Global Publishers
March 20, 2026
0 Comments
Waislamu wa Afrika Mashariki wanatarajiwa kuadhimisha sikukuu ya Eid-ul-Fitr siku ya leo Ijumaa Machi 20, 2026 kufuatia kuonekana kwa mwezi mpevu jioni ya Alhamisi, tukio linaloashiria kumalizika kwa mwezi mtukufu wa Ramadhani.
Nchini Kenya, Kaimu Kadhi Mkuu Sukyan Hassan alithibitisha kuwa mwezi huo umeonekana katika maeneo mbalimbali, huku ushahidi wa uhakika ukitolewa kutoka Kaunti ya Kwale, hasa eneo la Ramisi.
Akizungumza kupitia Ofisi ya Kadhi Mkuu, alisema kuwa watu watatu waliuona mwezi huo kwa nyakati zinazokubalika kisheria, na ushuhuda wao kuthibitishwa na viongozi wa dini wa eneo husika.
“Mwezi mpevu unaoashiria mwanzo wa mwezi wa Shawwal umeonekana kwa mafanikio jioni hii katika maeneo mbalimbali nchini. Ushahidi uliopatikana unakidhi matakwa ya Kiislamu,” alisema.
Kwa mujibu wa tangazo hilo, kuonekana kwa mwezi huo kunamaanisha kuwa Ramadhani umefikia tamati rasmi baada ya siku 29 za mfungo, na kesho yake kuwa siku ya kwanza ya mwezi wa Shawwal pamoja na maadhimisho ya Eid-ul-Fitr.
Eid-ul-Fitr ni miongoni mwa sikukuu muhimu zaidi kwa Waislamu duniani, ikiashiria mwisho wa kipindi cha mfungo wa Ramadhani, ambapo waumini hujihusisha na ibada, sadaka, na matendo ya huruma.