Dar es Salaam. Kifo cha Jaji mstaafu Julie Manning kimetamatisha safari ya maisha ya mwanamke huyo aliyeacha alama ya kipekee katika tasnia ya sheria nchini na ukanda wa Afrika Mashariki, akitambulika kama miongoni mwa waanzilishi wa mafanikio ya wanawake katika taaluma hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa ya Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Jaji Manning amefariki dunia leo Ijumaa, Machi 20, 2026 katika Kituo cha Afya cha Hitech Sai, Upanga jijini Dar es Salaam, alipokuwa akipatiwa matibabu.
Msiba wake uko nyumbani kwake eneo la Oysterbay, jijini Dar es Salaam huku mipango ya mazishi ikiendelea kuratibiwa.
Safari na rekodi za kihistoria
Historia ya Jaji Manning inaonyesha mwanzo wa safari iliyojengwa juu ya uthubutu na ubora wake kitaaluma.
Alionyesha mapema uwezo mkubwa uliomwezesha kusoma katika Shule ya Wasichana Tabora, kabla ya kuandika historia mwaka 1961 alipochaguliwa kujiunga na Kitivo cha Sheria cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ambacho kilikuwa cha kwanza Afrika Mashariki kwa wakati huo.
Akiwa mwanamke pekee miongoni mwa wanafunzi 13 wa mwanzo wa kitivo hicho, alifanikiwa kuweka rekodi ya kuwa mwanamke wa kwanza kutoka Tanganyika na Afrika Mashariki kusomea sheria katika kiwango hicho. Mafanikio hayo yaliweka msingi wa mabadiliko makubwa katika mtazamo wa nafasi ya wanawake kwenye taaluma ya sheria.
Alipohitimu mwaka 1963, aliweka rekodi nyingine kwa kuwa mwanamke wa kwanza Mtanzania kupata shahada ya sheria.
Baada ya kuhitimu, aliajiriwa katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kama mwandishi wa sheria, na kuwa mwanamke wa kwanza kushika nafasi hiyo nchini.
Mwaka 1973, historia kubwa zaidi iliandikwa alipoteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama Kuu na aliyekuwa Rais wa wakati huo, Mwalimu Julius Nyerere. Uteuzi huo ulimfanya kuwa mwanamke wa kwanza nchini Tanzania na Afrika Mashariki kufikia wadhifa huo, hatua iliyovunja vizingiti vya kijinsia katika mfumo wa mahakama.
Mwaka 1975, aliteuliwa kuwa mbunge na baadaye waziri wa sheria, akawa miongoni mwa wanawake wa kwanza kushika nafasi ya uwaziri kamili nchini. Katika kipindi chake cha uongozi hadi mwaka 1983, alisimamia kwa karibu misingi ya haki na utawala wa sheria, akichangia kwa kiasi kikubwa katika ujenzi wa taasisi za kisheria.
Urithi wa utumishi uliotukuka
Mbali na nyadhifa hizo, Jaji Manning aliendelea kulitumikia taifa katika nafasi mbalimbali ikiwemo kuwa Kamishna wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi na mjumbe wa Tume ya Kurekebisha Sheria. Kupitia majukwaa hayo, aliendelea kutoa mchango mkubwa katika kuimarisha mifumo ya kisheria na demokrasia nchini.
Kutokana na mchango wake huo, mwaka 2011 alitunukiwa medali na Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete, ikiwa ni kutambua utumishi wake uliotukuka kwa taifa.
Wadau wa sekta ya sheria wanasema Jaji Manning ataendelea kukumbukwa kama kinara aliyefungua milango kwa wanawake katika taaluma ya sheria na uongozi wa umma. Wanasisitiza kuwa, licha ya kifo chake kuacha pengo kubwa, mchango wake utaendelea kuwa sehemu ya historia ya taifa.
Mwanasheria mkongwe na aliyewahi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Andrew Chenge amesema marehemu Manning atakumbukwa kwa kuwa mwanamke wa kwanza Mtanzania kupata shahada ya sheria na miongoni mwa waanzilishi wa taaluma hiyo nchini.
Amesema Manning alikuwa mwandishi mahiri wa sheria na alitoa mchango mkubwa katika kuandaa misingi ya sheria nyingi zilizotumika nchini.
Aidha, amewataja baadhi ya wanasheria waliomfuata katika taaluma hiyo, akiwemo marehemu Deo Makanza na George Liundi.
“Kwa ujumla, Julie Manning atakumbukwa kwa mchango wake mkubwa katika tasnia ya sheria na katika kupigania haki za wanawake na usawa wa kijinsia nchini,” amesema Chenge.
Kwa upande wake, Wakili Peter Madeleka amesema kumbukumbu ya Manning itaendelea kuishi kama mfano wa mwanamke aliyefungua njia kwa wengine kujiamini na kuingia katika taaluma ya sheria.
Amesema ujasiri wake katika kutafsiri na kusimamia sheria kwa haki ulimfanya kuwa kioo cha kuangaliwa na vizazi vijavyo, huku akibainisha kuwa hakuwa na woga katika kusimamia haki kwa mujibu wa sheria.
Wanaharakati wa haki za binadamu pia wamemtaja Manning kama kiongozi aliyesimama imara katika kutetea haki za makundi yote bila ubaguzi.
Dk Ananilea Nkya amesema marehemu alikuwa na uzalendo wa dhati na uwezo mkubwa wa kufikiri na kuchambua masuala ya haki.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, Dk Anna Henga amesema kifo cha Manning kimeacha pengo kubwa, akimtaja kuwa jaji aliyesaidia kuondoa mitazamo ya kijinsia katika taaluma ya sheria.
Amesema kupitia maamuzi na maandishi yake ya kisheria, Manning alionyesha umahiri mkubwa uliowahamasisha wanawake wengi kuamini kuwa wanaweza kushika nafasi za juu katika mfumo wa mahakama.
Kwa ujumla, maisha ya Julie Manning yanabaki kuwa somo na chachu ya mabadiliko, yakionyesha namna uthubutu, elimu na uzalendo vinavyoweza kubadili historia na kufungua milango kwa wengine katika jamii.
