Global Publishers
March 21, 2026
0 Comments
Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Iringa, imemhukumu kifungo cha miaka miwili jela Sajenti Rogers Mmari baada ya kupatikana na hatia ya kosa la kuua bila kukusudia lililosababisha kifo cha Nashon Kiyeyeu (23).
Hukumu hiyo imetolewa Machi 19, 2026 na Jaji Angaza Mwipopo baada ya kuridhika na ushahidi uliothibitisha kuwa mshtakiwa alihusika na tukio hilo lililotokea Desemba 14, 2024 katika eneo la Ipogoro.
Mahakama ilieleza kuwa mshtakiwa, akishirikiana na mgambo Thomas Mkembela, alimpiga marehemu aliyedaiwa kuhusika na wizi wa simu, hali iliyosababisha majeraha makubwa na kifo chake.
Aidha, ilibainika kuwa baada ya tukio hilo mshtakiwa alikimbilia Moshi kabla ya kukamatwa na kurejeshwa Iringa. Mahakama pia ilibaini hakukuwa na kumbukumbu ya mtuhumiwa katika daftari la mahabusu kituo cha Polisi Ipogoro.
Jaji Mwipopo alisema ushahidi haukuonesha nia ya moja kwa moja ya kuua, hivyo kumtia hatiani kwa kosa la kuua bila kukusudia chini ya vifungu vya sheria na kumpa adhabu hiyo.
Familia ya marehemu imeeleza kutoridhishwa na hukumu hiyo, huku wananchi wakitoa maoni tofauti kuhusu uzito wa adhabu hiyo.