Dereva mbaroni kwa kusafirisha wahamiaji haramu

Njombe. Jeshi la polisi mkoa wa Njombe linamshikilia Sipha Credo Mgonde (47) ambaye ni dereva na mkazi wa Mbagala  jijini Dar es salaam kwa tuhuma za kusafirisha wahamiaji haramu ambao wanatajwa kuwa ni raia wa kigeni kutoka huko nchini Ethiopia.

Dereva huyo amekamatwa katika Kijiji cha Mtewele kilichopo Halmashauri ya Wilaya ya Wanging’ombe huko mkoani Njombe akiwasafirisha raia hao kutoka Dar es Salaam kwenda huko Tunduma mkoani Songwe.

Hayo yamesemwa leo Machi 20, 2026 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe Mahamoud Banga wakati akizungumza na waandishi wa habari mkoani hapa.

Amesema mtuhumiwa huyo amekamatwa akiwa na gari ndogo yenye namba za usajili IT 4443 aina ya Sienta nyeupe kwenye barabara kuu ya Wanging’ombe kuelekea mkoani Mbeya.

Amewataja watuhumiwa wengine ambao ni raia wa kigeni kuwa ni Yansar Manere Erkao (28), Amanuel Degele Eremo (28) na Abraman Linnah (28) wote hao wamekamatwa na wapo kituo cha polisi Ilembula kilichopo huko wilayani Wanging’ombe mkoani Njombe wakisubiri taratibu za kisheria ili kukabidhiwa katika idara ya uhamiaji.

“Katika kijiji cha Mtewele Wilaya ya Wanging’ombe Jeshi la Polisi limefanikiwa kumkamata Sifa Credo dereva na mkazi wa Mbagala akiwa anasafirisha raia wa kigeni ambao ni Waethiopia kutoka Dar es Salaam kwenda Tunduma,” amesema Banga.

Amesema jeshi hilo pia limefanikiwa kuwafikisha mahakamani watuhumiwa watatu na mahakama kuu imeweza kuwatia hatiani kwa makosa mbalimbali yakiwemo ya mauaji.

Amesema Mahakama Kuu Kanda ya Iringa ilimuhukumu Mussa Msolla kunyongwa hadi kufa kwa kosa la mauaji huku mahakama hiyo pia iliwahukumu Ally Jumanne Mtinangi na Shabani Selemani pia kwa kosa la mauaji yaliyofanyika kwa nyakati tofauti.

Kamanda wa polisi mkoa wa Njombe Mahamoud Banga akizungumza na waandishi wa habari mkoani hapa.

Ametoa wito kwa wananchi wa mkoa wa Njombe kuacha kujichukulia sheria mkononi na badala yake wafanye kazi na kujipatia kipato ambacho ni halali kinyume cha hapo jeshi hilo halitosita kuchukua hatua endapo matukio ya kihalifu yatajitokeza.