MSHAMBULIAJI Mtanzania, Cyprian Kachwele amejiunga na Halifax Wanderers FC ya Ligi Kuu Canada kwa mkataba wa mkopo wa mwaka mmoja akitokea Whitecaps FC 2.
Mkataba huo unatamatika Desemba 31 mwaka huu na inaelezwa Kachwele amesajiliwa ili kukiongeza nguvu kikosi cha Wanderers.
Inaelezwa sababu ya nyota huyo kutolewa kwa mkopo ni kumpa muda zaidi wa kupata nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza na kuonyesha uwezo wake.
Hata hivyo, Kocha wa Wanderers, Vanni Sartini, ni moja ya watu waliopambana kuhakikisha timu hiyo inampata nyota huyo na kama atafanya vizuri huenda akanunuliwa moja kwa moja.
Akimzungumzia mshambuliaji huyo mwenye miaka 21, Sartini, alisema: “Cyprian amekuja kuleta changamoto kwa wapinzani kutokana na umbo lake, urefu na kasi.
“Anaweza kupita katikati ya mabeki, kushinda mipira ya juu, kufunga kwa miguu yote miwili na kushirikiana vizuri na kiungo wa kati. Ni mshambuliaji wa kisasa anayefanya mazoezi kwa bidii na ana uzoefu wa Whitecaps na timu ya taifa ya Tanzania.”
Baada ya uhamisho huo, Kachwele alisema: “Nafurahi kujiunga na kikosi cha Halifax na kuanza kufanya kazi na timu, natarajia kucheza mbele ya mashabiki wa timu hii na pia kupata fursa ya kufanya kazi tena na kocha Vanni.”
Kwa mara ya kwanza kocha huyo alifanya kazi na Kachwele mwaka 2023 alipojiunga na Vancouver Whitecaps akitokea Azam FC.
