JKU imetamba mafanikio yanayopatikana ni kutokana na nidhamu iliyopo baina ya wachezaji na viongozi na wanachofanya hivi sasa ni kuhakikisha wanarudisha ubingwa wa Ligi Kuu Zanzibar.
Akizungumza na Mwanaspoti, Kocha Mkuu wa timu hiyo, Ali Bakari alisema mbinu inazozitumia timu kutafuta matokeo ndizo zilizowafikisha hapo na wala hawana mpango wa kurudi nyuma zaidi ya kuwania ubingwa wa Ligi Kuu Zanzibar.
“Nidhamu siyo lazima mchezaji amuamkie mwalimu shikamoo bali ni namna wanavyoheshimu wanachoambiwa na makocha wao kabla wakati na baada ya mechi,” alisema.
Alisema timu hiyo imerudi kwenye ushindani wa kuwania ubingwa wa Ligi Kuu Zanzibar ZPL msimu wa 2025-2026 ili kulirejesha taji hilo nyumbani.
Kocha huyo alisema mipango ya timu hiyo ni kuhakikisha inajipanga kwa kufanya maandalizi yenye tija.
Alisema kadiri timu inavyojiandaa kwa kutumia muda mwingi kufanya mazoezi ndivyo inavyoongeza nafasi ya kushinda mechi zake, hivyo JKU tayari imeshaanza kujiandaa na mechi 10 za mwisho wa msimu na haitarajii kuharibu kwani hizo ndiyo kipimo bora cha mbio za ubingwa.
Alisema mechi 10 ndizo zitaamua anayestahili kuchukua ubingwa msimu huu kushuka kwa timu na kubaki kwa msimu ujao.
JKU baada ya kucheza mechi 20 imekusanya pointi 36 ikishika nafasi ya tano ikitofautiana kwa pointi mbili pekee na kinara Fufuni yenye 38.
Timu hiyo ilitwaa ubingwa wa ZPL msimu wa 2023-2024 kabla ya msimu wa 2024-2025 kuvuliwa ubingwa huo na Mlandege.