Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Kanda ya Serengeti kimetuma salamu za pongezi kwa waumini wa Dini ya Kiislamu nchini kufuatia kumalizika kwa mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, kikieleza kuwa kipindi hicho ni msingi muhimu wa kujenga jamii bora.
Leo Ijumaa Machi 20, 2026, baadhi ya waumini wa madhehebu ya dini ya Kiislamu wameadhimisha siku ya Eid, huku wengi wakijiandaa kusherehekea siku hiyo kesho Jumamosi Machi 21, 2026.
Katika taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa leo, chama hicho kimesema mafanikio ya Waislam katika kutekeleza ibada ya funga yanaashiria nidhamu, uvumilivu na kujitafakari, mambo ambayo ni nguzo ya haki na maendeleo katika jamii.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa mafundisho ya Ramadhani yanaendelea kuwa chachu ya kukuza upendo, umoja na kuwajali wengine, maadili yanayohitajika katika kuijenga Tanzania yenye mshikamano na maendeleo endelevu.
Aidha, Chadema Kanda ya Serengeti imesisitiza kuthamini mchango wa dini ya Kiislamu pamoja na taasisi zake katika kulinda utu wa binadamu na kuhimiza uwajibikaji, ikibainisha kuwa nafasi ya dini katika kujenga jamii bora haiwezi kupuuzwa.
“Katika nyakati ambazo taifa linahitaji mshikamano na uongozi unaozingatia haki kwa wote, nafasi ya taasisi za dini inabaki kuwa muhimu zaidi,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.
Chama hicho pia kimeahidi kuendelea kudumisha ushirikiano mzuri na viongozi wa dini ya Kiislamu pamoja na taasisi nyingine za kidini kwa lengo la kujenga jamii yenye amani, haki na maendeleo kwa wote.
Katika hatua nyingine, chama hicho kimewaomba Mashehe wa mikoa ya Shinyanga, Simiyu na Mara kufikisha salamu za Eid kwa Waislam wote katika maeneo hayo.
Taarifa hiyo imehitimishwa kwa kuwatakia Waislam wote Eid njema yenye amani, furaha na baraka tele.