Jeshi la Polisi lawashikilia wawili kwa mauaji ya Nyanza

Dar es Salaam. Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam linawashikilia watuhumiwa wawili wanaohusishwa na mauaji ya Athumani Nyanza, ambaye mwili wake ulipatikana ukiwa umefukiwa kwenye shimo karibu na nyumba yake Mtaa wa Kimya Kimya, Kata ya Zingiziwa, Chanika.

Taarifa za awali zinaeleza kuwa marehemu Nyanza anadaiwa kuuawa na mpenzi wake, kabla ya mwili wake kuondolewa na kufukiwa katika eneo hilo ili kuficha tukio hilo.

Mashuhuda wa eneo hilo wamedai kuwa kinyume na matarajio, mauaji hayo hayakutokea nyumbani kwa marehemu, bali alichukuliwa na kupelekwa eneo jingine kabla ya kuuawa, hali iliyoongeza sintofahamu kwa wakazi wa Chanika.

Akizungumza na waandishi wa habari Machi 20, 2026, Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro amesema watuhumiwa hao wamekamatwa Machi 18, 2026, mkoani Morogoro.

Amesema uchunguzi uliofanywa kwa kushirikiana na wananchi umewezesha kukamatwa kwa mtuhumiwa mmoja anayefahamika kwa jina la Rahema Maulidi (42), mkazi wa Kigamboni, pamoja na mwenzake mmoja ambaye jina lake limehifadhiwa kutokana na uchunguzi unaoendelea.

“Watuhumiwa hawa wanashikiliwa na wanaendelea kuhojiwa kwa kina kuhusiana na tukio hilo, huku taratibu za kisheria zikiendelea ili waweze kufikishwa mahakamani,” ilieleza taarifa hiyo.

Jeshi hilo limepongeza ushirikiano wa wananchi uliosaidia kufanikisha kukamatwa kwa watuhumiwa hao, likisisitiza kuwa utaendelea kuwa muhimu katika mapambano dhidi ya uhalifu.

Aidha, Polisi imewahimiza wananchi kuendelea kutoa taarifa sahihi na kwa wakati ili kusaidia kudhibiti vitendo vya uhalifu na kuimarisha usalama katika maeneo yao.

Akizungumza na Mwananchi, Machi 20, 2026  rafiki wa marehemu, Madebe Lidai amesema bado hawajakabidhiwa mwili na endapo wakifanikiwa kukabidhiwa leo wanatarajia kuzika Machi 21, 2026.

Kutoka kukabidhiwa mwili huo ni kutokana na kusubiri uchunguzi wa vinasaba (DNA), ambavyo walielezwa majibu yake yanatoka kati ya saa 24 hadi 48.

“Bado hatujakabidhiwa mwili na tulitegemea leo lakini  tutapewa hivyo tunaweza kutoa taarifa kamili ya mazishi”