumatano kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha ambapo timu hizo zimeshindwa kufungana.
Katika mechi hiyo, Yanga iliwakosa wachezaji sita wanaouguza majeraha ambao ni Clement Mzize, Dickson Job, Ibrahim Abdullah ‘Bacca’, Laurindo Aurelio ‘Depu’, Chadrack Boka na Edmund John.
Licha ya kukosekana kwa nyota hao, Yanga imetoka uwanjani bila ya kuruhusu bao ilipocheza kwa mara ya kwanza mechi ya ligi bila ya uwepo wa walinzi wake wawili wa kati wanaounda kikosi cha kwanza, Dickson Job na Ibrahim Abdullah ‘Bacca’, huku waliochukua nafasi zao, Bakari Mwamnyeto na Frank Assinki wakilinda vizuri lango la kipa Djigui Diarra aliyefikisha clean sheet tisa.
Hata hivyo, shida imebaki katika ushambuliaji ambapo jana Yanga imemkosa Laurindo Aurelio ‘Depu’ anayeuguza majeraha, huku pia mapema tu dakika 21, ikampoteza Prince Dube aliyetolewa baada ya kuumia. Emmanuel Mwanengo akachukua jukumu la kuongoza safu ya ushambuliaji.
Huenda baada ya mechi hiyo ya jana Yanga ikaongeza majeruhi kwani mbali na Dube aliyetolewa dakika ya 21 kwa kuumia, pia beki wa kulia, Israel Mwenda naye hakuendelea kipindi cha pili kutokana na kile cha kwanza kuumia, nafasi yake akachukua Yao Kouassi Attohoula.
Suluhu hiyo imeifanya Yanga kufikisha pointi 37 ikiendelea kukaa kileleni kwa tofauti ya pointi tisa dhidi ya Azam na JKT Tanzania zinazoshika nafasi ya pili na tatu zikiwa na pointi 28, huku Simba ni ya nne na pointi 27.
Yanga imecheza mechi 15 ikikamilisha duru la kwanza, Azam imeshuka dimbani mara 14 na leo Alhamisi itakuwa Kigoma kukabiliana na Mashujaa ikienda kuhitimisha duru la kwanza, wakati Simba ina mechi 12, leo ni ya 13 dhidi ya Pamba Jiji, hivyo ikipiga vizuri hesabu zake katika mechi hizo tatu ili kuwa sawa na Yanga, itakuwa nyuma ya watani zao hao wa jadi kwa tofauti ya pointi moja. Wakati Yanga jana ikivutwa shati, TRA United ilimaliza ikiwa pungufu ya mchezaji mmoja baada ya kiungo wake, Mzamiru Yassin kuonyeshwa kadi ya pili ya njani iliyoambatana na nyekundu dakika ya 77..