Global Publishers
March 20, 2026
0 Comments
Kuelekea maadhimisho ya sikukuu ya Eid El-Fitri, Jeshi la Polisi nchini limetangaza kuwa limejipanga kikamilifu kuhakikisha usalama wa wananchi unadumishwa katika kipindi chote cha sikukuu hiyo.
Akizungumza na vyombo vya habari, Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime, amesema kuwa hali ya usalama nchini iko shwari na hakuna dalili za tishio lolote kubwa linaloweza kuvuruga amani wakati wa sherehe za Eid El-Fitri.
Amefafanua kuwa Jeshi la Polisi limeongeza ulinzi katika maeneo mbalimbali ikiwemo misikiti, viwanja vya wazi, maeneo ya starehe, pamoja na sehemu ambazo wananchi hukusanyika kusherehekea pamoja na familia, ndugu na marafiki. Aidha, doria na operesheni maalum zimeimarishwa kuhakikisha kila eneo linakuwa salama.
Katika taarifa hiyo, Misime amewataka wazazi na walezi kuwa makini zaidi kwa kuwalinda watoto wao na kuhakikisha hawawaachi bila uangalizi, hasa katika maeneo yenye mikusanyiko mikubwa ya watu. Amesema hatua hiyo ni muhimu ili kuepusha changamoto zinazoweza kujitokeza wakati wa shamrashamra za sikukuu.
Vilevile, ametoa wito kwa wananchi wanaosafiri kwenda kusherehekea katika maeneo mbalimbali kuhakikisha wanaacha ulinzi wa kutosha majumbani mwao ili kuzuia matukio ya wizi na madhara mengine yanayoweza kutokea wakati nyumba zikiwa hazikaliwi.
Jeshi la Polisi limehimiza pia ushirikiano wa karibu kati ya wananchi na vyombo vya ulinzi na usalama kwa kutoa taarifa za haraka za viashiria vya uhalifu au vitendo vyovyote vinavyoweza kuhatarisha amani.
Kwa ujumla, Polisi wamesisitiza kuwa wataendelea kuwepo katika maeneo mbalimbali nchini ili kuhakikisha wananchi wanasherehekea Eid El-Fitri katika mazingira ya amani, usalama na utulivu.
