Ambokile atuliza presha Mbeya City

MSHAMBULIAJI wa Mbeya City, Eliud Ambokile amesema licha ya mwenendo usioridhisha wa kikosi hicho msimu huu katika Ligi Kuu Bara, lakini bado wana nafasi ya kubadilisha upepo mbaya unaowaandama, kutokana na ubora wa wachezaji waliopo kikosini.

Akizungumza na Mwanaspoti, Ambokile, alisema bado wana wachezaji wazuri wanaoweza pia kubadilisha hali iliyopo, licha ya ushindani mkali uliopo katika kila mechi kutokana na mahitaji ya kila timu msimu huu.

“Hakuna anayefurahia mwenendo tuliokuwa nao kwa sasa, sisi kama wachezaji hatujakata tamaa kwa sababu nafasi tuliyopo na gepu la pointi na waliokuwa juu yetu tunaweza kulifikia na kuwapita, jambo muhimu ni kupambana zaidi,” alisema Ambokile.

Kauli ya nyota huyo inajiri baada ya mwenendo usioridhisha wa timu hiyo ambapo hadi sasa imeshinda mechi tatu, sare nne na kupoteza tisa kati ya 16 za Ligi Kuu Bara ilizocheza msimu huu, huku ikifunga mabao 13 na kuruhusu 22, ikishika nafasi ya 14 katika msimamo ikikusanya pointi 13.

Ambokile aliyeichezea Mbeya City tangu mwaka 2017, pia amewahi kupita Black Leopards FC ya Afrika Kusini, TP Mazembe ya DR Congo na Nkana FC ya Zambia, huku akikirejesha tena kikosi hicho Ligi Kuu Bara, baada ya kushuka msimu wa 2022-2023.

Katika msimu uliopita wa 2024-2025, Ambokile aliiwezesha Mbeya City kurejea Ligi Kuu ikitokea Ligi ya Championship, baada kikosi hicho kumaliza nafasi ya pili na pointi 68, nyuma ya Mtibwa Sugar, iliyoibuka mabingwa kwa kukusanya pointi 71.

Msimu wa 2024-2025, nyota huyo aliifungia Mbeya City mabao 12, kati ya 68, japo msimu huu wa 2025-2026, amefunga mabao mawili ya Ligi Kuu, huku la mwisho alifunga katika sare ya timu hiyo ya bao 1-1 dhidi ya Dodoma Jiji, Februari 3, 2026.