Aliyemuua baba yake ahukumiwa kunyongwa hadi kufa

Arusha. Mahakama Kuu, Masijala Ndogo ya Bukoba, imemhukumu adhabu ya kunyongwa hadi kufa Victor Alex baada ya kumkuta na hatia ya kumuua baba yake mzazi, Alex Marcel, kwa kumkata kwa panga.

Mauaji hayo yalitokea Aprili 29, 2024 katika Kitongoji cha Rwamashanga, Kijiji cha Ruzinga, wilayani Karagwe, mkoani Kagera.

Hukumu hiyo ilitolewa Machi 18, 2026 na Jaji Lilian Itemba aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo ya jinai namba 8150/2025, na nakala yake kuwekwa kwenye tovuti ya mahakama.

Jaji Itemba amesema baada ya kuchambua kwa makini ushahidi wote uliowasilishwa mahakamani, hoja kuu inayopaswa kuamuliwa ni kama upande wa mashtaka umeweza kuthibitisha hatia ya mshtakiwa bila kuacha shaka yoyote ya msingi, hususan kwa kuzingatia kwamba hakuna shahidi aliyeshuhudia tukio la mauaji.

Amesema katika kesi hiyo ushahidi uliotolewa ni wa kimazingira na kwamba kutokana na ushahidi uliopo, imebainika bila ubishi kuwa mshtakiwa alihusika katika ugomvi mkali na baba yake (marehemu kwa sasa) siku ya tukio, ambapo alionekana pia akitoa vitisho huku akinoa panga.

Ilidaiwa kuwa kabla Alex hajafariki, alimtaja mshtakiwa kuwa ndiye aliyemshambulia.

Zaidi ya hayo, mlolongo wa matukio unaonesha ukaribu wa muda kati ya ugomvi huo na kifo cha marehemu, pamoja na kupatikana kwa panga iliyodaiwa kufichwa kwa maelekezo ya mshtakiwa, na fulana yenye madoa ya damu kutoka chumbani kwake. Mshtakiwa alishindwa kutoa maelezo ya kuridhisha kuhusu mazingira hayo yote.

“Hali hizi, zinapochukuliwa kwa pamoja, zinaunda mnyororo thabiti na usiovunjika unaoelekeza kwa mshtakiwa na haziendani na dhana yoyote inayofaa ya kutokuwa na hatia.”

Jaji amesema utetezi wa mshtakiwa kwamba alikuwa anaenda kuuza mbuzi hauwezi kueleza wala kuvunja ushahidi wa kimazingira uliowasilishwa dhidi yake, hususan ugomvi, vitisho na mazingira ya kifo cha marehemu. Ameongeza kuwa aina ya majeraha yaliyosababisha kifo, kukatwa sehemu muhimu kama shingo na kichwa, inaonesha wazi kuwepo kwa nia ovu.

“Upande wa mashtaka umefanikiwa kuthibitisha bila shaka yoyote kwamba mshtakiwa ndiye aliyesababisha kifo cha marehemu kwa makusudi. Hivyo basi, Mahakama inampata mshtakiwa na hatia ya kosa la mauaji kama alivyoshtakiwa,” amesema Jaji Itemba.

Mahakama ilihitimisha kwa kumhukumu adhabu ya kunyongwa hadi kufa kwa mujibu wa kifungu cha 197 cha Kanuni ya Adhabu.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, Victor Alex alidaiwa kumuua baba yake kwa kumkata kwa panga katika maeneo ya shingo na kichwa, majeraha yaliyosababisha kupoteza damu nyingi na hatimaye kifo chake.

Shahidi wa saba alidai kuwa siku ya tukio alikwenda nyumbani kwa Alex kuchukua ndizi, na alipofika alikuta mshtakiwa akibishana na baba yake, ambapo baba huyo alimtaka mshtakiwa asirudi nyumbani.

Alidai mgogoro ulisababishwa na mshtakiwa kudai kuwa alikuwa akizalisha ndizi za kutengeneza pombe lakini baba yake hakuwa akimpa chochote, ugomvi uliofikia hatua ya kutishiana.

Alidai aliondoka eneo hilo na kwamba baadaye siku hiyo hiyo alirudi na kumkuta Alex akiwa na jicho lililovimba na damu mdomoni akidai kushambuliwa na mshtakiwa, na kumwomba atoe taarifa kwa mwenyekiti.

Alidai kuwa wakati akielezwa hayo, mshtakiwa alikuwa akinoa panga lake akionya kwamba angemshambulia mtu yeyote atakayemripoti.

Shahidi huyo alidai kuwa aliwaacha mshtakiwa na baba yake, ambapo baadaye alipoenda tena usiku alimkuta Alex amefariki.

Ripoti ya uchunguzi wa mwili wa marehemu iliyowasilishwa mahakamani ilithibitisha kuwa chanzo cha kifo kilikuwa kupoteza damu nyingi kutokana na majeraha ya kukatwa sehemu muhimu za mwili, ikiwemo shingo na kichwa.

Shahidi aliyeufanyia mwili huo uchunguzi alieleza kuwa majeraha hayo hayawezi kusababishwa na ajali au sababu za kawaida, bali ni matokeo ya shambulio la kutumia kitu chenye ncha kali.

Katika utetezi wake, mshtakiwa alidai kwamba Aprili 29, 2024 aliamka saa moja asubuhi, akaenda kumsalimia baba yake kisha akaenda shambani kwake bondeni anapolima nyanya na viazi. Alidai nyanya zake zilikuwa zimeathiriwa na baridi kali na kwamba hakuwa na dawa ya kuua wadudu.

Alidai alirudi jioni na kulala, na Aprili 30, 2024 asubuhi alichukua mbuzi kwenda kumuuza katika soko la Kayanga kwani alihitaji pesa za kununulia dawa za kuulia wadudu. Akiwa katika kijiji cha Nyabwigira alisimamishwa na walinzi wa doria waliomtuhumu kwa kuiba mbuzi huyo.

Alidai baadaye polisi walifika, wakamfunga pingu na kumpeleka Kituo cha Polisi cha Kayanga ambapo alibaki kizuizini. Alikana kuongoza polisi kwenda kuonyesha panga lolote, na kudai kuwa alipopelekwa kwenye shamba la mananasi nyumbani kwa Mzee Apollo, shahidi wa saba alijitokeza na panga na kumkabidhi Inspekta Nyanda.

Aidha, alikana kwamba fulana ya njano na panga iliyotolewa mahakamani ilikuwa yake, na kudai kuwa alilazimishwa kusaini hati katika kituo cha polisi bila maelezo. Alisema pia hakuna sampuli ya damu iliyochukuliwa kutoka kwake.