Fidia Sh2.9 bilioni yafungua njia mradi wa maji Mbeya

Mbeya. Serikali imeanza mpango wa kumaliza kero ya maji mkoani Mbeya baada ya kutoa zaidi ya Sh2.9 bilioni kulipa fidia kwa wananchi wanaopisha mradi wa kimkakati wa maji kutoka Mto Kiwira wilayani Rungwe.

Fidia hiyo inahusisha wananchi 819 waliokuwa na mashamba na makazi katika vijiji 10 vinavyopitiwa na mradi huo, pamoja na makaburi 79 yaliyohamishwa kupisha utekelezaji wake.

Mradi huo unaotekelezwa na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Mbeya chini ya mkandarasi China Railway Construction Engineering Group, unagharimu Sh119 bilioni na unatarajiwa kuwa suluhisho la muda mrefu la upatikanaji wa maji katika Mkoa wa Mbeya na maeneo jirani.

Akizungumza Machi 19, 2026 wakati wa ziara ya waandishi wa habari, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa mamlaka hiyo, Barnabas Konga amesema mradi huo umefikia asilimia 49 ya utekelezaji, huku hatua inayofuata ikiwa ni ulazaji wa mabomba kwa umbali wa kilometa 37.24 kutoka Mto Kiwira hadi eneo la New Forest.

“Kimsingi Serikali tayari imetoa Sh2.9 bilioni kwa ajili ya fidia. Hatua hii inafungua njia ya kuanza ulazaji wa mabomba makubwa ya kusafirisha maji,” amesema Konga.

Amefafanua kuwa Julai 9, 2024, mamlaka hiyo iliingia mkataba na kampuni ya uthaminishaji ya Romatun Limited kwa ajili ya kuthaminisha mali za wananchi, hatua iliyowezesha ulipaji wa fidia kwa haki.

Ujenzi wa tenki lenye uwezo wa kuhifadhi lita  milioni tano linajengwa katika eneo la New Forest Mkoa wa Mbeya kupitia mradi wa  kimkakati  kutoka chanzo cha mto Kiwira Wilaya ya Rungwe wenye thamani ya zaidi ya Sh 119 bilioni. Picha na Hawa Mathias

Kwa upande wa ujenzi wa tenki la New Forest, lenye uwezo wa kuhifadhi lita milioni tano za maji kwa siku, Konga alisema kazi zinazoendelea ni pamoja na usukaji wa nondo na maandalizi ya kumimina zege la juu, kazi itakayofanyika kwa siku tatu mfululizo.

Mbali na mradi huo, Konga amesema juhudi nyingine zinaendelea kukabiliana na changamoto ya maji, ikiwa ni pamoja na uchimbaji wa visima vitano katika kata za Itezi, Nsalala na Ruanda, pamoja na maboresho ya pampu za kusukuma maji.

Amebainisha kuwa uwekezaji mkubwa wa miundombinu ya maji, ukiwemo mradi wa = Bwawa la Mwalimu Nyerere, umechangia kupunguza tatizo la kukatika kwa maji mara kwa mara.

Naye mkandarasi wa mradi huo, Joseph Darabe, amesema kazi ya umwagaji zege itafanyika kwa kutumia mitambo ya kisasa ili kuhakikisha ubora na kasi ya ujenzi.

Amesema hadi sasa Serikali imeshatoa Sh31.4 bilioni kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo, kati ya hizo Sh14.9 bilioni ni malipo ya awali na Sh16.4 bilioni zimelipwa kwa mkandarasi.

Kwa mujibu wa mpango, mradi huo unatarajiwa kukamilika Desemba 3, 2026, hatua itakayowezesha wananchi kuanza kunufaika na huduma ya maji safi na salama.

Mkazi wa Swaya, Sekela Mwakyusa amesema upatikanaji wa maji utasaidia kuondoa mzigo mkubwa kwa wanawake na kutoa nafasi ya kushiriki zaidi katika shughuli za kiuchumi.

“Tunashukuru Serikali kwa kulipa fidia na kuharakisha mradi. Wanawake tumekuwa tukitumia muda mwingi kutafuta maji, sasa tutapata nafasi ya kufanya shughuli nyingine za maendeleo,” amesema.