Global Publishers
March 20, 2026
0 Comments
Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu la Iran (Islamic Revolutionary Guard Corps) limethibitisha kifo cha msemaji wake, Brigedia Jenerali Ali Mohammad Naini, kufuatia shambulizi lililoripotiwa kufanyika alfajiri ya leo na kuhusisha vikosi vya Marekani kwa ushirikiano na Israel.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na IRGC leo Ijumaa, Machi 20, 2026, Naini (68) aliuawa katika tukio hilo ambalo limeelezwa kuwa ni sehemu ya mashambulizi yanayoendelea katika eneo la Mashariki ya Kati, hali inayozidi kuongeza wasiwasi wa usalama na mvutano wa kijeshi.
Kifo chake kinakuja muda mfupi baada ya kuonekana kwenye televisheni ya taifa ya Iran akitoa kauli kali akisisitiza kuwa nchi yake bado ina uwezo mkubwa wa kuzalisha makombora, hata katika mazingira ya vita. Kauli hiyo iliripotiwa na Shirika la Habari la Fars, ambapo Naini alinukuliwa akisema uzalishaji wa silaha hizo unaendelea bila kukwama.
Tukio hili linaongeza idadi ya maafisa waandamizi wa kijeshi waliopoteza maisha tangu kuanza kwa mzozo unaoendelea, ambao umeanza kusambaa na kuathiri kwa kiasi kikubwa usalama wa kikanda.